Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kutoka kambi ya Azam FC... Ujio wa Samake ni uchungu kwa Akaminko, Navaro

Akaminkoooo Zali Kutoka kambi ya Azam FC... Ujio wa Samake ni uchungu kwa Akaminko, Navaro

Mon, 22 Jul 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Muda wa maisha ya James Akaminko ndani ya kikosi cha Azam FC unahesabika na dakika zinaenda kasi sana.

Wakati wowote kuanzia sasa chochote kinaweza kumtokea kiungo huyo aliyepata sifa kubwa katika msimu wake wa kwanza alipotua Chamazi.

Msimu wa 2024/25, Kocha Youssouph Dabo hakuona Akaminko kama ni mtu sahihi katika mipango yake, hivyo alimuweka kwenye orodha ya wasiotakiwa.

Lakini stori ya Adolf Bitegeko Mtasingwa kuhusishwa na Yanga iliwashtua Azam na kusitisha mpango wa ‘kumkata’ Mghana huyo.

Mbaya zaidi Bitegeko ambaye awali alisaini mkataba wa mwaka mmoja dirisha dogo lililopita, hakuipokea ofa ya nyongeza ya mkataba kutoka Azam.

Viongozi wakaamini anawasumbua kwa sababu tayari ameshasaini Yanga.

Kwa hiyo wakaamua kubaki kwanza na Akaminko, huku wakitafuta mtu sahihi katika eneo hilo kwa sababu Sospeter Bajana na Yahya Zayd ni majeruhi na watakosekana katika sehemu muhimu ya msimu, mechi za raundi ya awali ya Ligi ya Mabingwa Afrika, Azam ikipangwa kuumana na APR Rwanda, raundi ya kwanza.

Lakini sasa amepatikana Mamadou Samake, kiungo fundi kutoka CR Belouizdad ya Algeria, aliyewapoteza Yanga katika kipigo cha 3-0 katika mchezo wa kwanza wa hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa msimu uliopita.

Kukosekana kwake katika mchezo wa marudiano uliopigwa Dar es Salaam yawezekana ndiyo kulikuwa ahueni ya Yanga na kushinda 4-0.

Kwa hiyo, Akaminko hana tena nafasi Chamazi na alishaambiwa atatolewa kwa mkopo kwenda Coastal Union ya Tanga.

Hata hivyo, mwenyewe hakukubaliana na mkopo huo akisema ni bora avunjiwe mkataba aondoke zake.

Mkataba wake unataka alipwe Sh300 milioni endapo utavunjwa.

Mabosi wakakubali kumvunjia na wamlipe aondoke kwa sababu ya nafasi za wachezaji wa kigeni na kanuni inahitaji kila klabu kusajili wachezaji wasiozidi 12.

Mpango ulikuwa aondoke, ili Samake achukue nafasi yake.

Lakini mwamba akarudi kwa viongozi kuomba huruma kipindi cha usajili ni kama kimeisha, wakimuacha sasa ataenda wapi…kwa nini hawakumuacha mapema ili apate muda wa kutafuta timu.

Hii hoja nayo ikawa na mashiko kwa mabosi hivyo wakaamua kubaki naye.

Hata hivyo, hakukuwa na nafasi ya kumsajili Samake kama Akaminko atabaki…sasa itakuwaje?

Mungu bariki, ripoti ya madaktari ikafika kwa mabosi ikionesha kiungo Mcolombia, Franklin Navarro hajapona sawasawa majeraha yake.

Basi huyo ndio akapitiwa na panga na jina lake halikusajiliwa kwenye mfumo, akiungana na kina Alassane Diao na Ali Ahamada ambao nao ni majeruhi wa muda mrefu.

Nafasi kwa Samake ikapatikana kwa gharama ya Navarro, huku Akaminko akipumua kwa kunusurika.

Lakini haya mambo ya usajili huwa hayaishi hadi yaishe kabisa na dirisha lifungwe.

Kwa kuwa Azam, mipango yao ilikuwa kumwondoa Akaminko endapo atapatikana kiungo mzuri zaidi yake, mipango hii ikabaki hivyo hivyo baada ya kupatikana kwa Samake.

