Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kuna shida Chelsea, Thiago Silva afichua mazito

Thiago Silva Chelsea Kuna shida Chelsea, Thiago Silva afichua mazito

Fri, 23 Aug 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Chelesea kuna shida na kwa sasa mambo hayajatulia kwenye kutengeneza kikosi huku Kocha Enzo Maresca akiendelea na mazoezi na anachotaka ni wachezaji 24 tu wa kuwafundisha, huku wengine wakipishana kwenye viwanja vingine vya mazoezi vya klabu hiyo tajiri ya London.

Inaelezwa tatiizo ni wingi wa wachezaji na imeleta usumbufu kwa baadhi ya wachezaji na inaelezwa wengine wamekuwa hawana furaha, pia wanalazimika kutumia viwanja tofauti vya mazoezi.

Nyota wa zamani wa klabu hiyo, beki Thiago Silva aliyeondoka msimu uliopita, aliwahi kusema wingi wa wachezaji walioko Chelsea ni moja ya mambo yaliyochangia kufanya vibaya msimu uliopita na hata nje ya uwanja wachezaji hawakuwa na furaha na wengine walipokonywa makabati ya nguo baada ya wengine kutua kwani hayakutosha.

"Baada ya mabadiliko ya umiliki, wachezaji wengi waliingia. Ilibidi hata kuongeza ukubwa wa chumba cha kubadilishia nguo kwani hakikuwa kinatosha kwa wachezaji wote, wachezaji walikuwa wanaudhika na kujisikia vibaya kwa sababu si kila mtu anaweza kucheza. Kocha anaweza kuchagua wachezaji 11 pekee lakini unakuta tupo 30."

Hata hivyo, kutokana na wingi huo, inaelezwa baadhi wameanza kupewa 'thank you' na wameambiwa waanze kutafuta timu watakazozichezea, huku wengine wakitakiwa kufanya mazoezi kwa makundi ili kumpa urahisi kocha Maresca kuwapa mbinu zake.

Wachezaji walioambiwa hawatakuwepo kwenye mpango wa Maresca msimu huu ni Raheem Sterling, Ben Chilwell, Romelu Lukaku, Kepa Arrizabalaga na Trevoh Chalobah na hawatoweza kufanya mazoezi na kikosi cha kwanza kwenye Uwanja wa Cobham na wanne kati yao waliigharimu Chelsea Pauni 270 milioni kama ada ya usajili, huku Chalobah akiwa ni zao la Akademi yao.

Nyota Conor Gallagher ilikuwa hivyo hivyo kwake na sasa ametua Atletico Madrid, huku Armando Broja yupo mbioni kutua Ipswich Town kwa mkopo wa msimu mmoja.

Timu kibao zimeonyesha nia ya kutaka kumsajili Sterling wakati Chelsea inafanikisha dili la Pedro Neto kutoka Wolves kwa Pauni 54 milioni na akiwa nyumbani kwake na alipewa jezi yenye namba yake (7).

Kwa mujibu wa tovuti ya Daily Mail, orodha ya watakaoachwa ni ndefu na inafikia 13 na wapo watakaotolewa kwa mkopo na kwa sasa wanafanya mazoezi chini ya kocha Carlo Cudicini ambaye ni maalum kwa kuwafundisha wachezaji wanaotarajiwa kutolewa kwa mkopo.

Mastaa hao wengine ni pamoja na David Datro Fofana, Angelo, Lucas Bergstrom, Deivid Washington, Tino Anjorin, Alex Matos, Harvey Vale na Broja na wapo kwenye mseto wa wale wenye uzoefu, vijana, wenye umri mkubwa na wale wasiokuwa na uzoefu pia.

Beki wa zamani wa Manchester United, Rio Ferdinand alidai mastaa hao wamekuwa wakikuta barua za kuambiwa watafute timu kupitia email zao, hata hivyo, kocha Maresca amesisitiza wachezaji wote walioambiwa watafute timu aliongea nao ana kwa ana.

Kwa mujibu wa tovuti ya Mail ambayo mwandishi wao alikuwa katika viwanja vya Cobham kushuhudia mazoezi ya matajiri hao wa Jiji la London, Jumatano ya wiki hii, iliripoti kulikuwa na wachezaji 24 waliokuwa wanafanya mazoezi na 20 kati yao ni wa ndani kisha wanne ni makipa Robert Sanchez, Djordje Petrovic, Filip Jorgensen na Marcus Bettinelli wakiwa wanajiandaa kukutana na Servette kutoka Uswiss katika michuano ya Europa Conference League, mchezo uliopigwa jana usiku.

Wachezaji hao walikuwa wakifanya mazoezi katika eneo lililokuwa na miti mirefu kiasi ambacho hata wenzao waliotengwa kama wakiamua kuwatazama basi wasingewaona.

Moja ya mambo ya kusikitisha kwa wachezaji walioambiwa hawaruhusiwi kufanya mazoezi na timu ni hawajapewa eneo maalumu la kufanyia mazoezi, hivyo kama wakiona uwanja wa timu ya wanawake upo huru hufanyia huko ama muda mwingine hufanyia katika viwanja vya Akademi.

Vile vile wanaruhusiwa kutumia maeneo mbalimbali vilivyopo ndani ya jengo la Cobham ikiwamo mabwawa ya kuogelea, Gym na vifaa vingine vya mazoezi.

Baadhi ya mashabiki wamekuwa wakichukizwa sana na hali ya mastaa kutengwa hususan kwa Chalobah na Conor Gallagher ambaye ameshauzwa.

Chanzo: Mwanaspoti