Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kwa heri Profesa wa Kombe la Dunia

Jorge Lobo Zagallo 5967 Kwa heri Profesa wa Kombe la Dunia

Tue, 9 Jan 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Rasunda Stadium, Manispaa ya Solna, Stockholm, Brazil "Canary Squad", walishinda ubingwa wa kwanza, Kombe la Dunia. Ni mwaka 1958. Walicheza fainali dhidi ya wenyeji, Sweden.

Fainali za Kombe la Dunia 2022 zilipomalizika, ni binadamu wawili tu waliokuwa hai, kikosi cha Brazil kilichobeba World Cup 1958; Mário Jorge Lobo Zagallo na Edson Arantes do Nascimento Pele, ambaye alikuwa dogo kwa kila mtu.

Pele alikuwa na umri wa miaka 17, alipocheza, alipofanya mabalaa na kubeba ndoo 1958.

Desemba 29, 2022, ikiwa ni siku 11 tangu kumalizika World Cup 2022, Pele alifariki dunia. Hivyo, binadamu pekee aliyekuwa amesalia hai kwenye kikosi cha Brazil - World Cup 1958, alikuwa Zagallo. Januari 5, 2024, Zagallo naye alivuta pumzi ya mwisho. Brazil ya World Cup 1958, imemalizika.

Brazil, leo na siku nne mfululizo, bendera ya taifa inapepea nusu mlingoti. Wanamwomboleza mwanasoka mwenye mchango mkubwa mno kwenye mafanikio yao. Wameshinda World Cup mara tano. Zagallo amehusika moja kwa moja mara nne.

Mwaka 1958. Kisha, 1962, fainali za Chile, Brazil ikimkosa Pele kwa sababu alikuwa majeruhi, Zagallo mshambuliaji wing ya kushoto, alikuwa anarudi nyuma kukaba na kupandisha mashambulizi. Ulikuwa mtindo mpya wa uchezaji wakati huo. Brazil ikabeba World Cup mara mbili mfululizo.

Mwaka 1965, Zagallo alistaafu kucheza soka. World Cup 1970, fainali za Mexico, Zagallo akiwa na umri wa miaka 38, alikuwa Kocha Mkuu, akaipa Brazil World Cup ya tatu. Akawa binadamu wa kwanza kushinda World Cup akiwa mchezaji, vilevile kocha.

World Cup 1994, fainali za Marekani, Zagallo alikuwa mratibu wa timu ya Brazil, ikabeba ndoo ya nne ya World Cup. Hivyo, Zagallo aliisaidia Brazil kubeba World Cup mara mbili akiwa mchezaji, moja kocha mkuu na moja mratibu.

Brazil ilibeba World Cup ya tano mwaka 2002, Zagallo hakuwa sehemu ya kikosi hicho. World Cup 1974, Zagallo akiwa kocha mkuu, aliifikisha Brazil nusu fainali. World Cup 1998, aliiwezesha kushika nafasi ya pili.

Niliushuhudia 'uchawi' wa Zagallo kwa macho yangu World Cup 1998. Brazil ile ya Zagallo ilivutia mno kuitazama. Aliitwa Profesa. Alisheheni maarifa ya soka.

Kila nafsi itaonja mauti. Usiku mwema Profesa wa World Cup.

Ndimi Luqman MALOTO

Chanzo: www.tanzaniaweb.live