Mabosi wakaingia sokoni kutafuta timu kwa ajili ya Akaminko na sasa inakaribia kufanikiwa, kwani kuna vidogo wa Algeria wameulizia huduma yake na wanaonekana wako ‘serious’.

Kama hilo litafanikiwa, basi Akaminko hatakuwa sehemu ya Azam msimu ujao kama ilivyo kwa Franklin Navarro ambaye alijiunga na timu hiyo dirisha dogo la msimu uliopita akisaini mkataba wa mwaka mmoja.

Hii ina maana ikifika Desemba mchezaji huyo atakuwa amemaliza mkataba wake na sijui kama ataongezewa, kwani tangu aje amecheza mechi moja tu ya ligi dhidi ya Simba, tena kwa dakika zisizofika 20.

Kwa usajili wa Samake, Azam wanakuwa wamekamilisha harakati za dirisha hili na sasa wanaelekeza nguvu, akili ha muda kwenye maandalizi ya msimu mpya.

Kocha Dabo ambaye aliondoka hapa Morocco wikendi iliyopita kurudi Tanzania kuhudhuria kozi ya CAF ya Diploma A, anataka kujenga kikosi chenye uwezo wa kutoa ushindani wa kweli kwenye mashindano yote msimu ujao.

Kuhusu Ligi ya Mabingwa ambayo Azam wameitolea macho kweli kweli, Dabo anasema timu yake ina nafasi kubwa licha ya kupangwa katika njia ngumu.

"Azam haijawahi kufika hatua ya makundi na safari hii njia sio rahisi. Lakini hakuna njia rahisi katika Ligi ya Mabingwa. Hawa ni mabingwa na unatakiwa kupambana nao ili nawe uwe 'level' zao."

Dabo anawalenga Pyramids kutoka Misri anaposema hivyo, japo mwenyewe anasema hata APR ni wakubwa kuliko Azam kwa hiyo kabla ya Pyramids kwanza lazima kuwaheshimu hawa Wanyarwanda.

"Si unawaona kwenye CECAFA, wako fainali na wamewatoa Al Hilal, timu bora kabisa. Maana yake wanajua kuzicheza mechi za mtoano na inabidi tujipange hasa."

Dabo anakumbuka maajabu ya Tengueth, timu yake ya Senegal iliyoitoa Raja Casablanca mwaka 2021.

"Kila mtu alitukatia tamaa baada ya kupangwa ma Raja, lakini tuliwatoa, acha tuone na safari hii itakuwaje," anamalizia Dabo ambaye timu kamuachia msaidizi wake, Bruno Ferry.

Kwenye makaratasi ya TFF, Azam FC walimuandikisha Ferry kama Kocha Mkuu na Dabo kama msaidizi wake kwa sababu za kisheria.

Dabo ni kocha mwenye Diploma A ya UEFA aliyoisomea Ufaransa, ambayo kwa Afrika inahesabika kama Diploma B ambayo haitoshi kwa Kocha Mkuu wa timu ya Ligi Kuu Bara.

Bruno Ferry ni kocha mwenye Diploma A ya CAF aliyoisomea Senegal, ambayo ndio inatakiwa kisheria kwa kocha mkuu wa Lgi Kuu Bara.

Kwa hiyo, Azam walimuajiri Dabo kwa sababu ya uwezo, lakini wakampa nafasi ya kutafuta mtu mwenye cheti kinachokubalika Tanzania, ili aandikishwe kama kocha mkuu.

Dabo ndiyo akamleta Bruno Ferry…akaandikishwa. Lakini sasa kwa kusoma kwake huku, maana yake akimaliza na kufaulu, mambo yatabadilika na kutambulika kama kocha mkuu wa kikosi hicho ambacho juzi usiku kilipata ushindi wa mabao 3-0 katika mchezo wa kirafiki wa kujipima nguvu ikiwa kambini Morocco.

Azam ilipata ushindi huo dhidi ya US Yacoub Al Mansour ya Morocco kupitia mabao ya Cheikh Sidibe aliyefunga kwa penalti, Gibril Sillah na Jhonier Blanco aliyefikisha bao la tatu tangu ajiunge na timu hiyo.

Chanzo: Mwanaspoti