Siku chache kabla ya kifo chake hadi sasa kunasambaa video inayotambulishwa kwa jina la “Pele Did It First” ikionyesha ustadi tofauti ambao mashabiki wa soka wameshuhudia kutoka kwa Diego Maradona hadi sasa kwa Neymar Junior.
Ni stadi za kupokea mipira, kumtoka mlinzi, kufunga na ujanja mwingi wa kumhadaa adui. Kila stadi ya mchezaji mmoja wa kizazi hiki inapoonyeshwa, baadaye huja ya Pele ambayo kutokana na teknolojia ya wakati huo picha zake zimefifia.
Lakini kama kuna mtu anapiga rainbow flick, basi Pele alishafanya hivyo zamani na kama atapiga chenga ya kuruka mpira, basi nyota huyo wa zamani wa Brazil alishafanya enzi hizo akisakata soka kuanzia miaka ya hamsini hadi sabini alipostaafu.
Edson Arante Descimento Pele aliitawala dunia kutokana na uwezo wake. Alifunga mabao, aliburudisha watazamaji na alitwaa mataji akiwa na klabu yake ya Santos na taifa lake la Brazil. Na akahitimisha ufalme wake kwa kutwaa Kombe la Dunia mara tatu, rekodi ambayo inaweza kuchukua karne nyingine kuvunjwa.
Lakini gwiji huyu alifanya haya yote kutokea kwao Brazil, barani Amerika Kusini tofauti na nyota wengine wa sasa ambao hawawezi kung’aa hadi wahamie barani Ulaya.
Si Ronaldo de Lima, wala si Alfredo Di Stefano, wala Diego Maradona, wala George Weah, wala Ali Daei, wala Samuel Eto’o, wala Mohamed Salah au Sadio Mane. Wote walilazimika kwenda barani Ulaya kutangaza ufalme wao ambao hata hivyo haujagusa chembe ya alichokifanya Pele.
Wanachoweza kufanya wafalme wa sasa ni kufikia rekodi zake za kufunga mabao na hii inawezekana kwa sababu michuano sasa imekuwa mingi kiasi kwamba imekuwa rahisi kwa Cristiano Ronaldo na Lionel Messi kujivunjia rekodi za mabao watakavyo.
Lakini wanachoshindwa ni kutwaa mataji makubwa, hasa Kombe la Dunia zaidi ya mara moja, labda tu Shirikisho la Kimataifa la Soka litakapobananisha fainali hizo ili zifanyike kila baada ya miaka miwili. Bila hivyo, hakuna ambaye atamfikia Pele.
Nimeanzia mbali kutaka kujenga hoja yangu hapo katika kuu-tawala ulimwengu wa soka kutokea Brazil. Sioni, katika hali ya sasa, m-chezaji nyota kutoka Amerika Kusini, Kaskazini, Asia, Afrika au Oceania ambaye ataweza kutikisa dunia bila ya kwenda barani Ulaya.
Ni kweli kwamba misuli ya kifedha ya klabu za Ulaya inasababisha wawe na macho yanayoona mbali na kuweza kuchukua vipaji wakati vijana wakiwa bado wadogo sana, kama Barcelona walivyofanya kwa Messi, au Real Madrid walivyofanya kwa Vinicius na hivi sasa wakihangaika na Endrick, ambaye wameshaingia naye makubaliano lakini atajiunga nao baada ya kufikia umri wa miaka 18.
Lakini ni kitu gani kinazuia mabara mengine kubakia na nyota wake. Jibu rahisi ni ukosefu wa fedha. Lakini swali gumu zaidi ni “kwa nini ukosefu wa fedha?”
Kocha wa zamani wa Real Madrid, Jose Mourinho amekuwa akiamini kuwa kama Afrika itaenda fainali za Kombe la Dunia na nyota wake bila kupokwa na mataifa ya Ulaya, uwezekano wa kutwaa Kombe la Dunia ni mkubwa.
Na anaweza kuunganisha mambo mengi kuongeza nguvu kwenye hoja yake. Fainali ya mwaka huu ya Kombe la Dunia ilikutanisha Argentina na Ufaransa, ambayo ilijaa wachezaji wenye asili ya Afrika wakiongozwa na Kylian Mba-ppe, ambaye anatokea Cameroon.
Ni wachezaji wangapi wenye asili ya Cameroon walichezea mataifa tofauti kwenye fainali za mwaka huu. Achilia mbali Cameroon, vipi kuhusu Ghana, Nigeria, Senegal na hata Sudan ya Kusini. Ni wengi.
