Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kwa Simba hii kuna jambo! wapo kila kona

Simba Na Mashabiki Kwa Simba hii kuna jambo! wapo kila kona

Sat, 31 Aug 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Ligi Kuu Bara imesimama hadi Septemba 11, huku zikishuhudiwa mechi 13 zikipigwa na kufungwa jumla ya mabao 22, ilihali Simba ikitawala kila kona, japo timu sita zimesaliwa na viporo vya mechi moja moja kukamilisha michezo ya raundi ya pili ya ligi hiyo.

Ligi hiyo inasimama ikiwa raundi ya pili ili kupisha mechi za kimataifa kwa timu za taifa kuwania tiketi ya fainali za Afcon za mwakani zitakazofanyikia Morocco, ambapo Tanzania itakuwa na mechi mbili dhidi ya Ethiopia, Septemba 4 ikipigwa Kwa Mkapa na ugenini dhidi ya Guinea, Septemba 10 na itaendelea tena Septemba 11.

Hadi inasimama juzi ikipigwa michezo mitatu, Yanga ikiiua Kagera Sugar kwa mabao 2-0 na Namungo kufa nyumbani mbele ya Fountain Gate kwa idadi kama hiyo mbali na sare ya 1-1 ya KMC na Coastal Union, vinawa wa ligi hiyo ni Simba yenye pointi sita kama Singida Black Stars kila moja ikicheza mechi mbili.

Mbali na kuongoza msimamo, kikosi hicho chja Kocha Msauzi, Fadlu Davids, pia imefunika kwa kuwa timu yenye mabao mengi hadi sasa ikifunga saba, lakini ikiwa haijaruhusu nyavu zao kuguswa kama ilivyo kwa Yanga, Azam Fc, JKT Tanzania, Pamba Jiji, Tanzania Prisons na Mashujaa.

Huu ni msimu wa pili kati ya 11 Simba ikicheza mechi mbili na kufunga mabao saba bila nyavu zake kuguswa, ikifanya hivyo 2017-2018 ilipoanza kwa kuicharaza Ruvu Shooting 7-0 kisha suluhu na Azam msimu ambao ilibeba taji ikiipokea Yanga iliyokuwa imetwaa mara tatu mfululizo kama ilivyo sasa. Yanga imebeba taji hilo kuanzia 2021-2022, 2022-2023 na 2023-2024.

Mbali na kuongoza mabao ikifunga saba ikiwa ni wastani wa kila moja imefunga mabao 3.5, Simba pia ina mfungaji kinara kwa sasa ambaye ni Valentino Mashaka mwenye mabao mawili, huku winga wa timu hiyo, Edwin Balua akiwa kinara wa kufunga bao la mapema zaidi akitumia dakika 13, akilipiku bao la kwanza la msimu huu kwa kikosi hicho lililofungwa na beki wa kati Che Fondoh Malone dhidi ya Tabora United aliyefunga dakika ya 14.

Mbali na nyota hao kuongoza mabao ya mapema zaidi hadi sasa, lakini kiungo mshambuliaji wa timu hiyo kutoka Ivory Coast, Jean Charles Ahoua anaongoza kwa wachezaji walioasisti mabao akifanya hivyo mara tatu, huku kipa Moussa Camara akiongoza clean sheet akiwa na mbili kama ilivyo kwa makipa wengine, Patrick Munthali (Mashujaa), Mussa Mbisa (TZ Prisons) na Yona Amos (Pamba Jiji).

Kwa mabao yaliyofungwa dakika za lala salama, Awesu Awesu pia wa Simba yupo katika orodha hiyo sambamba na beki Salum Chuku wa Tabora United kila mmoja akifunga bao dakika ya 90+2 katika mechi za timu hiyo, huku bao la Chuku likiipa ushindi wa 2-1 Nyuki wa Tabora mbele ya Namungo.

Nyota wengine wa mabao wa jioni ni Clement Mzize wa Yanga aliyefunga dakika ya 88 wakati Yanga juzi ikiifunga Kagera Sugar 2-0 na lile la Maabad Maulid wa Coastal Union aliyefunga kwa penalti dakika 87 kuiokoa isilale mbele ya KMC juzi na kuifanya itoke sare ya 1-1 ugenini jijini Dar es Salaam.

Hadi sasa katika mechi hizo 13 na mabao 22 yaliyofungwa, ni moja tu ndilo la kujifunga lililowekwa wavuni na kipa wa Dodoma Jiji, Daniel Mgore wakati akijaribu kuokoa shuti kali la pembeni la nyota wa Mashujaa, Crispin Ngushi katika mechi ya fungua dimba ya msimu huu iliyopigwa Lake Tanganyika, mjini Kigoma.

Pia zimeshuhudiwa penalti tatu, zilizopigwa bila kukoswa kupitia Djuma Shaban (Namungo), Heritier Makambo (Tabora United) na Maabad Maulid, huku kukiwa hakuna kadi yoyote nyekundu.

Pia katika mabao 22, wachezaji 20 wamehusika kuyatia wavuni, nyota wa kigeni wakiongoza orodha kwa kufunga 11, huku tisa yakiwa ya wazawa wakiongozwa na Valentino aliyetupia mawili.

Wageni 11 waliofunga mabao hayo ya Ligi Kuu hadi sasa ni; Mghana Emmanuel Kayekeh (Singida BS), Mkenya Elvis Rupia (Singida BS), Mohammed Camara raia wa Guinea anayekipiga Singida BS), beki Mcameroon Che Fondoh Malone(Simba) na Beki Mu Ivory Coast, Tra Bi Tra (Singida BS). Wengine ni Mganda Steven Mukwala, Jean Ahoua (Ivory Coast) wote Simba, Wakongomani Djuma Shaban (Namungo), Heritier Makambo (Tabora Utd) na Maxi Nzengeli wa Yanga na Ibrahim Elias, raia wa Somalia anayekipiga KMC.

Mbali na Valentino, wazawa wengine waliofunga hadi sasa katika orodha wa wafungaji ni Maabad Maabad (Coastal Union), Clement Mzize(Yanga), Edger William na Seleman Mwalimu (Fountain Gate), Awesu na Balua (Simba), Joshua Ibrahim (KenGold) na beki Salum Chuku (Tabora United).

Hata hivyo, timu sita ikiwamo Yanga, Azam, KMC, Coastal Union, JKT Tanzania na KenGold zimecheza mechi moja moja kulinganisha na nyingine 10 zilizocheza michezo miwili kila moja.

Akizungumzia ligi hiyo, nyota wa zamani aliyewahi kukipiga Simba, Yusuph Mgwao aliliambia gazeti hili kuwa uwepo wachezaji wa kigeni umechangia kwa kiasi kikubwa kuwafanya wazawa kuwa na mwanzo mzuri katika ligi.

“Kwa wachezaji wa Tanzania kiukweli naona kuna mwamko mkubwa na yote inatokana na changamoto wanazopata kutoka kwa wa kigeni na limekuwa darasa kubwa kwa vijana wetu,” alisema.

Kipa wa zamani wa Yanga, Juma Pondamali ‘Mensah’ alisema: “Tunapoona wachezaji wetu wanaanza vizuri tunafarijika sana kwa vile tunakuwa na uhakika kuwa timu ya taifa itafanya vizuri kwa kuwategemea hao baadaye.”

Chanzo: Mwanaspoti