Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kwa jambo hili, Azam heshima na maokoto

Azam Complex Rev Uwanja wa Azam Complex

Sun, 8 Oct 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Kuna ishu ya heshima kwa kuwa na muda mfupi katika ulimwengu wa soka, lakini pia Azam FC imezipiga bao klabu kongwe za Simba na Yanga kwa kumiliki uwanja wa kisasa.

Azam ni miongoni mwa timu chache nchini zenye kumiliki viwanja vyake zenyewe zikiwamo Mtibwa Sugar, Ihefu FC na nyingine, lakini klabu hiyo imefunika kutokana na Uwanja wa Azam Complex kutumika hadi kwenye mechi za kimataifa.

Kama kungekuwa na ligi ya kumiliki viwanja, basi Azam FC ingekuwa bingwa kwa kunyakua kitita cha Sh100 milioni kama zile inazopewa bingwa wa Ligi Kuu kutoka kwa wadhamini wakuu - Benki ya NBC.

Kwa sasa uwanja huo unatumika kwa baadhi ya timu za ndani na nje ya nchi kutokana na Uwanja wa Mkapa kufanyiwa marekebisho.

Hii ni makala ya Azam FC inayoumiliki Uwanja wa Azam Complex, inavyojitengenezea heshima kubwa ndani na nje ya mipaka ya Tanzania, lakini ikivuna maokoto ya maana ikizifunika hadi Simba na Yanga zenye umri wa miaka zaidi ya 80 na ambazo pengine zingepaswa kwa sasa kuwa na viwanja binafsi.

MSHIKO ULIVYO

Kuupata Azam Complex kwa timu za ndani ambazo zinafanyia mazoezi zinalazimika kutoboka Sh600,000 kwa mchana na Sh1.5 Milioni kwa usiku.

Kwa matumizi ya mechi kwa timu za ndani ni Sh5.9 milioni kwa mchana na hata usiku, lakini kwa timu za nje zenyewe zinatozwa zaidi ya Sh2.5 milioni kwa mazoezi na hata mechi zikitofautiana kiasi flani kidogo cha fedha.Kwa hesabu za haraka makadirio yanaonyesha hadi sasa kiasi cha Sh91 milionizimeingia Azam kwa timu za ndani na nje zilizoutumia uwanja huo - fedha hizo zikitokana na mechi kadhaa zilizopigwa Azam Complex.

YANGA

Yanga ni miongoni mwa timu zilizoutumia Uwanja wa Azam Complex kwenye mechi zote tatu za Ligi Kuu na michuano ya kimataifa.

Baada ya Uwanja wa Mkapa kufungwa matumizi, Yanga ilianza kucheza na KMC, JKT Tanzania ilizoshinda kwa mabao 5-0 kila moja kisha kuifumua Namungo kwa bao 1-0, ikiutumia uwanja huo wa Azam Complex.

Kwenye michuano ya kimataifa Yanga imeutumia Uwanja wa Azam kama dimba la nyumbani dhidi ya Asas ya Djibouti kwenye hatua ya awali na kuifunga mabao 5-1 na kuitoa kwa jumla ya mabao 7-1 kwani mchezo wa awali, Wadjibouti ndio waliouomba kuutumia kama uwanja wao wa nyumbani na kulala 2-0. Mechi ya mwisho ilikutana na Akl Merrikh ya Sudan na kuifunga bao 1-0 na unaambiwa kila mechi moja ya kimataifa, Yanga imelazimika kulisha Sh 5.0 na kwa hesabu za mechi hizo sita ina maana imeiingizia Azam FC zaidi ya Sh 35.4 milioni.

SIMBA

Bingwa wa Ngao ya Jamii, Simba imeutumia Uwanja wa Azam kwa mechi moja tu ya kimataifa hadi sasa iliporudiana na Power Dynamos ya Zambia katika raundi ya pili ya Ligi ya Mabingwa Afrika, kwa vile mechi za Ligi Kuu imekuwa ikiutumia Uwanja wa Uhuru.