Vipi kuhusu wale wenye asili ya Amerika Kusini. Ni wengi pia kutokana na nchi za barani Ulaya kuweka sheria inayoruhusu uraia pacha na hivyo kuwa rahisi kwa wachezaji kutoka nje ya bara hilo, hasa Amerika Kusini kupewa uraia wa mataifa ya Ulaya, hasa Hispania, Ujerumani, Ufaransa, Uswisi, Ubelgiji na England.
Lakini hoja hapo si kuonyesha kwamba Afrika inaweza kutwaa Kombe la Dunia kwa kutumia nyota wake wote, wakiwemo hao waliochukua uraia wa mataifa ya Ulaya, la hasha. Bali kuonyesha Afrika ina vipaji ambavyo vinakosa mazingira mazuri ya kuibukia ndani ya mataifa yao.
Hoja kubwa zaidi inajengwa na mshambuliaji wa zamani wa AC Milan, Mario Balotelli ambaye anaona kuwa Afrika ikiimarisha miundombinu yake ya soka, basi inaweza kutawala soka. Balotelli, ambaye huamini hakuna mchezaji nyota kumzidi yeye, anasema kama Afrika itajenga viwanja vizuri na kuweka mazingira mazuri ya uwekezaji, ligi za nchi zitakuwa bora na hata ile michuano ya klabu ya Afrika itakuwa bora zaidi na hivyo hakutakuwa na sababu ya nyota wetu kukimbilia Ulaya. Watabakia hapa Afrika kama Pele alivyobakia Brazil hadi alipokaribia kustaafu alipoitwa kwenda Marekani kuichezea New York Cosmos.
Na ndoto ya Balotelli itatimizwa, maana yake itafikia wakati hata mashabiki wa soka wa barani Ulaya watataka wawaone nyota wa Afrika kama ilivyokuwa kwa Pele. Kuna wanaosema Pele hakustahili taji hilo la ufalmne kwa sababu hakujaribiwa barani Ulaya, lakini hoja hiyo inakosa nguvu pale linapoingizwa suala la fainali za Kombe la Dunia ambako Brazil ya Pele ilikutana na nyota kutoka kila kona ya dunia.
Kutokana na ufalme wake, Santos ilialikwa sehemu kadhaa duniani kwenda kucheza mechi za kirafiki. Na ingawa mechi za kujiandaa kwa msimu hujumuisha wachezaji vijana na wageni, mechi dhidi ya Santos ya Pele hakuna klabu ya Ulaya iliyochezesha kikosi dhaifu.
Mechi kati ya Santos na Inter Mil;an iliingiza watu 100,000 na Pele akaibuka shujaa baada ya timu yake kushinda kwa mabao 4-1, huku mashabiki zaidi ya 10 wakijeruhiwa katika jitihada za angalau kumuona nyota huyo kwa mbali.
Bado nabakia kwenye hoja ya Balotelli kwamba Pele aliona hayo yote kwa sababu aliamini kwa wakati ule “hakukuwa na haja ya wachezaji wazuri kuhamia barani Ulaya” baada ya kuulizwa kuhusu madau ya Real Madrid na Inter Milan kumtaka gwiji huyo.
Mazingira hayo yaliyosababisha Pele asione umuhimu wa kukimbilia barani Ulaya, ndiyo ambayo Afrika inatakiwa iyatengeneze. Yaani ‘George Weah’ atwae Balon d’Or, akiwa anaichezea klabu ya Monrovia Breweries badala ya AC Milan.
Yaani wakala wa Kelvin-Prince Boateng awe anafanya kila jitihada kufanikisha usajili wa nyota huyo kuchezea Asante Kotoko, na si viongozi wa soka wa Ghana kufunga safari hadi Ujerumani kwenda kumshawishi achezee taifa hilo baada ya kufuzu fainali za Kombe la Dunia.
Pele ameacha changamoto hiyo kwa mabara mengine ambayo yanazalisha nyota wengi, lakini hawatoi burudani kwa nchi zao na ufalme wao hauonekani hadi wakimbilie Ulaya.
Afrika inahitaji kuboresha michuano yake ili ivutie kibiashara na kuziwezesha klabu kuimarika kifedha na kuanza kushindana na mataifa ya Ulaya katika kununua wachezaji na hatimaye ligi za nchi kuvutia dunia nzima. Kama alivyosema Pele, kufikia hatua hiyo hakutakuwa na “haja kwa wachezaji nyota kukimbilia Ulaya”.