Vichwa vya habari vya vyanzo mbalimbali vya habari za michezo juma hili vimegubikwa na habari za uhamisho wa wachezaji mbalimbali hapa nchini. Habari hizi zinaongelea zaidi nani anatoka na nani anaingia hasa katika klabu kubwa za Yanga na Simba.
Azam ambayo imekuwa bize na usajili hata wakati ligi inaendelea haifuatiliwi sana na hivyo wanafanya mambo yao bila presha nyingi kutoka nje.
Kuna tetesi za wachezaji Stephane Aziz KI wa Yanga na Clatous Chama wa Simba ambao wamekuwa mihimili kwenye klabu zao, kutoongeza kandarasi.
Aziz Ki ndiye mfungaji bora na amechangia pakubwa Yanga kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Bara na Kombe la Shirikisho (FA) na tetesi hiz9i zinawashtua sana mashabiki wa timu hizi, ingawa si mara ya kwanza timu hizi zinapoteza nyota muhimu.
Simba iliwahi kumpoteza Chama na maisha yakaendelea ingawa wengine wanasema timu iliyumba alipokwenda RS Berkane ya Morocco.
Binafsi naona tatizo kubwa kwa Simba lilikuwa ni kushindwa kuwa na mpango wa kuziba mapengo ya Chama na Luis Miquissone aliyejiunga na Al Ahly ya Misri.
Msimu uliopita Yanga ilimpoteza mshambuliaji wake kinara, Fiston Kalala Mayele aliyeshinda taji la ubingwa wa Ligi Kuu Bara, Kombe la Shirikisho (FA), Ngao ya Jamii na medali ya mshindi wa pili wa Kombe la Shirikisho la Afrika (CAF Confederation Cup).
Pia alishinda tuzo binafsi ya mchezaji bora wa msimu, mfungaji bora mwenza wa msimu na mfungaji bora wa kombe la shirikisho barani Afrika.
Mlolongo wa mafanikio kupitia klabu na mafanikio binafsi ya Mayele yanaeleza kwa nini uhamisho wake uliongelewa sana si Tanzania pekee hata nje ya mipaka.
Baada ya mafanikio hayo, klabu za Afrika na Asia zilibisha hodi Yanga kusaka saini ya mkali huyo. Inawezekana Yanga iliponzwa na mafanikio yake.
Kumbuka hii ilitokea Yanga ikiwa imeshaagana na kocha aliyekuwa sehemu ya mafanikio yao Mtunisia Nasredeen Nabi ambaye nafasi yake ilichukuliwa na Muargentina Miguel Gamondi.
Ni kawaida timu zinapofika kilele cha mafanikio hujikuta katika hali ya wachezaji na hata maafisa wa benchi la ufundi kuwindwa na klabu nyingi zenye msuli wa fedha na kiu ya mafanikio.
Baada ya fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya, FC Porto ya Ureno dhidi ya Monaco ya Ufaransa mwaka 2004, klabu hizo zilipoteza nyota wake wakubwa na kwenye mabenchi ya Ufundi.
Chelsea ilimng'oa Kocha Jose Mourinho aliyeiongoza Porto kubeba taji kwa ushindi wa mabao 3-0 katika fainali hiyo, huku ikimbeba pia Didier Drogba kutoka Monaco.
Kwa Mayele, kuna waliokuwa wakitamani aondoke, hasa wapinzani kutokana na mchango wake kwa Yanga, huku wale wa Jangwani akiomba na kukesha abaki kutokana na umuhimu wake ingawa pande zote zinakubaliana juu ya nafasi yake kwenye kikosi cha Wanajangwani hao katika misimu yake miwili na ile stahili yake ya ushangiliaji ikiwa kama bonasi.
Soka ni mchezo unaoamuliwa na mabao na Mayele aliamua michezo mingi kwa mabao yake na kuibeba Yanga na unaweza kusema ni bahatoi au mkakati wa benchi la ufundi kwa jinsi alivyokuwa na mwendelezo na hakupata majeraha mabaya katika misimu miwili ya ligi akifunga mabao 33.
