Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kwa Chama, Benchikha muongo

Simba Vs Yanga Chama Yulee.jpeg Kwa Chama, Benchikha muongo

Wed, 13 Dec 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Tangu achukue mikoba rasmi ya kuifundisha Simba, Kocha Abdelhak Benchikha amekuwa muongo!

Kuna jambo naona ni kutudanganya tu. Clatous Chota Chama na Mzamiru Yassini wamekuwa watu wa kuanzia benchi! Hakuna ubaya kwa wao kuanzia benchi, shida ipo kwa wanaochukua nafasi zao.

Tangu aje Tanzania, sijawahi kumwelewa Sadio Kanoute. Hata siku moja. Hata mara moja! Namuona mara nyingi uwanjani akicheza rafu tu na akionywa kwa kadi za njano zisizokuwa na idadi.

Huenda Kanoute ni mchezaji mzuri lakini sio kwa Simba. Nimeona ndiye chaguo la kwanza la Benchikha mbele ya Mzamiru. Pengine ni maamuzi ya kiufundi sana ambayo mimi na wewe sio rahisi kuona lakini mpira ni mchezo wa wazi.

Bado anapoingia Mzamiru Yassini kuna vitu vingi sana analeta. Mzamiru ana faida nyingi uwanjani kuliko Kanoute. Sio kwa ubaya. Sio kwa kumsagia kunguni. Kanoute ni mchezaji mzuri lakini hana uwezo wa kuanza mbele ya Mzamiru.

Kuna mahali naona Kama Benchikha anatudanganya. Kuna kitu naona hakipo sawa. Wachezaji wazawa pale Simba ambao wamebaki kwenye ubora wa hali ya juu, ni Kibu Dennis na Mzamiru Yassin. Najua kocha bado ni mpya.

Najua anahitaji muda kuwajua wachezaji wote na ubora wao lakini, Mzamiru anahitajika sana kikosi cha kwanza. Hapa naona kama kocha anatudanganya kutuaminisha Kanoute ni bora kuliko Mzamiru.

Ni mechi ya pili sasa Chama anaanzia benchi. Kiukweli hapa pia kuna namna anatudanganya. Ni kweli Chama hayuko kwenye ubora wake msimu huu kama wengi tunavyomjua. Ni kweli na yeye ni binadamu kama wengine kuna muda anakuwa na siku mbaya kazini.

Pamoja na hayo yote, bado hawezi kuwekwa benchi na Essomba Onana. Huu ni Uongo. Onana ni mzuri lakini anahitaji muda kuingia kwenye mfumo wa Simba na ligi yetu. Kitendo cha kumuanzisha kwenye nafasi ya Chama ni uongo.

Pamoja na Chama kupungua ubora msimu huu lakini sio wa kuwekwa benchi na Onana. Nadhani kocha bado na yeye anajitafuta. Naona Benchikha bado anawasoma wachezaji wake kwa mechi mbili mfululizo Chama ametokea benchi. Hajafunga bao lolote wala kutoa pasi ya bao lakini amekuwa moto mno kuliko Onana. Sio kwa ubaya, Chama bado ana ubora wa kuanza kikosi chochote cha Ligi Kuu Bara.

Akiingia tu, unaona utulivu kwenye timu. Hana spidi miguuni, ana spidi kichwani. Akili yake ina kasi sana akiwa na mpira. Ni fundi haswa. Bado Simba inamhitaji sana uwanjani na hasa timu inapokuwa eneo la mwisho la ushambuliaji.

Mtu pekee anayeweza kumpeleka benchi kwa sasa Shomary Kapombe ni Kouassi Attohoula Yao. Kwa bahati mbaya, hayuko Simba. Ndiye mchezaji pekee kwa sasa kwenye ligi yetu ambaye nikisikia ameanza na Shomary yuko nje siwezi kushtuka.

Kuna mechi nimemuona Benchikha ameanza na bwana mdogo Israel Mwenda. Sio mchezaji mbaya hata kidogo lakini bado Kapombe yuko juu. Mwenda ni mchezaji anayejitafuta, Kapombe ni mchezaji ambaye amejipata muda mrefu. Tatizo la nchi yetu, kuna muda unamchoka tu mtu kwa sababu umemuona kwa muda mrefu.

Tunawanyooshea vidole wachezaji wetu wengi sana wazawa lakini ukweli ni kuwa hatuna mbadala wao. Tunasema John Bocco kazeeka lakini tuna mbadala wake? Mbwana Samatta umri umeenda, ni kweli lakini nani anafaa kuvaa viatu vyake? Hapa ndipo tatizo kubwa la soka letu lilipo.

Ni kweli kwa mipango ya baadaye, Mwenda anaweza kuja kuwa msaada kwa timu lakini kwenye mechi kubwa za Simba, bado zinamhitaji mchezaji mkubwa.

Kocha inabidi aangalie mechi zenye uzito wa Kapombe na zile zenye uzito wa Mwenda. Linapokuja suala la Ligi ya Mabingwa Afrika, anahitajika sana mtu mkubwa. Mwenda bado hawezi kuibeba timu kama Kapombe lakini ni vyema akaanza taratibu kupata dakika chache uwanjani.

Simba chini ya Benchikha haijashinda mechi hata moja lakini kuna namna Simba imebadilika kiuchezaji.

Kuna namna Simba imeanza kurudi kwenye soka lake la asili. Naanza kushawishika kuwa kama Benchikha atapata muda wa kutosha na wachezaji wake hata wanne, Simba wanaweza kuja kusumbua.

Timu ilitoka sare kule Botswana lakini waliupiga mwingi. Simba imefungwa kule Morocco, lakini imeubonda mwingi sana.

Ni kusema tu soka wakati mwingine ni mchezo wa kikatili sana. Bado kwenye matokeo kocha ana deni kubwa lakini taratibu kiuchezaji timu inabadilika.

Ujenzi wa timu unaonekana uko imara. Simba wakimpa kocha muda na wachezaji wake, anaonekana atakuja kutengeneza timu nzuri. Lakini kitendo cha kuanza na Onana kama mbadala wa Chama, huo ni uongo. Kitendo cha kuanza na Israel Mwenda badala ya Kapombe, huo ni uongo pia.

Mzamiru Yassini ndiyo mpigania Uhuru pale Msimbazi. Bado ana uwezo mkubwa sana wa kumfanya awe kikosi cha kwanza. Ngoja tuone mechi tatu zilizobaki. Ngoja tuone Benchikha anataka kutudanganya tena na lipi!

Chanzo: Mwanaspoti
Related Articles: