Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kuta chujio Ligi Kuu Bara

Aishi Manula Back.jpeg Aishi Manula

Thu, 14 Dec 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Ligi Kuu Bara msimu huu (2023/24) inaendelea huku Azam FC ikiwa kinara kwenye msimamo baada ya kucheza mechi 12 ikikusanya pointi 28 na rekodi mbalimbali zikiwekwa. Kuna rekodi mbaya miongoni mwake ni hii ya timu ambazo zimeruhusu mabao mengi hadi sasa.

Iko hivi. Ni timu 16 zinazoendelea kupepetana huku mizunguko ikiwa ni tofauti kwa timu zote kwani baadhi ya zimecheza mechi nyingi zaidi, nyingine zikicheza michezo michache kutokana na kuwa na ratiba ngumu.

Licha ya hayo yote katika mechi zilizochezwa hadi sasa imeonekana timu nyingi zimekosa ubora na umakini eneo la ulinzi kwani kati ya timu 16 ni tatu pekee zilizofungwa mabao chini ya 10.

Hivyo, timu nyingine 13 zimefungwa mabao kuanzia 10 na kuendelea ambayo kwa hesabu za haraka ni wastani wa kuruhusu bao kwenye kila mechi kutokana na idadi ndogo ya michezo waliyocheza hadi sasa.

Timu hizo zimetumia makipa tofauti, lakini hilo halijazifanyi kuepuka kufungwa kwani mara nyingi zilijikuta tu mpira umetingia nyavuni. Kupitia makala haya utapata kuzijua timu hizo huku tatu zilizokwepa vipigo vya mabao mengi zikiwa ni mabingwa watetezi Yanga, Kagera Sugar na Azam FC.

Mtibwa Sugar - 24

Wakata Miwa hawa wa Turiani ndio wanaongoza kufungwa mabao mengi zaidi, nyavu zao zimetikiswa mara (24) kwenye michezo 12 waliyocheza hadi sasa huku wakifunga mara 11 tu.

Mtibwa imewatumia makipa wawili tu Razack Shekimweli na Mohamed Makaka, kila mmoja ameruhusu nyavu kutikiswa mambo yamekuwa ndivyo sivyo kwa timu hiyo ambayo inaburuza mkia.

KMC FC-19

Licha ya kuwa na mwendelezo mzuri lakni langoni kwao kuna ‘Chujio’ kwani mechi 12 ilizocheza hadi sasa, imefungwa mabao 19, ikishika nafasi ya pili kwa kutunguliwa.

Chama hilo msimu huu limemtumia kipa mmoja tu ambaye ameruhusu mabao yote hayo, Wilbol Maseke lakini mambo bado yamegonga mwamba na wapinzani kufunga mara kwa mara.

Vipigo vikubwa alivyokutana navyo kipia huyo hadi sasa ni dhidi ya Yanga 5-0 na Azam FC 5-0, hivyo amefungwa mabao 10 kwenye mechi mbili huku mengine tisa katika mechi nyingine 10, licha ya ukuta kuwa mbovu mabao yake ya kufungwa yanaendana sambamba na kufunga kwani imefunga mabao 19.

Tanzania Prisons-16 Wabishi hawa wa Jiji la Mbeya nao langoni kwao kupo hoi msimu huu, wamefungwa mabao 16 hadi sasa huku safu yao ya ushambuliaji ikifunga mabao 13 kwenye mechi 12 walizocheza.

Timu hiyo ipo nafasi ya 11 kwenye msimamo wa ligi imetumia kipa mmoja tu ambaye ni Yona Amosi ambaye anaongozwa na safu ya ulinzi inayoundwa na mabeki tofauti tofauti.

Ihefu FC-16

Mbabe wa Yanga kwa misimu miwili mfululizo amefunga ikishinda idadi ile ile ya mabao 2-1 nayo ina hali mbaya, mechi 13 ilizocheza imefungwa mabao 16 huku ikifunga 10.

Imemtumia kipa mmoja tu mechi zote 13 ilizocheza, imekubali nyavu zake kutikiswa kwa idadi kubwa ya mabao, kocha wa makipa huenda akalazimika kumbadilisha kutumia kipa mwingine.

Mashujaa-15

Ni msimu wake wa kwanza Ligi Kuu, ilianza vizuri mechi zake tano za kwanza baada ya hapo dhahama ipo upande wake kwani imekuwa timu ya kujipigia kila ilipokutana na timu pinzani.

Mashujaa imewatumia makipa wawili hadi sasa Lameck Kanyonga na Hashim Mussa kwenye mechi 12 ilizocheza na makipa hao wote wameruhusu nyavu zao kutikiswa.

JKT Tanzania-15 Maafande hawa wa JKT Tanzania wamepanda daraja msimu huu kipigo chao cha kwanza kikubwa walichokutana nacho ni dhidi ya Yanga wakikubali kufungwa mabao 5-0.

Licha ya kutumia makipa wote watatu, bado shida ya nyavu zao kutikiswa mara kwa mara ipo palepale kutokana na kuruhusu mabao mengi wamemtumia Mrisho Mussa, Ismail Salehe na John Mwanda wote wakihusika kwenye mabao hayo.

Geita Gold- 14

Wachimba madini hawa wa Mjini Geita nao msimu huu makipa wao wameokata mpira kwenye nyavu mara 14 katika mechi 12 walizocheza hadi sasa.

Geita msimu huu wamewatumia makipa watatu, Costantine Malimi, Joseph Joseph na Samson Sebusebu na wote kila mmoja wamefungwa kwa wakati wake.

Dodoma Jiji-13

Walima Zabibu hawa wa Dodoma nao wametobolewa kinoma kwenye ligi wamefungwa mabao 13 katika mechi 12 walizocheza hadi sasa huku wao wakifunga 11.

Msimu huu pia Dodoma imewatumia makipa wanne, Mohamed Hussein, Aron Kalambo, Daniel Mgore na Katunzi kila mmoja kapewa dozi.

Simba -11 Licha ya usjili mkubwa waliofanya dirisha kubwa la usajili pia wamekuwa wahanga wa timu zilizopigwa mabao kuanzia 10 na kuendelea wakiruhusu mabao 11 kwenye nyavu zao.

Simba kwenye idadi hiyo ya mabao imewatumia makipa watatu Ally Salim, Aishi Manula ambaye amefungwa mabao matano kwenye mechi moja na Ayoub Lakred.

Coastal Union-11 Ipo nafasi ya saba kwenye msimamo licha ya kuruhusu mabao 11 kutikiswa nyavu zake imefunga mabao 10 tu hivyo wastani ni wakifunga wanafungwa unalingana. Imewatumia makipa watatu Ley Matampi, Justin Ndikumana na Robert Chuma. Ni kama Tabora United ambayo ni msimu wake wa kwanza imefungwa 11 pia hadi sasa.

Namungo FC-10 Imenolewa na makocha wawili msimu ukiwa bado haujamaliza ilianza na Cedrick Kaze na sasa imeachana na Denis Kitambi imeruhusu nyavu zake kutikiswa mara 10. Kwenye mabao hayo, imewatumia makipa wawili wazoefu Deogratus Munishi ‘Dida’ na Jonatahan Naimana wote wakitunguliwa kwa nyakati tofauti.

Chanzo: Mwanaspoti