Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kwa Simba hii... Tema mate chini

Mate Pic Data Baadhi ya Wachezaji waliopo kwenye Msafara wa Kikosi cha Simba

Wed, 11 Aug 2021 Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz

Klabu ya wekundu wa Msimbazi, Simba SC dirisha hili kubwa la usajili itafunga kwa kunasa nyota nane wapya watano wazawa na watatu wa kigeni ili kuboresha kikosi chao.

Usajili ambao wamefanya na wachezaji watakaobaki nao wa msimu uliopita watajenga kikosi kuwa na wachezaji wengi wote wenye uwezo bora. Kikosi cha Simba kina wachezaji ambao kila mmoja anafaa kuanza kile cha kwanza na wengine benchi kwa kutopata nafasi.

Ifuatayo ni ripoti ya Uchambuzi

MAKIPA

Mpaka sasa Simba kuna makipa wanne Aishi Manula, Benno Kakolanya na Ally Salim waliokuwepo na dirisha hili wamemuongeza kipa wa Prisons, Jeremia Kisubi.

Kutokana na makipa hao Manula anapewa nafasi ya kuendelea kuwa chaguo la kwanza kutokana na rekodi ambazo amekuwa akizionyesha kikosini.

Ushindani utakuwepo kati ya Kakolanya na Kisubi atakayekuwa namba mbili na mwingine chaguo la tatu na hilo litatokana na uwezo mazoezini, lakini kuna nafasi kubwa ya Salim kutolewa kwa mkopo.

BEKI WA KULIA

Dirisha hili Simba imemnasa beki wa KMC, Israel Patrick Mwenda ambaye ni bora katika eneo hilo kutokana na kiwango alichoonyesha msimu uliopita akiwa Taifa Stars. Usajili huo umewafanya Simba kuwa na mabeki wa kulia watatu - Mwenda, Shomary Kapombe ambaye anapewa nafasi ya kucheza mara kwa mara msimu ujao na David Kameta ‘Duchu’ ambaye kuna kila dalili ya akatolewa kwa mkopo kutokana na msimu uliopita kushindwa kupata nafasi kucheza mara kwa mara.

Licha ya kuletwa mabeki wa kulia kwa nyakati tofauti Kapombe amekuwa akicheza katika kikosi cha kwanza mbele ya makocha mbalimbali waliotua Msimbazi.

Kapombe ni wazi hana ushindani katika nafasi hiyo na ataendelea kucheza kwenye kikosi cha kwanza labda itokee amepata majeraha au kupumzishwa.

BEKI WA KUSHOTO

Katika nafasi ya beki wa kushoto, Simba wana mpango wa kumsajili baada ya kumkosa Edward Charles Manyama aliye kwenda Azam.

Simba walimtaka pia beki wa kushoto wa KMC, Bryson Raphael ambaye naye walishindwa kumpata baada ya kukamilisha usajili wake kuchezea Yanga msimu ujao.

Kama Simba ikitokea wameshindwa kumpata beki wa kushoto mpya maana yake Mohammed Hussein ‘Tshabalala’ ataendelea kutawala na kucheza mbele ya Gadiel Michael.

MABEKI WA KATI

Mpaka wakati huu unasoma hapa katika kikosi cha Simba kuna mabeki wa kati sita ambao kati yaao wanatakiwa kucheza wawili au watatu katika kila mechi moja.

Kwenye dirisha hili Simba imesajili beki wa kati kutoka DC Motema Pembe ya DR Congo, Henoc Inonga ambaye kama atakuwa katika kiwango bora atalazimika kupangua ukuta wa timu hiyo uliotumika zaidi msimu uliopita.

Mabeki wa kati msimu uliopita waliotumika zaidi ni Joash Onyango na Pascal Wawa ambao kama mmoja kati yao atashindwa kufanya vizuri maana yake Inonga maarufu kama Varane atachukua nafasi hiyo.

Wakati huohuo kuna mabeki wengine waatatu - Kennedy Juma, Ibrahim Ame na Erasto Nyoni ambao wamekuwa wakiingia na kutoka katika kikosi cha kwanza na hawachezi mara kwa mara.

Inaelezwa Ame anaweza kwenda kwa mkopo katika timu nyingine, lakini kwa upande wa Nyoni anaweza kucheza katika nafasi zaidi ya hiyo na hivyo ushindani wa nafasi hiyo unaweza usiwe changamoto kwake.

KIUNGO MKABAJI

Kabla ya dirisha la usajili litakalofungwa Agosti 31, Simba watafunga kwa kutambulisha kiungo mwingine kutoka Mali, Saido Kanoute ambaye anaweza kucheza nafasi ya ukabaji na ushambuliaji.

