Uongozi wa Simba umetangaza kiingilio cha Sh5000 hadi Sh200,000 kwa mashabiki wake wanaotaka kushuhudia mechi ya mwisho ya Kundi B ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Jwaneng Galaxy.
Akizungumza na wanahabari leo Afisa Habari, Ahmed Ally amewaomba mashabiki wa timu hiyo kujitokeza kwa wingi kwenye mchezo huo unaotarajiwa kuchezwa Jumamosi hii kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa.
Ahmed ametangaza bei ya chini ya tiketi za kuingia uwanjani ni Sh5000 kwa majukwaa ya mzunguko wakati VIP B ni Sh20,000, VIP C Sh10,000 na VIP A itakuwa Sh30,000.
Mbali ya kuwepo na tiketi hizo ambazo zimezoeleka kutakuwa na tiketi za Platinum zitakuwa zikiuzwa kwa Sh150,000 kwa watu maalumu na VVIP Sh200,000, pia kutakuwa na tiketi za vikundi maarufu kama Mnyama Package ambazo zitakuwa zinahitaji mashabiki kuanzia 20 na Executive Tickets kwaajili ya wafanyakazi wa kampuni mbalimbali ambao wanataka kuingia kwa pamoja na kukaa sehemu moja.
Wawakilishi hao wa Tanzania wataingia katika mchezo wa siku ya Jumamosi dhidi ya Jwaneng Galaxy kwa malengo mawili kwanza kulipa kisasi cha kufungwa mabao 3-1 jijini Dar es Salaam, pili kuhakikisha wanapata ushindi wa angalau bao 1-0 ili kutinga hatua ya robo fainali ya CAF kwa mara ya tano ndani ya miaka sita.
Simba ina pointi sita katika nafasi ya pili, sawa na Wydad Casablanca iliyo katika nafasi ya tatu, huku Jwaneng ikishika mkia kwa pointi nne. Asec Mimosas imeshafuzu ikiwa na poini 11 kileleni mwa Kundi B.
Wekundu wa Msimbazi wanahitaji kushinda tu ili kwenda robo fainali. Mchezo huo muhimu kati ya Simba na Jwaneng utachezwa kwenye Uwanja wa Mkapa kuanzia saa 1:00 usiku.