juzi usiku Yanga ilikamilisha jumla ya timu nne zilizotinga nusu fainali ya michuano ya Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC) baada ya kuifunga Geita Gold kwa bao 1-0 katika pambano kali la robo fainali lililopigwa Uwanja wa Azam Complex, jijini Dar es Salaam.
Ushindi huo uliifanya Yanga kuungana na timu za Singida Big Stars, Azam na Simba zilizotangulia mapema. Singida ikiifunga Mbeya City kwa mabao 4-1, Azam ikiing’oa Mtibwa Sugar kwa mabao 2-0 na Simba kuinyoosha Ihefu kwa mabao 5-1.
Mechi hizo za nusu fainali zinatarajiwa kupigwa kwenye viwanja vya Nangwanda Sijaona, Mtwara na Liti, mkoani Singida huku fainali ikirejeshwa kule kulitokea mtafaruku mwaka jana, yaani Mkwakwani jijini Tanga.
Mechi hizo zinazungushwa mikoani katika kile kinachoelezwa kuwa ni kutangaza mpira wa miguu na kuipa nafasi mikoa yote kushuhudia mechi za mashindano makubwa.
Tayari mechi za nusu fainali zimeshawahi kuchezwa mikoa tofauti tangu mtindo huo wa kusambaza soka uanze kutumiwa kwenye michuano ya Kombe la TFF, ambalo linadhaminiwa na Azam.
Binafsi sioni mantiki ya kueneza soka kwa kutumia mashindano ya klabu, labda tu kama ni ile inayochezwa kwa kituo, yaani michuano ya wiki moja au mbili kama Ligi ya Mabingwa wa Mikoa (RCL).
Lakini kutumia michuano ya mtoano eti kuusambaza mchezo wa mpira wa miguu sioni kama ni sahihi. Badala yake mtindo huo utajumuisha gharama kubwa za mechi kutokana na ukweli kundi la watu wengi litasafirishwa kwenda kwenye mechi hizo, lengo hasa likiwa ni “ambiance”.
Huwa tunaona orodha ya maofisa wa mechi inayotolewa na Shirikisho la Soka (TFF) kila wakati kabla ya mechi za hatua ya juu, hasa fainali kiasi ilikuwa ajabu hakuna ofisa hata mmoja aliyejitokeza katika sakata la Rais Wallace Karia na Haji Manara wakati orodha ya maofisa wa mechi hiyo ilikuwa takriban watu 18 waliotoka mikoa tofauti wakiwemo maofisa wa itifaki na ulinzi, ambao wangeweza kumdhibiti Haji kabla ya kumkaribia Karia.
Lakini langu leo si hilo. Langu ni kuhusu kuzururisha mechi za hatua ya juu za michuano ya Kombe la Azam, badala ya viwanja kutegemea orodha ya ubora kama inavyofanyika kwa wenzetu, ila fainali ndio inayopelekwa kwenye uwanja mahususi.
Wenzetu uwanja kama wa Mkapa unatumiwa zaidi na timu za taifa, hasa kwenye mechi muhimu. Angalia Wembley au Allianz Arena au Olimpia Stadium wa Berlin, ambao una historia kibao za Olimpiki.
Lakini timu ya taifa ya nchi inaweza kutumiwa kusambaza mapenzi ya soka kwa kuipeleka viwanja tofauti na vyenye hadhi ili wananchi wa maeneo tofauti wasioweza kusafgiri umbali mrefu nao waione.
Lakini hilo pia litategemea masuala mengine kama viwanja vya kimataifa vya ndege kwa kuwa timu ya taifa inatakiwa icheze na timu za mataifa mengine.
Hawa wa klabu hawana budi kuhakikisha timu kutoka maeneo yao zinafanya kazi ya kuhakikisha zinapanda kucheza ligi za juu ili kuwapa nafasi mashabiki wao waone timu kubwa zikija mikoa yao.
Tusipofanya hivyo tunaendelea kujenga wigo mkubwa zaidi kwa Simba na Yanga, ambazo ni nadra sana kushindwa kufikia hatua za kuanzia robo fainali za michuano ya Kombe la Azam. Kwa hiyo, ukipeleka mechi ya nusu fainali inayohusisha Yanga au Simba dhidi ya timu nyingine, ambayo pia si ya mkoa huo, unakuwa umewapa Yanga au Simba nguvu zaidi kwa kuwa watajaza uwanja kuzomeana.
