Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kwa Taifa Stars si vazi la taifa, ni maandalizi

Taifa Stars AFCON Vazi Kwa Taifa Stars si vazi la taifa, ni maandalizi

Mon, 15 Jan 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Macho ya Watanzania hivi sasa yameelekezwa Ivory Coast ambako timu yao ya taifa inashiriki fainali za Mataifa ya Afrika (Afcon 2023), hii ikiwa ni mara ya tatu kwa taifa hili kufuzu kucheza mashindano hayo makubwa barani Afrika.

Lakini, wakati wakisubiri Taifa Stars ishuke uwanjani keshokutwa Januari 17 itakapomenyana na Morocco, kumeibuka mjadala wa mavazi baada ya timu nyingine kuonekana zimevalia sare zinazoonekana zimebuniwa kwenye nchi zao, tofauti na timu nyingine ambazo ama huvalia suti za kimagharibi au suti za kimichezo.

Wakati Ghana wamewasili Ivory Coast wakiwa wamevalia fulana na juu yake wakijizungushia vile vitenge maarufu nchini humo za Kente, Guinea walivalia vazi mithili ya kanzu huku chini wakiwa wamevalia suruali, vipande vyote viwili vikishonwa kwa vitenge na Nigeria ambao ndio maarufu kwa mavazi yanayochukuliwa ni ya kitaifa kwa Afrika Magharibi, Senegal na Gambia wameibuka na sare ambazo zinaonekana ni ubunifu wa wazawa.

Ni mashati na suruali au kaptura ilioshonwa kwa kitambaa cha wax. Namibia pia wameshona sare zinazotokana na ubunifu wa wananchi hao, huku mashati na suruali hizo za bluu zikiwa zimewekwa nakshi za rangi za bendera ya nchi yao.

Nchi hizo na mataifa mengine yaliyozingatia fasheni katika ushiriki wao wa Afcon 2023 ambazo zinafanyika Januari 2024 kutokana na hali mbaya ya hewa katikati ya mwaka, zimenogesha mashindano hayo ambayo yanashirikisha nyota wanaoshirili ligi mbalimbali ulimwenguni, zikiwemo zile kubwa za barani Ulaya.

Kitu kilicho wazi ni kuwa hiyo haikutokea kwa bahati mbaya na si kwa sababu eti kuna vazi la taifa, kama baadhi ya watu wanavyojadili kiasi cha kutaka ziwekwe nguvu kwenye vazi la taifa ili Tanzania iwe na utambulisho. Hilo limefanyika kwa sababu kulikuwa na maandalizi na waliofanya waliona ukubwa na uzito wa kushiriki mashindano hayo ndio maana wakajipanga vizuri kuanzia kimpira hadi kimavazi.

Kwa bahati, karibu mataifa yote makubwa yameanzia kambi zao nchini mwao na si kuikimbiza timu yao nje ya nchi ambako zinachokipata huko ni uwanja kama vile wa Benjamin Mkapa, Amaan ama Azam Complex. Na kikubwa zaidi ni kuirahisishia timu kama Misri kupata mechi ya kirafiki nyumbani, hivyo kupata fursa ya kuwaonyesha wananchi wao jinsi walivyojiandaa kabla ya kuondoka kwenda Ivory Coast.

Ilikuwa ni muhimu kwa Shirikisho la Soka nchini (TFF) kuanzia kambi hapa nyumbani na kucheza mechi moja ya kujipima nguvu hapa Tanzania kabla ya wachezaji kusafiri kwenda Ivory Coast. Kuna sherehe ambazo huonekana kama si za maana, zile za kuagwa na viongozi na kukabidhiwa bendera. Zile zina uzito wake na humaanisha kitu kikubwa kwa wachezaji wanapoona serikali inaiangalia timu kwa macho mawili na ina matarajio makubwa kwao.

Kwa wachezaji ambao baadhi hawajawahi kuja hata Tanzania tangu wapate akili, hili lilikuwa ni jambo kubwa kwao kujua, si hisia za viongozi wa serikali pekee, bali hata umma wa Watanzania kwa kucheza mechi moja mbele yao au hata kuwaona mashabiki jinsi wanavyofuatilia timu yao mazoezini na hivyo kupata picha ya matarajio ya taifa kwao.

Timu ingekuwa hapa, suala la mavazi lingeweza kujitokeza au kuibuliwa na wadau wa mavazi kama Sheria Ngowi, ambaye amekuwa karibu na mchezo wa soka.

Timu ingekuwa hapa, sioni kama Rais Samia Suluhu Hassan angeshindwa kupata wazo la kuwaita Ikulu kula nao chakula na kuwaeleza matarajio yake na serikali yake. Na jinsi ya kwenda Ikulu ingezusha suala la sare.

Pengine baadhi wanaweza kusema cha muhimu ni timu kupata maandalizi mazuri, lakini uwakilishi wa nchi huambatana na mambo mengi, ndio maana wenzetu wamefikiria hata hayo mavazi maarufu nchini mwao wakijua kabisa watatikisa vyombo vya habari, kama ilivyofanyika, na nchi yao na utamaduni wake kutangazwa Afrika na duniani kwa jumla. Ni lazima tufikirie nje ya boksi wakati tunapopata nafasi kubwa kama ya kushiriki fainali za Mataifa ya Afrika, ambazo mwaka 2027 tutaziandaa kwa kushirikiana na Kenya na Uganda.

Kwa hiyo, Nigeria, Ghana, Senegal, Gambia, Guinea na nyingine hazikuvaa sare zile za kitamaduni kwa kubahatisha, bali zilikuwa na maandalizi ya kutosha yaliyowapa fursa ya kufikiria hata mavazi badala ya masuala ya kiufundi pekee. Hii ndio akili tunayotakiwa tuwe nayo na ndio maana pale shirikisho kuna idara tofauti kama ufundi, mashindano, masoko, habari, biashara na nyingine kwa ajili ya kila moja kuchangia nini kifanyike katika kila jambo linalofanyika.

Hizi ni idara ambazo pia zinatakiwa ziwe zinafanya ujasusi kujua suala kama fainali za mwaka huu zitajikita kwenye nini kulingana na mwenendo wa mambo mbalimbali duniani, kama suala la fasheni lilivyoteka fainali za mwaka huu.

Hata kama hatuna vazi la taifa, bado wadau wangeweza kufikiria waivike timu nguo gani ili kujitofautisha na nchi nyingine na hivyo kulitangaza taifa letu. Hayo yote hayawezi kufanyika bila ya kuwa na maandalizi jumuishi.

Chanzo: Mwanaspoti