Kuna historia nyingine ni ngumu sana kuzivunja. Ni kama hii historia ya Simba na mashindano yanayoandaliwa na Shirikisho la Soka Afrika (CAF). Ni historia ya kuvutia sana.
Nimeona kelele nyingi sana huko mitaani kwa baadhi ya watu wa Yanga wakijinasibu kuwa, wao ndio wababe kwenye mashindano hayo. Inashangaza sana. Ukweli upo wazi.
Simba ndio timu ya kwanza nchini kufanya vizuri zaidi kwenye mashindano ya CAF. Ilianza 1974 na inafanya vizuri hadi leo. Mwaka 1974 ilifika nusu fainali ya Klabu Bingwa Afrika (sasa Ligi ya Mabingwa). Ndio rekodi ya kwanza kubwa kwenye mashindano ya Afrika kuwekwa na timu ya Tanzania.
Ilikuwa ni kama nyota inayoanza kuangaza kwa Simba. Miaka 19 baadaye ikafika fainali ya Kombe la CAF (michuano iliyoungwanishwa na Kombe la Washindi na kuwa Kombe la Shirikisho Afrika la sasa). Ikawa timu ya kwanza kwa Tanzania kufika fainali ya mashindano hayo.
Baada ya Simba kufika fainali mwaka 1993, imechukua miaka 30 kwa timu nyingine ya Tanzania kufika katika hatua hiyo. Ni Yanga ambayo imefika fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika msimu uliopita na kukosa kiduchu kubeba taji kwa kanuni ya bao la ugenini licha ya matokeo yote kuwa sare ya 2-2.
Yaani wakati Simba inacheza fainali ya CAF mwaka huo, hawa vijana wadogo wanaopiga kelele mitandaoni walikuwa hata hawajazaliwa. Sio kuzaliwa tu wala ilikuwa haijulikani kama watazaliwa.
Ila ajabu ni kwamba leo wanakuwa wa kwanza kukashfu fainali ya Simba. Huku ni kukosa adabu na heshima. Kufika fainali kwa Yanga mwaka huu haikupaswa kuwa sehemu ya kukosea heshima mafanikio hayo ya Simba.
Ni kweli kwamba Yanga ilikuwa timu ya kwanza nchini kufika hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika. Ilifanya hivyo mwaka 1998. Bahati mbaya ilimaliza wa mwisho katika kundi lake.
Iliichukua Simba miaka mitano tu kufikia rekodi hiyo ya Yanga kwa kufuzu hatua ya makundi mwaka 2003 tena kwa kuivua taji waliokuwa watetezi, Zamalek ya Misri. Kumbuka ni Zamalek ile sio hii inayofungwa na hata Wadjibouti. Wakamaliza katika nafasi ya tatu kwenye kundi lao ambalo lilitoa timu mbili zilizocheza fainali. Ilikuwa ni Enyimba na Ismailia. Enyimba wakatwaa ubingwa.
Lilikuwa ni kundi gumu, lakini Simba hakumaliza kinyonge. Alipata alama saba. Simba ilikuwa miongoni mwa timu chache zilizopata ushindi mbele ya Enyimba kwa mwaka huo.
Iliichukua Simba miaka 16 kurejea tena kwenye hatua ya makundi ilipofanya hivyo mwaka 2019 chini ya Kocha Patrick Aussems. Ilikuwa ni historia kubwa kwa Mnyama na nchi kwa ujumla.
Wakati ikiwachukua Simba miaka 16 kurejea mafanikio hayo, Yanga imewachukua miaka 25 kufika hatua ya makundi tena. Imefanya hivyo mwaka huu. Yaani wakati Yanga inacheza hatua ya makundi kwa mara ya kwanza mwaka 1998, Rais wa sasa wa Yanga, Mhandishi Hersi Said alikuwa kidato cha kwanza. Ni muda mrefu kweli.
Wakati Yanga ikisubiri kufika hatua ya makundi kwa mara nyingine, Simba ilicheza hatua ya makundi kwa mara nne na mwaka huu imefika kwa mara ya tano. Sio kucheza makundi tu, lakini ilivuka hadi robo fainali wakati mwingine ikiongoza kundi mbele ya vigogo kama Al Ahly. Bado kuna ulinganishi hapo? Hakuna.
Wakati Yanga ikisubiri kufika angalau hatua ya makundi kwa miaka 25, Simba imefika robo fainali ya mashindano hayo kwa mara tatu. Kwa sasa inalenga kufika hatua ya nusu fainali.
Ni wazi kuwa katika mashindano haya kuna mengi Yanga inapaswa kujifunza kwa Simba. Imefanikiwa vipi kucheza hatua ya robo fainali mara nyingi? Kuna kazi kubwa inafanyika.
Kufika fainali ya Kombe la Shirikisho kwa Yanga mwaka huu ni darasa. Kuna uzoefu wamepata. Hata hivyo kwenye Ligi ya Mabingwa mambo ni tofauti kabisa. Huku kuna vigogo wakubwa. Inabidi kukaza msuli kweli kweli.
Yanga imepangwa kundi moja na Al Ahly ya Misri. Hawa ni watetezi. Simba katika miaka mitano iliyopita amekutana na Ahly kwenye kundi moja mara mbili. Mara ya kwanza ilikuwa 2019, Simba ikashika nafasi ya pili. Ikafuzu robo fainali na Ahly.
Ikakutana kundi moja tena mwaka 2021. Simba ikaongoza kundi mbele ya Al Ahly. Ni ajabu na kweli.
Mbali na Ahly, Yanga ipo na CR Belouizdad ya Algeria na Medeama ya Ghana. Hapa mtihani mkubwa kwa Yanga ni kuvuka kwenda robo fainali. Atakwenda na nani? Tusubiri kuona kama atafanya maajabu ya Simba ya mwaka 2019.
Kwenye kundi la Simba kuna Wydad Casablanca, Jwaneng Galaxy ya Eswatin na ASEC Mimosas ya Ivory Coast. Rekodi ya Simba inawaweka katika nafasi mbili za juu za timu zinazoweza kuvuka kwenda robo fainali. Japo kwenye uhalisia ni kundi gumu pia, lakini Simba imewahi kuvuka makundi magumu zaidi ya hili.
Kama Yanga itajifunza kwenye mafanikio ya Simba hapa karibuni, tunaweza kuona timu mbili za Tanzania zikifika robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa msimu huu.
Yote kwa yote, Ijumaa ni ufunguzi wa African Football League. Simba itacheza na Al Ahly kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa.
Mara mbili za mwisho kwa Ahly kucheza na Mnyama kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, ilipasuka. Itakuja na jipya gani mwaka huu? Tusubiri tuone!