Lakini Singida Big Stars akicheza nyumbani dhidi ya Yanga katika nusu fainali, ana uhakika wa angalau robo ya mashabiki kuwa ni wale halisi huku wakipewa nguvu na mashabiki wa Simba ambao ni nadra kukosekana katika mtanange kama huo, kama ambavyo ingekuwa kwa Azam wangecheza uwanja wao wa Azam Complex.
Timu hizo zikifuzu mara nyingi kucheza hatua hizo na mechi zikafanyika kwenye viwanja vyao, hakuna shaka kuwa zitakuwa zimeongeza idadi ya mashabiki kuliko kwenda kucheza uwanja usio na mwenyeji, lakini kihalisia Simba au Yanga ndio wenyeji.
Waingereza wameziheshimisha mechi za hatua za juu za michuano yao ya Kombe la FA kwa kuzipeleka kwenye Uwanja wa Wembley, jijini London. Wembley ni uwanja ambao kila mwanasoka anayecheza Ligi Kuu ya England anaota kuwa siku moja acheze hapo kwa kuwa huwezi kucheza kama hujafikia hatua za juu za michuano mikubwa.
Uwanja huo hautumiki hovyo hovyo kwa mechi zisizo na umuhimu labda kwa maombi maalum.
Leo hapa, hakuna mchezaji wa Ligi Kuu anayeota kucheza kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, kwa kuwa ni wa kawaida licha wageni kuushangaa wanapokuja Tanzania. Wachezaji wa Ligi Kuu na hata Ligi Daraja la Kwanza wameshazoea kucheza Kwa Mkapa kwenye mechi tofauti na baadhi zisizo hata na hadhi hiyo.
Wapo wanaopata nafasi ya kuutumia hata kwa mechi za mabonanza ya mashirika au taasisi nyingine, achilia mbali wale wanaoenda hapo kwa ajili ya matamasha mengine.
Matokeo yake ni ubora wa uwanja kuzidi kuporomoka, kiasi kwamba picha za televisheni zinazopigwa wakati wa mechi huonyesha wazi wazi maeneo yenye nyasi za rangi ya kahawia inayoashiria kukauka au kuwa na magonjwa.
Kwa kuona hivyo Shirikisho la Soka la Afrika (CAF) eti limetushauri tuupumzishe. Yaani sisi wenyewe hatuoni kama tunauchosha hadi tushauriwe na wageni ambao kutokana na uzuri wa Uwanja wa Mkapa wanataka kuutumia kwa mashindano mengine makubwa.
Bila ya ushauri huo, uwanja ungeendelea kutumika kana kwamba hauhitaji matunzo maalum ya kuufanya uendelee kubakia na ubora wake.
Wakati Wakenya walipoutumia Uwanja wa Kasarani kwa ajili ya sherehe za kuapishwa Uhuru Kenyatta, waliufunika kwa zuria ili magari yasiuharibu. Sisi hatujafanya shughuli za kisiasa Uwanja wa Mkapa, lakini matamasha yamekuwepo.
Najaribu kuonyesha athari za kutouthaminisha Uwanja wa Benjamin Mkapa kiasi cha kuonekana wa kawaida na hivyo kukimbizia mechi za hatua ya juu ya Kombe la Azam kwenye viwanja vingine kwa kisingizio cha kusambaza soka.
Katika hali ya kawaida mechi za hatua ya juu ya Kombe la Azam ndizo zilizotakiwa zichezwe Kwa Mkapa badala ya mechi kibao za Ligi Kuu. Mbali na kuzifanya mechi hizo kuwa na hadhi kubwa, pia zinampa hata mdhamini fursa ya kutangazwa zaidi kwa kuwa Uwanja wa Mkapa upo katika jiji ambalo lina vyombo vingi vya habari ambavyo husaidia kuongeza thamani ya udhamini.
Hatuwezi kusambaza mpira wa miguu kwa kuzunghusha mechi za michuano ya juu ya klabu, bali kwa kuihimza klabu katika mikoa kufanya juhudi kubwa kupanda daraja. Na hii itaongezwa nguvu kwa kukuzwa soka la vijana ambalo litatoa wachezaji wengi wenye uwezo wa kupambania klabu zao hadi hatua za juu.
Kuzungusha mechi za hatua za juu za michuano ya klabu ni siasa ambayo haisaidii soka kukua.