Katika mechi hiyo pekee ambayo Simba imeutumia Azam Complex, imeambulia sare ya 1-1 na kuvuka kwenda makundi kwa faida ya bao la ugenini baada ya awali kutoka sare ya 20-2 ugenini mjini Ndola, Zambia na imekamuliwa Sh 5.9 milioni kwa mechi hiyo pekee.

SINGIDA FG

Singida Nig Stars ni miongoni mwa timu changa nchini ambazo zilifanya vizuri msimu uliopita wa Ligi Kuu ikimaliza nafasi ya nne.

Nafasi hiyo iliwakatia tiketi ya kushiriki kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika pamoja na Azam FC ambao walitolewa hatua za awali na Bahir Dar Kenema kwa mikwaju ya penati 4-3 baada ya kutoka sare ya mabao 3-3. Singida imetumia Uwanja wa Azam Complex kucheza mechi mbili za kimataifa pamoja na mazoezi mara mbili ambayo gharama yake ni Sh600,000 kwa siku.

Ilianza na JKU ya Zanzibar hatua za awali na kuifunga kwa mabao 4-2 kisha mchezo wa kwanza kufuzu makundi dhidi ya Future FC ya Misri kwa bao 1-0.

Kwa matumizi ya mechi mbili na mazoezi mara mbili Azam imevuna Sh 13 milioni kutoka kwa Singida hadi sasa kwa mechi hizo, kwa vile kwenye Ligi Kuu timu hiyo inautumia Uwanja wa Liti, uliopo Singida.

BUMAMURU FC

Bumamuru FC ya Burundi iliuchagua Uwanja wa Azam Complex kama uwanja wake wa nyumbani katika mechi ya kwanza hatua ya awali ya Ligi ya Mabingwa dhidi ya Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini na Azam imeingiza Sh12.5 milioni.

AS ARTA SOLAR

Timu hiyo iliuchagua uwanja huo katika mechi ya kwanza za Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Zamalek.

Klabu hiyo ambayo makao yake makuu ni Djibouti ilitumia kucheza mechi ambayo ilitozwa Sh 12.5 milioni.

TWIGA STARS

Timu ya taifa ya wanawake ‘TwigaStars’ ambayo ilikwenda Yamoussoukro kwenye mchezo wa kwanza kufuzu Michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika kwa Wanawake (WAFCON) dhidi ya Ivory Coast iliporejea iliutumia uwanja huo.

Mchezo huo wa pili ulipigwa Chamanzi Septemba 26 ambapo Twiga iligharimika kiasi cha Sh 5.9 milioni.

SERENGETI GIRLS

Timu ya taifa ya wanawake chini ya umri wa miaka 17 Serengeti Girls iliutumia pia uwanja huo kukipiga na Morocco katika mchezo wa kimataifa wa kirafiki.

Uwepo wao uliinufaisha Azam kuingiza kiasi cha Sh 11.8 milioni kwa michezo yote miwili waliyocheza.

POPAT ANENA

Akizungumza na Mwanaspoti, Mkurugenzi Mtendaji wa Azam FC, Abdulkarim Amin ‘Popat’ anasema hadi sasa timu hiyo imeingiza zaidi ya Sh100 milioni kutokana na uwanja wake kutumiwa na timu za ndani na nje ya nchi.

Popat anasema bajeti ya timu hiyo kwa mwaka kupitia uwanja huo inategemea na mechi zinazochezwa ambazo hadi sasa kwa kukadiria zaidi ya Sh100 milioni zipo kibindoni na huenda zikaongezekana kama klabu za Tanzania na zile za kimataifa zitaendelea kuomba kuutumia, jambo ambalo kwao ni faida kutokana na uwekezaji walioufanya.

“Hadi sasa timu yetu imeingiza kwa kukadiria milioni 100 kupitia Azam Complex na hizi ni hesabu za msimu huu. Lakini mechi kibao zimekuwa zikitumika kwenye uwanja huu na hata sasa tunaamini kuna michezo mingine itakuwa ikifanyika hapa. Ni kitu cha kufurahia kwa uwekazaji uliofanyika, lakini inategemea na mechi zinazochezwa pia, bajeti na bei zinabadilika kutokana na mechi zenyewe,” alisema Popat.

Chanzo: Mwanaspoti