Mchezo wa mkondo wa kwanza wa hatua ya mtoano (play off) baina ya Moro Kids ya Morogoro na Kurugenzi FC ya Simiyu umeshindwa kufanyika baada ya Kurugenzi kushindwa kufika katika mchezo uliopangwa kuchezwa leo, Aprili 27 kwenye Uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro.
Mchezo huo maalumu wa kutafuta timu itakayocheza First League maarufu Ligi Daraja la Pili kwa msimu ujao, ulipangwa kuzikutanisha timu hizo huku Kurugenzi wakitetea nafasi yao ya kubaki First League ilhali Moro Kids wakisaka kupanda kucheza ligi hiyo kwa mara ya kwanza.
Msimamizi wa mchezo huo, Moses Mashoto amesema wameuahirisha mchezo huo kikanuni baada ya Kurugenzi kushindwa kufika kwenye kituo bila taarifa yoyote.
"Kikawaida mchezo unaanzia kwenye kikao cha mchezo cha asubuhi na wenzetu hawakufika na hawakutoa taarifa, na hata muda wa mchezo ulipowadia hawakutokea. Kwa mujibu wa kanuni tumesubiri mpaka dakika 30 kisha tukaahirisha mchezo kwa mujibu wa kanuni zinazotuongoza," amesema Mashoto.
"Kilichofanyika sisi hatujawapa ushindi Moro Kids, bali tumeahirisha mchezo na jukumu la kutoa ushindi ni la Bodi ya Ligi. Tutakachofanya tutaandika taarifa ambayo kwa kile tulichoona na tutaiwasilisha Bodi kwa uamuzi zaidi."
Alipotafutwa na Mwananchi, Meneja wa Kurugenzi FC, Denis Nkulu amesema timu haijasafiri kutokana na kukosa fedha za nauli na wanajipanga kwa ajili ya adhabu yoyote itakayotolewa.
"Tulifanya maandalizi ya kucheza mechi lakini ulipofika muda wa kusafiri viongozi wetu wakasema hawana fedha za kutusafirisha ndiyo maana hatujasafiri. Na kwa hali ilivyo tunasubiri uamuzi wa TFF (Shirikisho la Soka Tanzania)," amesema
Kocha wa Moro Kids, Beda Sengo amesema walijiandaa kupata ushindi ili kujiweka katika mazingira mazuri ya kupanda daraja
"Tumefanya maandalizi yote kuhakikisha mchezo huu wa mkondo wa kwanza wa mtoano tunafanya vizuri, hata hivyo tutaendelea na maandalizi ili tukipangiwa kucheza mchezo wa pili tuwe timamu na tayari kupata matokeo," amesema Sengo.
Kwa mujibu wa kanuni ya 31 ya First League timu itakayoshindwa kufika uwanjani bila sababu za msingi zinazokubalika kwa TFF au Bodi ya Ligi na kusababisha mchezo usifanyike itakabiliwa na adhabu ya kupoteza ushindi na kushushwa madaraja mawili.
Kanuni hiyo inaongeza kuwa matokeo ya michezo yake yote yatafutwa au kupewa faida kwa timu zingine ambazo haijacheza nazo ili kutoa uwiano sahihi kwa timu zilizobaki kwenye ligi na endapo timu ilikuwa kwenye nafasi ya kushuka daraja timu hiyo itashushwa madaraja mengine mawili.