Timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ imepangwa katika kundi F la Fainali za Mataifa ya Afrika (Afcon) 2023 zitakazochezwa Ivory Coast kuanzia Januari 13 hadi Februari 11 ikiwa pamoja na timu za Morocco, DR Congo na Zambia.
Mechi za kundi hilo zitachezwa jijini San Pedro na timu mbili zitakazoongoza msimamo wake zitafuzu hatua ya 16 bora huku timu itakayoshika nafasi ya tatu itavizia nafasi moja kati ya nne za washindwa wenye matokeo bora (best losers) ili itinge hatua inayofuata.
Ni kundi ambalo sio jepesi kwa Taifa Stars kutokana na ubora wa vikosi ambavyo itaenda kupambana navyo katika fainali hizo ambazo hufanyika kila baada ya muda wa miaka miwili huku bingwa wake akipata zawadi ya kiasi cha Dola 5 milioni.
Ukiondoa ubora, Taifa Stars inakutana na timu zenye uzoefu mkubwa wa mashindano hayo ambapo kila moja kwa nyakati tofauti imewahi kutwaa ubingwa wa Afcon na zimekuwa na muendelezo wa kufanya vyema katika mashindano mbalimbali ambayo zimekuwa zikishiriki.Makala hii inakuletea dondoo za wapinzani hao watatu wa Taifa Stars kwenye fainali za Afcon mwakani ambao hapana shaka kazi ya ziada inapaswa kufanywa na timu hiyo ya Tanzania ili iweze kupenya na kuingia katika hatua ya 16.
Morocco
Ni miongoni mwa mataifa makubwa kisoka barani Afrika na kuthibitisha hilo, katika viwango vya ubora wa soka vya Shirikisho la Vyama vya Mpira wa Miguu Duniani (FIFA) vya mwezi uliopita, Morocco ilikuwa nafasi ya 13 kidunia na inashika nafasi ya kwanza Afrika.
Inanolewa na kocha mzawa Walid Regragui na nahodha Romain Saiss anayecheza soka la kulipwa huko Saudi Arabia katika timu ya Al-Shabab.
Morocco imefuzu fainali za Afcon 2023 baada ya kushika nafasi ya pili katika msimamo wa kundi K lililokua na timu za Afrika Kusini na Liberia, ikikusanya pointi 6 katika mechi tatu ilizocheza, ikishinda mbili na kupoteza mechi moja.
Mafanikio makubwa kisoka ya Morocco ni kutinga hatua ya nusu fainali ya Kombe la Dunia mwaka jana pindi mashindano hayo yalipofanyika Qatar lakini katika Afcon, imetwaa ubingwa mara moja ambayo ni mwaka 1976, ikimaliza katika nafasi ya pili mara moja mwaka 2004 na mwaka 1980 ilishika nafasi ya tatu lakini pia imetwaa ubingwa wa Fainali za Mataifa ya Afrika kwa wachezaji wanaocheza ligi za ndani (Chan) mara mbili ambazo ni 2018 na 2020.
Msingi mkubwa wa ubora wa Morocco ni nyota wake wanaocheza soka la kulipwa nje ya bara la Afrika hasa katika Ligi kubwa za Ulaya na Asia na mfano wa hao ni Achraf Hakimi (PSG), Sofyan Amrabat (Manchester United) na Nayef Aguerd (West Ham United).
Kwa mujibu wa mtandao wa transfermarkt unaojihusisha na utoaji tathmini ya thamani za wachezaji na timu, kikosi cha Morocco kinakadiriwa kuwa na thamani ya Euro 297.15 milioni na mchezaji ghali zaidi ni Hakimi mwenye thamani ya Euro 65 milioni.
DR Congo
Kwa mujibu wa mtandao wa transfermarkt kikosi cha DR Congo kinakadiriwa kuwa na thamani ya Euro 120. 25 milioni na mchezaji ghali zaidi ni nahodha Chancel Mbemba anayechezea Marseille ya Ufaransa mwenye thamani ya Euro 20 milioni.
