Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kwa heri Mayele mwenye jina, mambo makubwa

Mayele 0657 Facebook Mayele

Tue, 25 Jul 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Kama kuna uhamisho unasubiriwa kwa hamu sana kuhitimisha dirisha hili, basi ni taarifa za hatima ya mshambuliaji hatari wa Yanga, Fiston Kalala Mayele.

Hadi sasa bado haijawekwa bayana kama mshambuliaji huyo kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DR Congo) atabakia na klabu yake ya sasa ya Yanga kumalizia mwaka wa mwisho wa mkataba wake kama tulivyoelezwa kuwa aliongeza mwaka mmoja, au ataondoka kutafuta majani ya kijani zaidi baada ya kuwa Tanzania kwa miaka miwili.

Habari kwamba klabu ya Arabuni zinamsaka kwa udi na uvumba ndizo zinatawala, huku kukiwa na taarifa nyingine kando kuwa mshambuliaji huyo mwenye miaka 28 bado anamilikiwa na Maniema ya DR Congo ambayo ndiyo inaweza kuamua hatima yake.

Liwalo lolote lile, Mayele ataondoka au atabaki, lakini anaacha somo kubwa kwa wachezaji wengi, hasa vijana wanaotakiwa kujifunza mengi kutoka kwa kaka zao, hasa wachezaji wakubwa kama Mayele.

Katika mwaka wake wa pili Yanga, Mayele amedhihirisha thamani yake na kuongeza ukubwa wake, si tu katika soka la Tanzania, bali na Afrika nzima.

Amemaliza akiwa mmoja wa washambnuliaji wawili waliofunga mabao 17 msimu ulioisha, huku akiiongoza Yanga kufika fainali ya Kombe la Shirikisho, ikiwa ni mara ya kwanza kwa klabu ya Tanzania kufikia hatua hiyo tangu CAF ilipofanya maboresho ya michuano yake.

Wakati ikielekea fainali hiyo, Mayele alifunga mabao saba yalkiyoiwezesha Yanga kulingana kwa USM Alger ya Algeria, lakini ikashindwa kutwaa ubingwa wa kwanza Afrika kwa timu ya Tanzania kutokana na sheria ya bao la ugenini. Yanga ilifungwa mabao 2-1 katika mechi ya kwanza jijini Dar es Salaam, lakini ikaishangaza Afrika kwa kushinda bao 1-0 nchini Algeria na hivyo matokeo ya jumla kuwa mabao 2-2. Hiyo pia ni rekodi kwa klabu za Tanzania.

Hayo pekee hayamfanyi Mayele kuwa mchezaji mkubwa, sifa ambayo iliibua mjadala mkubwa msimu uliopita kutokana na baadhi ya watendaji wa klabu kuhoji ukubwa wake, wakinyooshe kidole kidadi ya mabao aliyofunga msimu uliopita kulinganisha na wachezaji wengine waliofunga kuanzia mabao 20 katika msimu mmoja.

Mayele aliweza kuweka chapa yake ya kipekee kutokana na jinsi ambavyo amekuwa akionyesha kutobweteka na sifa kemkem alizokuwa akipambwa na mashabiki wa Yanga kutokana na mabao yake, kiasi cha staili yake ya kushangilia mabao kusambaa sit u ndani ya Tanzania au ndani ya soka pekee, bali nje na maeneo mengine nje ya mchezo huu maarufu.

Staili hiyo iliigwa na wachezaji wengine na mashabiki, lakini zaidi ni jinsi ilivyoenea kwenye bendi za muziki wa dansi, kwaya za dini na nyinginezo hadi ndani ya majeshi.

Ni sifa ambazo zingeweza kumfanya abweteke au kuwa limbukeni badala ya kuongeza bidii awe mzuri zaidi na kuongeza thamani yake.

Uwanjani hakuwa na mechi ndogo ambayo ingeweza kusababisha aonyeshe kiwango kidogo. Kwake kila mechi ilikuwa ni fainali na kitendo cha mabeki wengi kumpania, kilisababisha afuatiliwe kwa makini na mashabiki kila alipocheza na hivyo kuwa bora zaidi kadri siku zilivyokwenda.

Haikuwa ajabu kwamba katika moja ya mechi za mwisho wa msimu, Mayele alionyesha kasi ya ajabu iliyoshangaza karibu bara zima la Afrika. Wakati Yanga ikihitaji ushindi muhimu ugenini nchini Afrika Kusini, na ikiwa imeshafunga bao la kuongoza, Mayele alitanguliza mpira mbele kiasi ambacho isingeweza kufikirika kuwa angeweza kumzidi kasi beki aliyekuwa mbele yake.

