Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kwa Mkapa wapewa heshima ya VAR

VAR Mkapaaa ,, Kwa Mkapa wapewa heshima ya VAR

Sat, 15 Jun 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Baada ya Waziri wa Fedha Mwigulu Nchemba kutangaza kuwa msimu ujao mechi za Ligi Kuu zitakuwa teknolojia inayomsaidia mwamuzi kufanya marejeo ya picha (Video Assistance Referee-VAR), Kaimu Mkurugenzi wa Michezo Ally Mayai amesema Uwanja wa Mkapa umeteuliwa kuwa kituo maalumu cha mafunzo kwa Afrika.

Mwigulu aliyasema hayo juzi Alhamisi, Juni 13, 2024 wakati akisoma Bajeti Kuu ya Serikali kwa mwaka mpya wa fedha 2024/2025.

Alisema:"Msimu ujao wa Ligi Kuu ya Tanzania tutaanza kutumia 'VAR' ili kuhakikisha matokeo yanayopatikana uwanjani yanakuwa ya haki maana kuna timu zimezidi - msimu mmoja penalti 10, halafu zikifungwa zenyewe magoli yanakataliwa. Na ili tuwe na 'VAR' za kutosha katika viwanja vyote, naleta pendekezo la kutoa msamaha kwenye uingizaji wa mashine za 'VAR' na vifaa vyake kwa ufafanuzi utakaotolewa hapo baadaye. Inawezekana," alisema Waziri huyo na mdau mkubwa wa michezo.

Akizungumza na Mwananchi jana, Mayai alisema serikali itakuwa na gharama kubwa mbili kwenye mchakato huo wa kufunga VAR nchini, ambapo moja ni kuhakikisha inatengeneza wataalamu wazuri, lakini nyingine ni kusimamia teknolojia hiyo jambo ambalo anaamini lipo ndani ya uwezo wao.

Hata hivyo, alisema kuwa wataalamu wa mafunzo hayo wanaletwa na Caf, na kila kitu kitakuwa kinafanyika kwenye Uwanja wa Benjamini Mkapa, sehemu ambayo imechaguliwa kwa ajili ya kuendesha mafunzo hayo kwa Bara la Afrika.

"VAR ni mitambo ambayo inasimamiwa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF), kwetu sisi tuna gharama ya namna ya kupata wasimamizi ambao watakuwa wamefuzu kusimamia mitambo hiyo, nafikiri ni fursa nzuri tumeipata sisi kuwa na kituo cha mafunzo hapa nchini, hili ndiyo wengi walikuwa hawalifahamu.

"Tanzania kupitia Uwanja wa Benjamin Mkapa ndio kituo kitakachotumika kuwanoa wasimamizi wa mtambo huo wa VAR kwa Afrika nzima, tutakuwa na gharama ya kuangalia jinsi ambavyo tutazalisha wasimamizi bora na wa kutosha wa ndani," alisema.

Mayai alisema wataalamu kutoka CAF ambao ndio walisimamia mchezo wa African Football League (AFL) na waliochezesha mchezo wa robo fainali Ligi ya Mabingwa Afrika kwenye mechi za Simba dhidi ya Al Ahly na Yanga dhidi ya Mamelodi msimu uliomalizika ni miongoni mwa wakufunzi watakaokuwepo Tanzania.

"Uwanja wa Mkapa ndiyo ambao umependekezwa na Caf kwanza, ndiyo maana uliona ulifanyia majaribio kwenye michuano ya African Football League (AFL) baada ya hapo ndiyo itasambaa sehemu nyingine, lakini kwanza hapa.

Mayai alisema kozi zitakazotolewa kwa wasimamizi hao ya kwanza itakuwa ya cheti na Diploma, ambapo mshiriki anaweza kumaliza hapa lakini bado asifuzu kuwa msimamizi.

"Kuwa msimamizi siyo elimu tu, mpaka pale ambapo utaidhinishwa kwamba unastahili kusimamia mitambo hiyo, nafikiri utaratibu mzima utatolewa na jinsi ambavyo watu wanaweza kusomea," alisema Mayai mchezaji wa zamani wa Taifa Stars.

Ikumbukwe kwamba, mpango wa matumizi ya VAR kwa msimu ujao wa Ligi Kuu Bara umeshaanza kufanyiwa kazi ambapo Shirikisho la Soka Afrika (CAF) kwa kushirikiana na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), hivi karibuni liliendesha mafunzo ya awali ya kufunga vifaa hivyo yaliyofanyika Uwanja wa Mkapa jijini Dar es Salaam yakiongozwa na Meneja wa Teknolojia ya Soka kutoka CAF, Wael Elsebaie.

Mafunzo hayo ya kuvifunga sambamba na kuviendesha vifaa hivyo yalishirikisha jumla ya watu sita wakiwemo Watanzania wanne na Wakenya wawili. Baada ya kukamilika kwa mafunzo hayo, inafahamika kuwa yataanza mafunzo kwa Waamuzi waweze kutumia VAR katika michezo mbalimbali.

Chanzo: Mwanaspoti