Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kwa Yanga hii mtateseka sana.... Mayele, Aziz Ki, Morrison wana jambo lao

Mayele Mateso Mayele

Sat, 30 Jul 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

FISTON Mayele amemaliza utata kwa kukubali kusaini mkataba mpya wa mwaka mmoja na sasa atakuwa kikosini hadi 2024, lakini usajili wa Stephane Aziz KI na Bernard Morrison ‘BM33’ umewafanya wakongwe kushindwa kujizuia wakisema sasa jamaa atafunga sana.

Msimu uliopita Mayele alimaliza kinara wa mabao wa timu hiyo akifunga mabao 16 nyuma ya George Mpole wa Geita Gold aliyebeba tuzo ya Mfungaji Bora wa Ligi Kuu, huku mengi yakitokana na asisti za mabeki, kitu ambacho inaelezwa safari hii atapata ahueni kwa kina BM33.

Mayele alibakiza mkataba wa mwaka mmoja kati ya miwili aliyoingia na Yanga msimu uliopita na inaelezwa amekubali kuongeza mwaka kusalia kikosini baada ya kufanya kikao na bilionea Ghalib Said ‘GSM’ ikiwemo kuboreshewa mshahara na marupurupu mengine.

Kama mambo yataenda vizuri maana yake ataendelea kuwa straika namba moja, huku nyuma na pembeni yake watakuwapo Aziz KI na BM33 wanaotajwa wamekuja kumrahisishia kazi ya kufunga tofauti na ilivyokuwa msimu uliopita.

Kuanza kikosini kwa Aziz Ki na BM33 kunawapa matumaini makubwa mastaa wa zamani na mashabiki wa Yanga, akiwamo Abedi Mziba ‘Tekero’ wakiamini kutaongeza nguvu katika safu ya ushambuliaji ambayo msimu uliopita ilimaliza na mabao 49 katika mechi 30.

Hata hivyo, uwepo wa nyota hao unaweza kufurahiwa zaidi na Mayele pengine kuliko mchezaji mwingine kikosini kutokana na uwezo mkubwa wa kupiga pasi za mwisho ambao unaweza kuwa faida kwa mshambuliaji huyo kutoka DR Congo.

Yanga sasa ina uhakika wa kutengeneza idadi kubwa za nafasi jirani na eneo la timu pinzani zinazoweza kuwa na faida kwa Mayele tofauti na msimu uliopita ambao licha ya kufunga mabao 16 Ligi Kuu hakupata huduma ya kutosha kutoka kwa viungo washambuliaji.

Takwimu za msimu uliopita zinaonyesha idadi kubwa ya mabao ya Mayele yalitokana na mchango wa wachezaji wa nafasi ya ulinzi, huku machache ya viungo washambuliaji tatizo ambalo Aziz Ki na Morrison wana kibarua cha kulitibu.

Kati ya mabao 16 ambayo Mayele alifunga manane yalitokana na pasi za mwisho za mabeki, matano kutoka kwa viungo washambuliaji na moja likifungwa na kiungo wa kati huku mengine yakitokana na makosa ya mabeki wa timu pinzani.

Djuma Shaban ambaye ni beki wa kulia ndiye alikuwa kinara wa kumlisha Mayele pasi za mabao ambapo alimuasisti mara tano akifuatiwa na kiungo mshambuliaji, Saido Ntibazonkiza aliyeasisti mara tatu kwa Mayele.

Asisti nyingine za Mayele zilitoka kwa kiungo mshambuliaji Feisal Salum ‘Fei Toto’ na beki wa kushoto, Yassin Mustafa kila mmoja alimpa mbili huku beki kiraka Kibwana Shomari na kiungo Salum Abubakar ‘Sure Boy’ kila mmoja akipiga pasi moja ya mwisho.

Katika msimu uliomalizika Morrison na Aziz Ki walikuwa na takwimu bora za kupiga pasi za mwisho kuliko kiungo yeyote wa ushambuliaji Yanga kwenye mashindano mbalimbali.

Morrison ambaye alikuwa Simba alikuwa na pasi za mwisho sita ambapo tano zilikuwa za klabu Afrika na moja Ligi Kuu wakati Aziz Ki kwenye mechi 26 za mashindano alizoichezea Asec Mimosas alipiga pasi za mwisho nne.

MSIKIE TEKERO

Akizungumza kwa niaba ya wakongwe wenzake, Abeid Mziba ‘Tekero’ alisema anaamini msimu ujao Yanga itakuwa tishio zaidi kwenye ushambuliaji.

“Wachezaji waliosajiliwa ni wazuri na wenye uzoefu mkubwa. Ukiwatazama Morrison na Aziz Ki sio tu wanaweza kupiga pasi za mwisho, ila wana uwezo pia wa kufunga mabao hivyo kama wasipopata changamoto naamini watakuwa na msaada mkubwa kwenye timu,” alisema Mziba aliyesifika enzi zake akicheza kwa mabao ya vichwa.

Naye kocha wa Yanga, Nasreddin Nabi alisema anaamini usajili wa wachezaji hao hautamnufaisha Mayele pekee, bali timu nzima. “Nimefurahishwa kuona uongozi umefanyia kazi mapendekezo yangu ya kuwasajili wachezaji hawa kwani naamini katika uwezo wao watakuwa na msaada.”

Chanzo: www.tanzaniaweb.live