Agosti 4, 2017 klabu ya Paris Saint-Germain (PSG) ya jijini Paris Ufaransa ilitangaza kuinasa rasmi saini ya staa wa kibrazili Neymar Jr akitokea klabu ya Barcelona, mwezi mmoja baadae Septemba 1, 2017 klabu hiyo ya PSG ikatangaza usajiri mwingine wa kinda wa miaka 18 Kylian Mbappe kutoka klabu ya Monaco.
Mastaa hawa wawili wa Kifaransa na Kibrazili walifanikiwa kujenga muunganiko mzuri wakiwa dimbani na hata kwenye maisha ya nje ya dimba.
Uhusiano kati ya Mbappe na Neymar ulianza kupungua taratibu baada ya uhamisho wa staa Muargentina na bingwa mara saba wa tuzo za Ballon d’or Lionel Messi akijiunga kutokea Barcelona mwishoni mwa msimu 2021 katika dirisha kubwa la usajiri barani ulaya ambapo Neymar alionekana kuwa karibu zaidi na Messi.
Tetesi za wawili hawa kuhusishwa na kutokuwa na maelewano zilipamba moto zaidi baada ya vyanzo vya habari nchini Ufaransa kuweka wazi kuwa Mbappe alikataa ofa kutoka klabu ya Real Madrid aliyohisishwa kujiunga nayo na kusaini mkataba mpya ndani ya PSG uliompa nguvu ya kufanya maamuzi dhidi ya wachezaji wenzake ndani ya klabu na mwanzoni mwa msimu huu 2022/2023 Mbappe alionesha utayari wa kutaka Neymar aondoshwe klabuni hapo.
Vyanzo hivyo viliendelea kwa kusema kabla ya kusaini mkataba mpya Mbappe hakuwa na furaha ndani ya klabu kutokana na kuwa na ushawishi mdogo sana kwa klabu na wachezaji wenzake kulinganisha na Neymar ambaye alionekana kuwa na ushawishi mkubwa ndani nani na nje ya uwanja, jambo ambalo halikumpendeza Mbappe.
Hata hivyo kupitia ukurasa wake wa twitter Neymar alionekana ku-like mtiririko wa posti mbalimbali za wadau wa soka zilizoelezea udhaifu na mapungufu yaliyopo kwenye mkataba mpya wa Mbappe aliosaini na PSG kitu ambacho kiliibua taharuki na kuwaaminisha mashabiki uwepo wa ugomvi baina yao.
Vuguvugu la mastaa hawa lilienda mbali zaidi hadi siku ya mechi ufunguzi wa msimu Agosti 13,2022 ambapo PSG alivaana na klabu ya Montpellier na kuibuka na ushindi wa mabao 5-2 ambapo Neymar alionekana akifoka baada ya Mbappe kukosa penati ya kwanza ya mchezo na tukio jingine lilionekana pale wawili hao walionekana wakigombania kupiga mpira wa adhabu ya penati ya pili ambayo baadae Neymar alifanikiwa kupiga na kufunga penati hiyo.
Hata hivyo baada ya mechi Meneja alipoulizwa kuhusu tukio hilo aliwaambia waandishi kuwa ni jambo la kawaida kwake (Neymar) kuwa kusikitishwa na ubora mdogo wa kiwango unaooneshwa na wachezaji wenzake na wakati huohuo kiungo mkongwe Marco Verratti aliongeza kwa kusema “Alifoka kidogo lakini hiyo ni kawaida.Ni mchezaji mzuri anayetaka kuleta mabadiliko. Ni vizuri anapokuwa na hasira, inamaana anajali hii timu”.
Mama yake Kylian Mbappe, Fayza Lamari alinukuliwa akisema “hili suala lipo kwenye mikono ya klabu ya PSG kwasasa na kila kitu kinaendelea vizuri”.
Mshauri wa klabu Luis Campos naye ameripotiwa akiwataka mastaa hawa kuzungumza juu ya tofauti zao ndani ya klabu na waache kuanika wazi tofauti zao mtandaoni na kuibua hofu na taharuki kwa mashabiki.