Kila nikiwafikiria Mamelodi Sundowns, siombei wakutane na Simba kwenye Robo Fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika. Jamaa wanatisha balaa.
Kama Simba watafanikiwa kupenya kuingia katika hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika, ni bora wakutane na kinara wa kundi A ambaye kuna uwezekano mkubwa akawa Wydad ya Morocco au kinara wa kundi D ambaye kuna uwezekano mkubwa akawa ni Esperance.
Licha ya ubishi wote ambao umekuwepo kijiweni, kwenye hili la Mamelodi, hakuna hata mmoja aliyethubutu kubisha zaidi wengi wametikisa kichwa kuashiria kuwa wanaunga mkono sala zangu kuwa Simba isikutane na Mamelodi Sundowns.
Jamaa kwanza wana bonge la timu halafu limeundwa na kundi kubwa la wachezaji wa nyumbani kwao Afrika Kusini lakini wengi wamekulia katika njia sahihi za kimpira maana kule Afrika Kusini kuna vituo vya soka la vijana vingi kuliko hata idadi ya timu zao.
Safu yao ya ulinzi sio tishio sana ila tatizo kubwa ni ile safu yao ya ushambuliaji. Ina watu wana njaa kweli na kumpiga mtu tatu, nne, tano na hata sita kwa ni jambo la kawaida wakiongozwa na yule Mnamibia, Peter Shalulile.
Sawa Simba inaweza kupata bao au hata mabao dhidi yao lakini je kwa ile beki ya Simba inaweza kuwazuia wale wasifunge? Kwanza Simba yenyewe imekuwa butu katika hatua hiyo ya makundi ya ligi ya mabingwa Afrika ambapo hadi sasa imefunga mabao mawili tu, je inaweza kuwafunga nyingi wale Mamelodi hata kama ukuta wao ndio dhaifu kama tunavyoaminishana?
Kinachonipa wasiwasi zaidi ni kasi ya wale watu wao pale mbele na udhaifu wa mabeki wa Simba kukabiliana na wachezaji wenye spidi na wanaoweza kumiliki mpira na kupiga pasi za haraka haraka. Kama hauna ukuta imara, basi angalau unapaswa kuwa na kiungo/viungo mahiri wa ulinzi wa kupunguza athari yao sasa, jamani mchezaji mwenyewe wa kutibua mipango ya Mamelodi ndio Sawadogo?
Na mbaya zaidi, wale jamaa hawamtegemei mchezaji mmoja katika kufunga mabao. Katika mabao 11 waliyofunga hadi sasa, wachezaji saba tofauti wamefunga na kati yao kuna washambuliaji, viungo na hadi mabeki.
Halafu nawakumbusha jamani, wale Mamelodi huwezi kuwadhulumu kirahisi maana bosi wao ndio rais wa Caf. Ukiwadhulumu jua cha moto utakipata.
Ukipangwa kucheza na wale jamaa unapaswa kujipanga vilivyo ili wasikutoe na kukuaibisha vinginevyo ukijichanganya wanaweza kukupiga 10 wale nimekaa paleeeeeeee.