Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kwa mapro hawa, Simba imeipiga bao Yanga

Morrison Ntibazonkiza Kwa mapro hawa, Simba imeipiga bao Yanga

Sat, 2 Dec 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Kuanzia miaka ya 2000 kuna wachezaji wengi wa kigeni ambao wamekuja kuzitumikia klabu za Simba na Yanga, na kufanya mambo makubwa, lakini kati ya timu hizo mbili huenda kuna moja imefaidika zaidi na huduma zao ama zimelingana.

Mwanaspoti linakuchambulia baadhi ya mapro hao na kile walichokifanya kwenye timu hizo huku mastaa wa zamani wakitoa neno kuhusiana na hilo.

EMMANUEL OKWI (UGANDA)

Staa wa zamani wa Simba, Emmanuel Okwi kwa mara ya kwanza alijiunga na timu hiyo (2009-2013) kisha akaondoka kwenda Etoile du Sahel (2013) ambako vigogo hao walimuuza kwa dola 300,000 zaidi ya Sh600 milioni.

Baada ya kushindwa kupata nafasi ya kucheza kwenye timu hiyo, Okwi alirejea katika klabu iliyomlea ya SC Villa ya Uganda mwaka huo huo (2013) ingawa baadaye akajiunga Yanga (2013/14) na (2014/2015) akarejea tena Simba.

Baadaye Okwi aliondoka tena Simba na kujiunga Sonderjyske (2015/17) ya Denmark, lakini maisha ya huko yalimshinda akaomba kuondoka na kurudi Villa na kisha 2017/19 akarudi Simba kabla ya msimu wa 2019/20 kuondoka kwenda Al Ittihad na ndoa ya Simba na Okwi iliishia hapo akiwa amerudi mara tatu kuitumikia.

Msimu wake wa mwisho Simba, Okwi alimaliza mfungaji bora wa mabao 19. Kutokana na muda mwingi aliyoitumikia Simba, hilo linathibitisha ndio waliofaidi zaidi huduma yake kuliko Yanga aliyoichezea nusu msimu.

HAMIS KIIZA (UGANDA)

Kwa mara ya kwanza kuichezea Yanga ilikuwa (2011-2015), ambako alicheza kwa mafanikio makubwa, jambo lililowashawishi Wanamsimbazi kutamani huduma yake na akajiunga nao 2015/16).

Japokuwa Simba alicheza msimu mmoja, huduma yake uwanjani haikuwa ya kinyonge alikuwa kinara wa mabao 19 ya timu yake, huku mfungaji bora wa Ligi Kuu akiwa Amissi Tambwe aliyemaliza na mabao 21.

Yanga ilifaidi zaidi huduma yake kwani ndani ya miaka mitatu aliyokaa na timu hiyo kwenye Ligi Kuu alifunga jumla ya mabao 34.

Kiiza aliwahi kuzungumzia hilo: “Yanga nilicheza kwa muda mrefu kuliko Simba, nadhani ndio waliofaidika na mimi na maisha yangu ya kiuchumi kwa asilimia kubwa niliyapata Yanga.”

AMISSI TAMBWE (BURUNDI)

Msimu mmoja aliocheza Simba (2013/14) alimaliza kinara wa mabao 19 kwenye Ligi Kuu, moto wake ni kama ulizidi baada ya kuhamia Yanga ambako alifunga si chini ya mabao zaidi ya 60 kwenye Ligi Kuu.

Mchezaji huyo anasema: “Ni kwasababu Simba nilicheza msimu mmoja ningecheza muda mrefu kama Yanga ningefunga sana, ila iliyofaidika na huduma yangu ni Yanga.”

SAIDO NTIBAZONKIZA

Baada ya Yanga kumsajili kiungo mshambuliaji Said Ntibazonkiza ‘Saido’ msimu wa 2020-22 alifanya vizuri, kisha akaibukia Geita Gold ambako alifunga mabao manne kabla ya kujiunga na Simba ambako alifunga mabao 13 hivyo akamaliza kinara wa mabao 17 na asisti 14.

Kiwango chake kimezifaidisha timu hizo, ukiachana na msimu huu ambapo Simba inaonekana kama wachezaji wana morali ya chini na huenda mambo yakabadilika kutokana na ujio wa kocha mpya Abdelhak Benchikha.

Saido akiwa Yanga, alikuwa miongoni mwa wachezaji walioipa ubingwa wa Ligi Kuu Bara msimu wa 2021/22 pamoja na ubingwa wa Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC).

BERNARD MORRISON (GHANA)

Yanga ndio ilikuwa ya kwanza kumsajili winga Bernard Morrison 2020, kisha akajiunga na Simba 2020/22 akarejea tena Yanga 2022/23, kiwango alichokionyesha kwenye timu hizo hakikutofautiana sana, isipokuwa akiwa na Wanajangwani aliwafunga Wanamsimbazi kwenye mechi ya dabi iliyochezwa Machi 8, 2020.

Morrison ametwaa ubingwa katika timu zote mbili alizozichezea kwa nyakati tofauti.

HARUNA NIYONZIMA

Kiwango alichokionyesha Yanga, baada ya kusajiliwa msimu wa 2011-2017 kilikuwa cha juu, tofauti na alivyocheza Simba 2017-2019 ambapo aliamua kurejea tena Jangwani 2020/21.

Niyonzima akiwa Yanga aliisaidia timu yake kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Bara mara tatu mfululizo na alipokwenda alipojiunga Simba alichukuwa ubingwa wa ligi mara mbili  mfululizo na kuandika rekodi ya kibabe ya kutwaa ubingwa wa bara mara tano mfululo. Hata hivyo, ‘Fabregas’ alipokuwa Simba hakuwa katika ubora kama aliokuwa nao pale Yanga.

WAONAVYO WA ZAMANI

Aliyekuwa beki wa klabu hizo kongwe, Godwin Aswile ‘Scania’ anasema kinachomshangaza ni Simba na Yanga kugombania wachezaji wa kigeni na baadhi yao anawaona hawana utofauti na wazawa.

“Kitu kinachonishangaza ni kuona mapro wanaong’ang’aniana nao ni wa kawaida na sio kama kipindi chetu walikuwa hakuna wachezaji wa kigeni, sisi tulijituma hata wakija ni wale ambao hata sisi wenyewe tunajua wazi kwamba ni watu wa kazi na kuamua matokeo nyakati ngumu, sasa mnakuwa na wageni ambao kwenye nyakati ngumu hakuna wanachokifanya,” anasema.

Mchezaji mwingine wa zamani wa Simba, Frank Kasanga ‘Bwalya’ anasema; “Mapro wanaocheza klabu hizo mbili wanakuwa na uwezo na anaona soka ni biashara hivyo mchezaji anawaniwa na watani hao kutokana na kiwango anachoonyesha akiwa timu moja wapo.

“Mfano Okwi naona Simba ilimfaidi zaidi huduma yake, maana hata alivyouzwa ilipata pesa, Tambwe Yanga imefaidi zaidi kwa maana ilikaa naye muda mrefu, Saido kazifaidisha timu zote mbili, jambo la msingi ni wachezaji hao kujitambua.”

Chanzo: www.tanzaniaweb.live