Lakini alifanya hivyo, alitoka kasi na kumpita beki wa Marumo Gallaxy kabla ya kutoa pasi ya mwisho kwa Kennedy Musonda aliyefunga bao zuri la pili kuiwezesha Yanga kwenda fainali ya kwa ushindi wa jumla ya mabao 4-1. Alikuwa amezima ubishi kwa waliokuwa wanahoji ukubwa wake.

Ukubwa wake haukuishia katika hayo tu. Wakati fulani Kocha Nasredine Nabi alimuelezea Mayele kama mmoja wa wachezaji wenye nidhamu ya hali ya juu. Alisema pamoja na sifa zote anazopata, Mayele bado aliendelea na nidhamu yake binafsi, nidhamu ya kitimu ya kufika kila eneo kwa wakati, na bila shaka nidhamu ya mbinu za kimchezo, ambayo huwashinda wachezaji wengi.

Ushuhuda huo umetolewa pia na wachezaji wenzake waliovutiwa na nidhamu na juhudi zake mazoezini.

Lakini hata kwa ambao tumekuwa tukimuangalia kwenye mechi, tumemshuhudia akikubali maamuzi ya refa bila ya kubnishana na waamuzi mara kwa mara. Hata anapochezewa rafu, ni nadra sana kumuona anahamaki. Ni mara moja tu ndipo alipoonyesha hasira baada ya kugongwa kwa makusudi.

Hizi ni sifa ambazo si mara nyingi zinakuwa kwa wachezaji wengi. Matatizo mengi ya wachezaji wadogo wanaofikiriwa kuwa wakubwa ni nidhamu binafsi, ya kitimu nay a mbinu za mchezo, au ya kufuata maelekezo ya mbinu za kocha kulingana na mchezo.

Wakati wa uhamisho ndio ambao wachezaji huonyesha rangi zao halisi, hasa usumbufu. Wapo wanaovujisha habari kuhusu uhamisho wao kwa lengo la kutaka klabu yake istuke na hivyo kuongeza dau. Wako ambao hususa hata shughuli za timu kushinikiza wahame na wako ambao huandika mengi kwenye akaunti zao za mitandaoni kuashiria kuwa wanaelekea kuondoka kwenye klabu zao za wakati huo.

Kila mara anapofuatwa na waandishi ambao hutaka kujua kituo chake kinachofuata, Mayele huwarudisha kwa uongozi wa Yanga kwamba wao ndio wanajua hatima yake. Zimeshatolewa habari kwamba vikao kadhaa vimefanyika kati ya menejimenti ya Mayele na viongozi wa Yanga, lakini kunaonekana weledi mkubwa katika kulinda kile kinachojadiliwa.

Hili pia linaongeza ukubwa na somo kwa wachezaji wengine, hasa wa Tanzania ambao hujenga urafiki mkubwa na waandishi wa habari na baadaye kuvujisha habari zao ili kuwatia joto viongozi na kushinikiza maslahi yao wakijua mashabiki watawakaba koo viongozi wafanye vile ambavyo mcheza anataka.

Kwa mchezaji mwenye weledi, stahiki zake huzungumzwa mezani na si kwa kutafuta huruma za mashabiki. Kadri anavyokuwa na watu wazuri katika kujadili mkataba, ndivyo maslahi yake yanavyokuwa bora zaidi kiasi cha kuzuia shauri lake kuisha kwa migomo.

Habari za Mayele zimekuwa siri kubwa na hivyo kusababisha ubashiri mkubwa wa hatima yake, kiasi cha habari hizo kuchosha mashabiki, ambao nadhani sasa wanataka taarifa rasmi kuwa ataondoka au la.

Pengine Mayele ataondoka. Kama ndivyo basi kwa heri Mayele. Umesaidia kulichamsha soka la Tanzania, umesaidia kulitangaza soka letu, umekuwa somo zuri kwa wachezaji, viongozi na mashabiki, umefundisha jinsi ya kutengeneza chapa kwa tabia, jitihada uwanjani, nidhamu na kutobadilisha staili ya ushangiliaji hadi ikatikisa vichwa vya kila mmoja.

Soka la Tanzania halina budi kujivunia kuwa na Mayele kwa kipindi cha miaka miwili. Na ligi kubwa husaka wachezaji wa aina hii. Kitendo cha Rais Emmanuel Macron kumpigia simu Kylian Mbappe kutaka abakie PSG msimu uliopita kililenga kulinda chapa ya Ligue 1.

Ndivyo ambavyo Serie A iliona umuhimu wa kuwa na Christian Ronaldo na ndivyo La Liga inavyoona umuhimu wa kuwa na Mbappe. Tunahitaji wachezaji wakubwa na wenye mambo makubwa.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live