DR Congo wamekuwa sio wanyonge katika Afcon kwani wamewahi kutwaa taji mara mbili ambazo ni 1968 na 1974, huku wakiwa wameshika nafasi ya pili mara mbili ambazo ni mwaka 1998 na 2015 huku wakiwa miongoni mwa mabingwa wa kihistoria wa mashindano ya Chan wakitwaa taji hilo mara mbili na waliwahi kushirki Kombe la Dunia mara moja ambayo ni 1974 walipoishia hatua ya makundi.
Katika viwango vya ubora wa soka vya Shirikisho la Vyama vya Mpira wa Miguu Duniani (FIFA) vya mwezi uliopita, Septemba ilikuwa nafasi ya 64 kidunia na inashika nafasi ya 12 Afrika.
Inanolewa na kocha raia wa Ufaransa, Sebastien Desabre ambaye aliwahi pia kuiongoza Uganda kufuzu fainali hizo za Afcon mwaka 2019.
DR Congo imefuzu fainali za Afcon 2023 baada ya kuongoza msimamo wa kundi K lililokua na timu za Mauritania, Gabon na Sudan, ikikusanya pointi 12 katika mechi sita ilizocheza, ikishinda nne na kupoteza mbili.
Wachezaji inaowategemea wanacheza katika Ligi kubwa za soka Ulaya mfano wakiwa ni Mbemba, Arthur Masuaku (Besiktas) na Yoane Wissa (Brentford).
Zambia
Zambia ‘Chipolopolo’ imefuzu fainali za Afcon 2023 baada ya kuongoza msimamo wa kundi H lililokua na timu za Ivory Coast, Comoro na Lesotho, ikikusanya pointi 13 katika mechi sita ilizocheza, ikishinda nne, kutoka sare moja na kupoteza moja.
Inanolewa na kocha raia wa Israel, Avram Grant na mastaa wake wanaongozwa na nahodha Lubambo Musonda anayeichezea Silkeborg ya Denmark.
Kwa mujibu wa mtandao wa transfermarkt, kikosi cha Zambia kinakadiriwa kuwa na thamani ya Euro 24.6 milioni milioni na mchezaji ghali zaidi ni Patson Daka wa Leicester City mwenye thamani ya Euro 18 milioni.
Chipolopolo imewahi kutwaa ubingwa wa Afcon mara moja ambayo ni mwaka 2012 huku katika miaka ya 1974 na 1994 ikimaliza katika nafasi ya pili na imechukua nafasi ya tatu mara tatu ambazo ni 1982, 1990 na 1996.
Katika viwango vya ubora wa soka vya FIFA vya mwezi Septemba ilikuwa nafasi ya 82 kidunia na inashika nafasi ya 17 Afrika.
Nyota tishio katika kikosi chao ni Daka, Kings Kangwa (Red Star Belgrade) na Fashion Sakala (Al-Fayhla).
Woga kando
Akizungumzia kundi walilopangwa, nyota wa Taifa Stars, Saimon Msuva alisema kuwa hawaihofii timu yoyote katika kundi hilo hasa Zambia na DR Congo ambazo wamewahi kucheza nazo mara nyingi.
“Wachezaji tayari tuna uzoefu na mashindano hayo na timu hizi mbili tunazijua tuliwahi kucheza nazo. Kikubwa ni sisi kwenda kupambana,” alisema Msuva.
Kiraka wa Taifa Stars, Novatus Dismas alisema wachezaji hawana woga na kundi hilo kwa sababu timu zote zilizofuzu ziko vizuri.
“Mpira umebadilika sana sasa hivi hakuna mambo ya majina makubwa.Sisi kama tegemeo la taifa hatutakaa kinyonge tutapambana,” alisema Novatus.
Kocha wa zamani wa Taifa Stars, Boniface Mkwasa alisema timu hiyo ina nafasi ya kuwashangaza wengi kwa kufanya vizuri Afcon.
“Ni ngumu kusema tunatoboa ila naamini tuna wachezaji wa viwango vikubwa wanaocheza Ulaya. Kikubwa maandalizi hakuna kinachotushinda,” alisema Mkwasa.