Kutokana na usajili huo maana yake Simba watakuwa na viungo wanne wakabaji ambao ni Kanoute, Taddeo Lwanga, Jonas Mkude na Mzamiru Yassin ambao kati yao kutakuwa na mchuano.

Kutokana na mchuano kati yao ubora alioonyesha Lwanga msimu uliopita kwenye nafasi hiyo ni wazi atapewa nafasi ya kuanza wakati huohuo Kanoute kama atakuwa kwenye ubora watacheza pamoja.

Mkude aliyekuwa nje ya timu pamoja na Mzamiru ambaye amekuwa na ingia toka katika kikosi cha kwanza wataendelea kuwa na mchuano wa kutosha ili kupata nafasi ya kucheza kikosi cha kwanza.

WINGA WA KULIA

Katika eneo la winga wa kulia napo kutakuwa na ushindani wa aina yake kutokana na usajili ambao Simba wameufanya licha ya kumuuza Luis Miquissone.

Kama kocha wa Simba, Didier Gomes atataka kutumia winga asilia maana yake kutakuwa na ushindani na Bernard Morrison ambaye alikuwepo tangu msimu uliopita.

Morrison katika kikosi cha Simba msimu uliopita hakuwa mchezaji wa kikosi cha kwanza na kwenye dirisha lijalo la usajili wamemuongeza Yusuph Mhilu ambaye atakuja kuongeza upinzani katika nafasi hiyo.

Ni wazi kama Mhilu atakuwa anacheza kama ilivyokuwa katika kikosi cha Kagera na iwapo Simba watakuwa wanataka kutumia winga asilia anaweza kucheza mbele ya Morrison.

KIUNGO - MSHAMBULIAJI

Katika eneo la viungo washambuliaji Simba wapo wanne Rally Bwalya, Said Ndemla, Clatous Chama na katika kipindi hiki wamewaongeza Jimson Mwanuke kutoka Gwambina na Abdulsamad Kassim kutokea Kagera Sugar ambaye anaweza pia kucheza nafasi ya kiungo mkabaji. Ni wazi kutokana na viwango vya Chama na Bwalya ambavyo wamevionyesha katika mechi walizocheza, hata msimu ujao licha ya maboresho hayo wataendelea kuwa wachezaji wa kikosi cha kwanza, iwapo watakuwepo Msimbazi.

Ndemla, Mwanuke na Kassim wataendelea kuwa wachezaji mbadala wa wawili haoa kama ikitokea kuna atakayekosekana katika mechi au kutolewa.

MASTRAIKA

Simba wamenogesha katika eneo hilo kwa kumsajili Kibu Denis ambaye msimu uliopita akiwa katika kikosi cha Mbeya City ni mmoja wa wachezaji waliofanya vizuri kwenye Ligi Kuu Bara.

Sio rahisi kwa Kibu kupata nafasi ya kucheza kwenye kikosi cha kwanza cha Simba mbele ya Chriss Mugalu, John Bocco na Meddie Kagere ambaye naye inaelezwa huenda akatolewa kwa mkopo.

Ni wazi Bocco aliyekuwa mfungaji bora msimu huu na Mugalu aliyeshika nafasi ya pili kwenye kinyang’anyiro hicho wataendelea kuwa wachezaji wa kikosi cha kwanza na wengine watafuata.

Kibu ana kazi kubwa ya kufanya ili aweze kupata nafasi ya kucheza mbele ya miamba hiyo miwili - Bocco na Mugalu ambao kila wakipata nafasi ya kucheza wamekuwa wakifunga mabao na kuisaidia timu yao kupata ushindi.

WINGA WA KUSHOTO

Katika eneo hilo baada ya kumuuza Miquissone na kumtoa kwa mkopo Perfect Chikwende Simba wamemsajili Mmalawi Peter Banda ambaye anatazamwa kuziba nafasi hiyo.

Banda ni mmoja wa mawinga wazuri, lakini kivuli cha kuziba pengo ambalo limeachwa na Miquissone kutokana na ubora aliyoonyesha kwa kipindi cha miaka miwili alichokuwa nchini sio kazi rahisi kwake.

Katika nafasi hiyo Banda atakuwa na mtihani wa kuwania kucheza na Hassan Dilunga ambaye hata msimu uliopita alikuwa akiingia na kutoka, ingawa kila alipoingia alisumbua kiasi cha kuchangia ushindi Msimbazi.

Baada ya Simba kumsajili Banda huenda wakaachana na Miraji Athuman ambaye ni mmoja wa mawinga wazuri wenye uwezo wa kufunga na kutengeneza nafasi za kufunga kwa wachezaji wengine.

Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz