Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kwa Benchikha lolote linaweza kutokea

Benchikha Kibarua Kwa Benchikha lolote linaweza kutokea

Sun, 14 Apr 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Kwa zaidi ya dakika tano, Kocha Mkuu wa Simba, Abdelhak Benchikha alionekana kusalia kwenye Uwanja wa Liti, mjini Singida huku akionekana kuzama katika tafakari nzito mara baada ya kushuhudia kikosi cha timu hiyo kikishindwa kuonyesha makali wakati wa mchezo wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Ihefu uliopigwa jana, mjini humo.

Nini kilitokea? Simba ambayo inaonekana kutokuwa na makali katika safu yake ya ushambuliaji ilifikisha mchezo wa nne mfululizo kucheza katika mashindano yote bila ushindi kwa kutoka sare ya bao 1-1 na wenyeji wao waliotangulia kupata bao dakika ya 41 lililofungwa na Mkenya Duke Abuya.

Mambo yalianza kuiendea kombo Simba katika michezo miwili ya hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa kufungwa nje ndani na Al Ahly ya Misri ikilala nyumbani 1-0 kisha kufungwa tena 2-0 ugenini na kutolewa michuanoni kwa jumla ya mabao 3-0.

Hata hivyo, walipoelekeza nguvu katika michuano ya ndani wakajikuta pia wakitolewa hatua ya 16 Bora ya Kombe la Shirikisho (FA) mbele ya Mashujaa kwenye Uwanja wa Lake Tanganyika, mjini Kigoma kwa mikwaju ya penalti (6-5) baada ya dakika 90 za pambano hilo kumalizika kwa sare ya 1-1.

Wakiwa na hesabu za Ligi Kuu pekee huku wakiwa nyuma kwa utofauti ya pointi saba (kabla ya kupunguza moja) na Yanga ambao wanaongoza msimamo huo wakiwa na pointi 52 kilele, Simba ilishindwa kutamba huku kocha wake akionekana wazi kutofurahishwa na kiwango cha timu yake.

Miongoni mwa matukio ambayo kocha huyo alichukizwa nalo ni pamoja na lile la mshambuliaji wake, Freddy Michael 'funga funga' kukosa bao la wazi.

Tukio hilo lilimfanya Benchikha kuvua kofia na kuitupa chini kwa hasira, kipande cha video ikionyesha kukadhabika kwa kocha huyo kimesambaa katika mitandao mingi ya kijamii kikihusishwa na tukio hilo.

Pia kitendo cha Benchikha kumfokea Freddy katika mchezo wa ligi dhidi ya JKT Tanzania kutokana na kushindwa kulinda mipira ambayo wenzake walikuwa wakimpasia hivyo huu, ni mwendelezo ya kufanya vibaya kwa mrithi huyo wa Jean Baleke.

TAHADHARI MAPEMA Benchikha ni miongoni mwa makocha wenye CV kubwa, uzoefu na uwezo mzuri wa kufundisha soka, pia ni miongoni mwa makocha wasio wavumilivu wa nyakati ngumu Katika Kazi yake.

Moja wapo ya maamuzi magumu kuwahi kuyachukua ni mwaka 2011 akiwa kama Kocha mkuu wa timu ya Taifa ya Algeria, alichukua alijiuzulu baada ya kufungwa mabao manne na timu ya Taifa ya Morocco katika mwendelezo mbovu wa matokeo katika timu yake hiyo.

Mwaka 2023 akiitumukia USM Alger, licha ya Mafanikio makubwa aliyoyapata klabuni hapo ikiwemo kutwaa kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Yanga, alijiuzulu kuifundisha Klabu hiyo kutokana na tukio la kuzomewa na mashabiki wakati na baada ya mechi kuisha Katika mwendelezo wa mechi za ligi kuu Algeria.

Kituo kinachofuata kwa Simba ni dhidi ya Yanga, nini kitatokea, ni suala la muda na kusubiri Jumamosi ijayo ya Aprili 20.

Je, Benchikha atabadili upepo wa mambo na kurejesha wimbi la ushindi Msimbazi au ataendelea pale alipoishia Roberto Oliveira 'Robertinho', aliyekumbana na kipigo cha aibu cha mabao 5-1 katika derby ya kwanza iliyopigwa Novemba 5 mwaka jana na kumfutisha kazi Msimbazi? Tusibiri tuone itakuwaje?

Chanzo: Mwanaspoti
Related Articles: