Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kuwakabili Waangola, tizi la Simba sio kitoto

Bocco Tizi Nahodha wa Simba John Bocco

Sat, 15 Oct 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Licha ya kupata ushindi mnono wa mabao 3-1 ugenini dhidi ya Primeiro de Agosto, Jumapili iliyopita, Simba imepania kuwazima kabisa wikiendi hii kuepuka kile kilichotokea msimu uliopita mbele ya Jwaneng Galaxy katika hatua hiyo.

Msimu uliopita walijikuta wakitupwa nje ya mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa kanuni ya bao la ugenini baada ya kupokea kichapo cha mabao 3-1 nyumbani kutoka kwa Jwaneng Galaxy ya Botswana licha ya kupata ushindi wa mabao 2-0 katika mchezo wa kwanza ugenini.

Jumanne asubuhi walirejea kambini kujiandaa na mechi dhidi ya Agosto itakayochezwa katika Uwanja wa Benjamin Mkapa kuanzia saa 10:00 jioni ambapo walianza na mazoezi ya kujiweka fiti waliyofanyia katika ‘gym’.

Baada ya hapo, juzi Jumanne walianza kufanya mazoezi ya mbinu uwanjani ambayo kwa kiasi kikubwa yalijikita katika kutengeneza wepesi na kasi.

Katika mazoezi ya juzi Jumanne, benchi la ufundi la Simba lilianza na program ya kuweka utimamu wa mwili na mnyumbuliko kwa kuwapa mazoezi tofauti wachezaji katika koni na vifaa vingine vya kuonyesha alama ambavyo vilipangwa.

Kocha Mkuu, Juma Mgunda na msaidizi wake, Selemani Matola walionekana kutotaka mchezo kwa wachezaji hao na kuthibitisha hilo, mtathmini wa viwango vya wachezaji wa timu hiyo, Kelvin Mavhunga aliwavalisha vifaa maalum vya kupima ufanisi wachezaji wote wa Simba waliokuwepo mazoezini ambavyo hutoa takwimu za kila mchezaji na ufanisi wake.

Baada ya hapo, wachezaji hao walihamia katika mazoezi ya kutengeneza nafasi na kufunga ambapo walianza kwa kushambulia kwa kasi na kutakiwa kupasiana kila wanapolikaribia lango na kisha kufunga.

Awali zoezi hilo lilikuwa ni baina ya wachezaji wa nafasi ya ushambuliaji na ile ya kiungo dhidi ya mabeki ambao walitakiwa kuzuia lakini baadaye, hata wale wa nafasi za ulinzi nao walitakiwa kushiriki katika kutengeneza nafasi na kufunga hasa wakitokea pembeni. kamilika kwa zoezi hilo kulifungua milango kwa lingine ambalo lilikuwa la mwisho nalo ni lile la kugawa timu mbili ambazo wachezaji wake walitakiwa kupigiana pasi za harakaharaka kuelekea kwa timu pinzani na kutakiwa kufunga pindi waliposogelea lango.

Katika zoezi hilo, straika Habibu Kiyombo na kiungo Augustine Okrah walionekana kuwa moto wa kuotea mbali kutokana na uwezo wao mkubwa walioonyesha katika kutumia nafasi.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live