Unajiuliza kama Mayele angepata majeraha mabaya hasa mwanzoni mwa msimu kabla ya ujio wa Kennedy Musonda dirisha dogo, hali ya wananchi ingekuwaje? Unajiuliza kama yaliyomtokea Mzambia Moses Phiri Simba yangemtokea Mayele ubingwa ungekuwepo?
Hata hivyo, Yanga ilikuwa na kikosi kipana lakini mstari wa umaliziaji ulimtegemea Mayele kwa kiasi kikubwa.
Haishangazi kuona ilimchukulia Mayele kama mchezaji wa kipekee kwenye timu yao kwa sababu haikumjua mfungaji mwingine.
Hata ilipomleta mshambuliaji wao hatari wa zamani Heritier Makambo bado alionekana kama bunduki iliyopata kutu.
Hali hii ya kuwa na wigo mwembamba upande wa wamaliziaji sidhani hata kama kocha Nabi angelikuwepo angekubali kuingia msimu wa tatu na presha ya kumtegemea mshambuliaji mmoja, Mayele.
Lazima Yanga ingeingia sokoni kutafuta mshambuliaji namba tisa wa kiwango cha Mayele au vinginevyo ingetafuta mawinga au viungo wa ushambuliaji wenye kufikisha angalau mabao 10 kwa msimu.
Hadi sasa naamini Yanga ilikuwa kwenye presha tena kubwa sana ya kupata mchezaji au wachezaji wa kurithi majukumu ya Mayele. Kufunga mabao. Hakuna aliyetarajia mrithi wa kiatu cha dhahabu kuwa mchezaji aliyekuwepo kipindi cha Mayele. Kumbuka Feisal Salum aliyekuwa anafuatia alitimkia Azam FC.
Bila shaka Mayele alifaidika na mafanikio yake au tuseme juhudi zake Jangwani. Upande wa mfukoni, mambo yake yamefika mahali pazuri ambako wanasoka wengi wanapenda kufikia kama wachezaji wa kulipwa.
Baada ya Mayele kuondoka Yanga imejaribu kutafuta washambuliaji bila kupata mbadala sahihi wa Mayele. Hafiz Konkon kutoka Ghana alichemsha na hata mzawa Mzize hajafikia kiwango cha Mayele. Lakini walichokitaka Yanga ni mabao walikuja kuyapata kutokea kwenye kiungo kwa kina Maxi Nzengeli, Mudathir Yahya, Pacome Zouzoua na Aziz Ki mwenyewe.
Ni yaleyale ya Mayele yanayoweza kuwasumbua Yanga msimu huu linapokuja suala la Azizi Ki. Rais wao Injinia Hesi Said alisema hawatashindwa kumbakiza mchezaji yeyote wanayemtaka. Hata hivyo, ili la Azizi Ki limekaa vibaya.
Limekaa vibaya kwa sababu Aziz Ki amemaliza mkataba na hivyo akiamua kuondoka klabu haitapata kitu isipokuwa kubaki na kumbukumbu nzuri ya burudani aliyowapa uwanjani, makombe kabatini na pesa za ubingwa kwenye akaunti.
Abaki, aondoke Aziz Ki, Yanga itabaki kuwa Yanga. Bila shaka uongozi umejiandaa kwa yote mawili; maana kumbakiza nao ni mtihani tena mtihani wa hesabu. Mimi na wewe hatuwezi kujua malengo yake na menejimenti yake na wanataka nini kimpira na kifedha. Hata upande wa pili watani zao Simba wanajikuta katika hali hiyo.
Hakuna kiongozi anayetaka kuacha wachezaji wenye kuisaidia timu lakini hakuna kiongozi anayependa kuachia pesa za kuisaidia timu. Pamoja na vipaji vya ushawishi, viongozi watapima suti zao kuendana na ukubwa wa kitambaa. Hayo ni maisha ya kila siku ya klabu za mpira. Watu wanaingia wanatoka, maisha yanaendelea.