Nyota wote walioondoka kikosini Yanga kwa ajili ya fainali za Mataifa ya Afrika (Afcon) 2023 wamerejea na sasa maswali kwa kocha Muargentina Miguel Gamondi kwanini timu haichezi vyema tangu ligi iliporejea yanataka majibu.
Kurudi kwa nyota wote ni jambo lililokuwa likisubiriwa kwa hamu na mashabiki wa timu hiyo ya Wananchi, lakini jambo hilo lina maana kubwa katika ugali wa wachezaji kwani kuna wenye kupata na wenye kupoteza kuanzia kwa kocha Gamondi hadi wachezaji. Kuna wachezaji watapata namba zao na kuna wengine watapoteza namba. Na Gamondi mwenyewe atakuwa kitanzini.
Hebu twende sawa. Yanga inajiandaa na mechi ya kwanza ya mzunguko wa pili wa Ligi Kuu Bara dhidi ya KMC itakayopigwa keshokutwa, Jumamosi mjini Morogoro.
Kabla ya hapo,Yanga ilikuwa inakosa huduma ya mastaa wake kadhaa akiwamo Stephane Aziz Ki ambaye aliwahi kujiunga na timu na kucheza mchezo wa mwisho wa mzunguko wa kwanza dhidi ya Tanzania Prisons, na kipa namba moja Djigui Diarra ambaye ametua nchini na kuwahi mchezo wa kwanza mzunguko wa pili dhidi ya KMC.
Kukosa huduma ya mastaa waliokuwa kwenye Afcon kule Ivory Coast, kulichangia Yanga kupata matokeo kwa jasho jingi ikitoka 0-0 dhidi ya Kagera Sugar, kabla ya kushinda kwa taabu 1-0 dhidi ya Dodoma Jiji, 2-1 dhidi ya Mashujaa na 2-1 dhidi ya Tanzania Prisons, huku mara mbili ikihitaji mabao ya 'jiooni' dakika tano za mwisho kutoka kwa Mudathir Yahya ili kupata pointi tatu. Kiufupi mambo yamekuwa magumu. Hamna zile dozi za 5G huku wapinzani wakipigiwa mpira mwingi.
Mbaya zaidi, baada ya mechi dhidi ya Mtibwa, kituo kifuatacho ni mechi ya nyumbani ya Ligi ya Mabingwa dhidi ya CR Belouizdad. Ndio, wababe wale ambao waliichakaza Yanga kwa mabao 3-0 kule Algeria Novemba 24, 2023.
CR Belouizdad wanakuja kwa Mkapa. Kwa hiyo zimebaki siku chache sana kabla ya kuwavaa wababe hao ili kuamua hatima ya Yanga kwenye Kundi D la Ligi ya Mabingwa ambako Yanga iko nafasi ya pili kwa pointi 5, sawa na vinara Al Ahly, ambao kesho watacheza ugenini mechi yao ya kiporo dhidi ya Belouizdad.
Belouizdad wakipata japo sare nyumbani kesho, watakuja Dar wakiwa katika nafasi ya pili kwani watafikisha pointi tano lakini kutokana na tofauti nzuri ya mabao ya kufunga na kufungwa watakuwa tayari wameishusha Yanga hadi nafasi ya tatu katika msimamo. Hii itazidi ugumu wa mechi hii ya Kwa Mkapa.
Na hii itamweka katika wakati mgumu kocha Gamondi, ambaye kiuhalisia ameanza vizuri maisha ya Jangwani akitoa vipigo vikubwa vikubwa kwa wapinzani wake. Hiyo ni kwa kocha Gamondi, kuna shughuli pevu pia kwa wachezaji.
WATAPOTEZA NAMBA Kurudi kwa nahodha Bakari Mwamnyeto, Ibrahim Hamad 'Bacca', Aziz Ki na Diarra kuna baadhi ya wachezaji watarudi kwenye benchi hii ni kutokana na ubora wa wachezaji waliorudi na kuwa na nafasi ya kuaminiwa kikosini.
Licha ya kocha Miguel Gamondi kufanya mabadiliko ya kikosi kutokana na kubanwa na ratiba lakini tayari alikuwa ametengeneza kikosi chake cha kwanza ambacho kilikuwa kinampa matokeo japo yamekuwa yakipatikana kwa shida sana. Kurudi Kwa Diarra kutamuondoa Metacha Mnata na Aboutwaleeb Mshery ambao wamecheza mechi nne za ligi na moja Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC).
Diarra akidaka mechi 11 kati ya 15 za mzunguko wa kwanza hivyo ni wazi kuwa ndiye kipa namba moja hivyo ataachiwa nafasi yake.
Wakati Diarra akiwaondoa makipa hao huku mmoja Metacha akiwa na kadi nyekundu pia kutakuwa na mabadiliko eneo la kiungo cha ushambuliaji ambalo lilihodhiwa na Aziz Ki kabla ya kwenda kwenye Afcon. Kutokuwepo kwake kulimfanya Farid Mussa arejee kikosini, akicheza eneo la winga sambamba na Maxi Nzengeli.
Beki Gift Fredy ambaye alikuwa anajitafuta amepata nafasi ya kucheza chini ya Gamondi akianzia Mapinduzi na sasa Ligi Kuu na kwenye eneo la ulinzi analocheza ameonyesha ubora hivyo ataleta mtihani kwa kocha kuendelea kumuamini au kuwarudisha Mwamnyeto na Bacca.
GAMONDI AFUNGUKA Kocha mkuu wa Yanga, Gamondi alisema anatambua umuhimu wa michezo yote miwili iliyo mbele yao na anapambana kuwarudisha wachezaji wake kwenye ubora wao lengo ni kuona wanafanya vizuri bila kujali ni mashindano gani.
"Kilio cha mashabiki kuwahitaji wachezaji wao kimeisha kwasababu nyota wote wamerejea kikosini na kila mmoja ana umuhimu wake, maandalizi yanakwenda vizuri sisi kama benchi la ufundi tunaendelea kufanya kila linalowezekana kwa kuhakikisha tunatetea taji na tunatinga hatua inayofuata.
"Diarra kurudi kwake kumeongeza nguvu kwasababu ni mchezaji mwenye uzoefu na amekuwa akifanya kazi yake kwa usahihi kwa kuanza na kuanzisha mashambulizi ukiachana na juhudi zake kwenye kulinda goli," alisema.
Akizungumzia nafasi yake kwenye mchezo dhidi ya KMC, alisema itategemea na namna atakavyofanya vizuri kwenye uwanja wa mazoezi huku akikiri kuwa kurejea kwake kumeongeza nguvu kutokana na ratiba waliyonayo.
"Tuna mechi ya ligi Jumamosi tayari Metacha hatutakuwa naye kutokana na kadi nyekundu hivyo kurudi kwa Diarra tayari tuna makipa wawili wazoefu mmoja ataanza na mwingine atasubiri benchi.
"Ukiachana na ligi pia tuna mchezo wa kimataifa ambao ni muhimu sana kwetu kujihakikishia nafasi ya kutinga hatua ya robo fainali hivyo kukamilika kwetu ni chachu ya kujiandaa kwa upana na kutoa mwanya kwa wachezaji wote muhimu kufungua miili yao kabla ya mechi yetu ya kimataifa ugenini," alisema.
MECHI ZA YANGA
KMC vs Yanga Februari 17
Yanga vs CR Belouizdad Februari 24