Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kutoka De Gea mpaka Onana, udadisi ulimuua paka

Andre Onana Ten.jpeg Kutoka De Gea mpaka Onana, udadisi ulimuua paka

Sun, 1 Oct 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Wazungu wana msemo wao. Wanasema ‘Curiosity killed a cat.’ Kwamba udadisi uliopitiliza ulimuua Paka. Paka ana tabia ya kuchunguzachunguza vitu. Vingine vinamuangukia vinamdhuru au kumuua kabisa.

Erik Ten Hag naye alikuwa miongoni mwa makocha ambao hivi karibuni aliamua kuingia katika mfumo mpya wa soka ulioletwa na kina Pep Guardiola. Mfumo wa timu kucheza kuanzia nyuma kabisa. Kuanzia kwa kipa.

Kwamba kipa lazima awe na matumizi mazuri ya miguu. Ni kweli. Ni mfumo unaonea kwa kasi. Kuna makipa ambao huwezi kuwatofautisha na wachezaji wa ndani. Wanatumia zaidi miguu kuliko mikono.

Lilikuwa suala la muda tu David De Gea kuondoka katika lango la Manchester United. Ni kweli matumizi yake ya miguu hayapo vizuri. Uwezo wake wa kutawanya mipira kuanzia chini upo duni. Kuanzia katika kurudishiana pasi na mabeki wake hadi kupiga pasi ndefu kwa wachezaji wa mbele De Gea alikuwa duni.

Akaletwa kipa Andre Onana kutoka Italia. Kipa wa kwanza Mwafrika kusimama katika lango la Manchester United. Furaha iliyoje kwa Waafrika.

Sio kitu cha kawaida sana. Sir Alex Ferguson hakuvutiwa na wachezaji wa Afrika kuanzia ndani hadi langoni. Lakini Ten Hag alimuamini Onana.

Hakumuamini kwa sababu ya Uafrika wake. Hapana, na yeye aliingia katika udadisi ule ule wa kutaka kuona timu yake inacheza kuanzia nyuma. Inacheza na golikipa ambaye ana matumizi mazuri ya miguu. Na sasa tunahisi kwamba huenda udadisi wake ukaiua timu.

Ni kweli Onana ni mzuri kuliko De Gea linapokuja suala la matumizi ya miguu. Ni kama vile anafanya masikhara langoni lakini uwezo wake wa kucheza kwa miguu ni mkubwa.

Tatizo ni kwamba katika mashuti saba aliyopigiwa langoni mashuti saba yamekwenda katika nyavu.

Achana na bao alilofungwa kizembe zaidi katika pambano la Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Bayern Munich, Onana amefungwa mabao mengine ambayo katika hali ya kawaida unaweza kudhani alistahili kufungwa lakini kama David de Gea angekuwa langoni si ajabu yasingefungwa.

Kwa miaka mingi, licha ya udhaifu wake wa hapa na pale lakini De Gea ndiye kipa ambaye ametupa kitu kinachoitwa ‘saves’ za uhakika miongoni mwa makipa wengi wa Ligi kuu ya England.

Hapa karibuni kichwa chake kilikuwa hakijakaa sawa lakini De Gea katika ubora wake aliwahi kuwa mchezaji bora wa Manchester United kwa misimu mitatu mfululizo.

Na hata sasa, linapokuja suala la michomo bado naona kabisa Onana hamuwezi De Gea. Linapokuja suala la miguu unaona kabisa De Gea hamuwezi Onana. Kupanga ni kuchagua. Onana ameturudisha tena darasani huku tukijiuliza, ni jambo gani bora.

Kuwa na kipa mwenye uwezo mkubwa wa kucheza kwa miguu au kuwa na kipa ambaye ana uwezo mkubwa wa kuokoa michomo lakini ana udhaifu miguuni.

Kuna timu zina bahati kuwa na makipa wenye vitu vyote hivi viwili. Manchester City ina Ederson. Liverpool ina Allison Becker. Lakini pia nimejua kwanini Timu ya Taifa ya Hispania ilimuacha De Gea katika Kombe la Dunia pale Qatar na badala yake ikaenda na David Raya wa Brentford ambaye kwa sasa ametua Arsenal.

Raya anaonekana kuwa na vyote. Miguuni yupo vizuri lakini pia anajua kuokoa michomo. Huu ni mjadala wa siku nyingine wa namna ambavyo amefanikiwa kumchomoa Aaron Ramsdale katika lango la Arsenal. Waingereza hawatapenda lakini ndio hali halisi.

Tukirudi katika lango la Manchester bado tunaweza kumpa muda Onana lakini inabidi ajirekebishe haswa. Kwa aina ya mabao ambayo ameshafungwa mpaka sasa ni wazi kwamba anahitaji kujirekebisha kukaa katika lango hilo.

United inapitia katika kipindi kigumu tangu kuondoka kwa Sir Alex Ferguson. Hakuna kocha wala mchezaji ambaye amekuwa salama kwa muda mrefu. Makocha wanabadilika na wachezaji wanabadilika.

Fikiria namna Ole Gunnar Solskjaer alivyotoa pesa nyingi kwa Harry Maguire lakini Erik Ten Hag amekuja kumuondoa katika nafasi yake na pia amemvua kitambaa cha unahodha.

Kama Onana ataendelea kufungwa mabao ya kijinga basi haitasaidia kitu katika suala zima la kuonyesha uhodari wake katika kutumia miguu yake.

Na muda si mrefu atatufungulia mjadala wa jambo ambalo ni muhimu zaidi kwa golikipa. Kuwa uhodari miguuni au mikononi?

Achilia mbali kuimarisha nafasi yake katika kikosi cha United lakini Onana anapaswa pia kutuheshimisha Waafrika katika lango la timu kubwa kama Manchester United.

Makipa kutoka Afrika, waliozaliwa Afrika huwa hawaaminiki katika milango ya timu kubwa barani Afrika.

Edouard Mendy alidaka Chelsea kwa sababu amezaliwa Ufaransa licha ya kwamba anachezea Timu ya Taifa ya Senegal. Makipa wa Afrika waliwahi kutamba katika timu za kawaida barani Ulaya lakini hawakuwahi kugusa katika timu kama Barcelona, Real Madrid, Juventus, Manchester United, Chelsea na kwingineko.

Huko huwa tunaweza kupeleka watu wa kusukumana na kukimbizana kama akina Didier Drogba, Michael Essien, Geremi Njitap, Samuel Etoo na wengineo.

Lakini nafasi ya kipa au kiungo mshambuliaji huwa hawatupi. Nadhani wanahisi hatustahili kupewa majukumu hayo.

Ukiona timu kama United imemuamini Onana basi ni nafasi ambayo anapaswa kudhihirisha kuwa Waafrika tunaweza. Tatizo ameanza kututia mashaka mapema. Kwa sasa tunaruhusiwa kumpa muda lakini asichelewe sana.

Asiipeleke United katika ule usemi kwamba udadisi ulimuua Paka.

Asimfanye Ten Hag aonekane kichekesho na inaonekana kama vile udadisi wake wa kutaka kumpata kipa anayetumia vizuri zaidi uwe wa kijinga zaidi. Wanaweza kuondoka wote wawili katika kikosi cha Manchester United.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live