Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kwa Mbwana Samatta, hapana aisee!

Samatta 8AE1231.jpeg Nahodha wa Taifa Stars, Mbwana Samatta

Wed, 24 Jan 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Wakati anatolewa nje katika kipindi cha pili cha mechi ya kwanza ya Tanzania dhidi ya Morocco, Mbwana Samatta alionekana mwenye huzuni na ambaye pengine moyoni hakuwa anakubaliana na uamuzi wa kumbadilisha wakati timu ikihitaji ushindi kwa udi na uvumba.

Hakuwa amejaribu kuunganisha mpira wowote wa krosi uliopigwa golini mwa Morocco na hata hivyo, ni mipira michache iliyopitishwa mbele ya lango la wababe hao wa Afrika Kaskazini.

Na kwa maana hiyo, hakuwa ameweza kutumia kipaji chake kikubwa cha kufunga mabao ya kichwa kwa kuwa hakukuwa na krosi nzuri zilizoelekezwa golini. Zaidi ya hapo, hakuwa amecheza kama mshambuliaji wa kwanza. Muda mwingi alikuwa akicheza kama mshambuliaji wa pili, akishirikiana na viungo kujenga mashambulizi.

Magoli ya vichwa ndio nguvu kubwa na siri ya mafanikio ya mshambuliaji huyo wa zamani wa Simba.

Wakati Aston Villa ikimtaka Mbwana Samatta kutoka Racing Club Genk ya Ubelgiji, wakongwe hao wa England walikuwa ndio timu pekee ya Ligi Kuu iliyokuwa haijafunga bao la kichwa licha ya kuwa moja ya timu zilizokuwa zinaongoza kwa idadi ya krosi msimu wa mwaka 2020/21.

Mshambuliaji mpya Mbrazili aliyenunuliwa majira ya joto, Wesley alikuwa anaonekana kupata shida kujiweka katika eneo ambalo angeweza kuunganisha mipira ya krosi kwa kichwa licha ya kuwa na uwezo mwingine katika ufungaji. Lakini hadi Villa wanamuhitaji Samatta, Wesley alikuwa ameshaumia mwezi Desemba na madaktari walisema asingeweza kucheza hadi msimu uishe.

Kitakwimu, Samatta ndio alikuwa amevutia sana kwa kuwa namba zake katika kufunga, hasa kwa mipira ya krosi, zilikuwa zinashawishi kuwa ndiye mshambuliaji pekee ambaye angeweza kuziba pengo la Wesley na kuondoa nuksi ya kushindwa kuunganisha krosi kwa kichwa, hasa kwa kuzingatia kuwa kocha wa wakati huo, Deam Smith alikuwa anapenda kutumia mipira ya krosi kutoka kwa mabeki wa pembeni.

Katika mabao 76 aliyofunga katika mechi 191 akiwa na RC Genk, mabao 22 alifunga kwa kichwa. Na katika mechi 17 za mwisho kabla ya kusaini mkataba na Villa, Samatta alikuwa amefunga mabao tisa kwa kichwa. Kwa hiyo alikuwa chaguo sahihi kwa timu ambayo iliweza kufikisha ndani ya eneo la penato, krosi 46 katika mechi 24, ikishika nafasi ya pili wakati huo nyuma ya Manchester City.

Na mbinu yake ilikuwa ikiwasumbua mabeki, hata wale vipande vya watu. Hujificha nyuma ya beki na kupiga hesabu za kasi ya mpira. Huchomoka ghafla ya kwenda kuunganisha wavuni krosi au kona kufunga bao kirahisi huku mabeki wakibaki wamepigwa butwaa. Kabla ya kwenda Villa, Samatta alifanya hivyo dhidi ya Liverpool katika mechi ya Ligi ya Mabingwa wa Ulaya, akiwakwepa Alex Alexander Chamberlin na James Milnner.

Na video ya bao hilo ndiyo iliyotumika kumtambulisha Samatta baada ya kusaini mkataba wa kuichezea Aston Villa na kuwa Mtanzania wa kwanza kucheza Ligi Kuu ya England.

Hiyo ndiyo nguvu ya Samatta! Kwa nini nguvu hiyo haionekani wakati anapocheza Taifa Stars. Kwa nini Aston Villa walitambua siri hiyo na wakaweza kuitumia hadi Wesley alipopona, lakini huku tunashindwa kuiona na kuitumia?

Awali Samatta alionekana, hasa mwanzoni alipokuwa akichezea timu ya taifa ya vijana chini ya miaka 20 na baadaye Taifa Stars. Lakini kadri siku zinavyokwenda ndivyo anavyoonekana kupungua kasi yake ya ufungaji, hasa wa mabao ya kichwa. Inawezekana kuwa ni umri, lakini bado angeweza kutumia kipaji chake cha kufunga kwa kichwa hata umri uende namna gani.

Katika miaka ya karibuni, mara nyingi Samatta amekuwa akicheza kama mshambuliaji wa pili badala ya kuwa kinara kusubiri krosi au kona ndani ya eneo la penati. Na kibaya zaidi, timu imekuwa haina mawinga wa asili wanaofurahia kumwaga golini mipira, huku mabeki wa pembeni wakiwa hawafanyi kazi hiyo sana, hasa baada ya Shomary Kapombe kuanza kuachwa.

Kwa hiyo, katika hali ya kawaida hutegemei kumuona mara kwa mara Samatta akiruka juu kujaribu kuunganisha wavuni mipira ya krosi, huku ikimuwia vigumu kutumia uwezo wake mwingine wa kufunga mabao kwa mashuti akitokea upande wa kushoto. Samatta amekuwa katika hali ngumu anapokuwa timu ya taifa na baadhi ya mashabiki washaanza kuguna, huku wakisema umefika wakati naye apumzike.

Ni kwa sababu walizoea kuona Samatta akiwanyanyua vitini kwa mabao safi ya kichwa ambayo hadi sasa yamefika 20 tangu aanze kuichezea timu ya taifa.

Na katika mechi dhidi ya Zambia, alionyesha kwa nini anastahili kuendelea kuwemo katika kikosi kinachoanza wakati alipotoa pasi safi ya mwisho kwa Simon Msuva aliyeiwezesha Tanzania kupata pointi moja ya kwanza katika fainali za Mataifa ya Afrika zinazoendelea nchini Ivory Coast.

Na kwa kuwa Samatta anaonekana kucheza zaidi kama mshambuliaji wa pili, Msuva ndiye amegeuka kuwa mfungaji wa Stars na katika mechi dhidi ya Zambia alifunga bao lake la 22 tangu aanze kuitumikia timu ya taifa ya Tanzania.

Katika mazingira kama hayo, Samatta atalaumiwa sana lakini bado uwepo wake uwanjani ni muhimu kwa Stars kwa kuwa huwafanya wachezaji wa timu nyingine kuwa na wasiwasi wakati wote, huku akiwa ni kiongozi anayeshimiwa na wenzake ndani nan je ya uwanja.

Chanzo: Mwanaspoti