Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kuna namna tunamkosea heshima Saido Ntibazonkiza

Saidooooo Saido Ntibanzokiza

Mon, 28 Feb 2022 Chanzo: Mwanaspoti

Saido Ntibazonkiza. Mtangazaji wa Azam TV, Baraka Mpenja hupenda kumuita ‘Godfather wa Bujumbura’. Ni mchezaji kweli kweli.

Jumatano iliyopita aliibeba Yanga katika mabega yake pale Manungu. Akaiamua mechi kupitia miguu yake. Akaifanya Mtibwa Sugar kile anachojisikia.

Saido alifunga goli la kwanza na kutoa pasi ya goli la pili Yanga ikinawiri pake katikati ya mashamba ya miwa. Ni sehemu ngumu kucheza. Tuliona kilichomkuta Simba pale.

Yanga ilikuwa ikirejea Manungu baada ya miaka Zaidi ya 20. Mtibwa Sugar huwa wanapaita Machinjioni lakini Saido alipageuza kuwa sebuleni kwake. Mechi ikawa nyepesi kwa Yanga.

Wengi tunaweza kumzungumza Saido baada ya mechi hiyo pale Manungu. Lakini ukweli ni kwamba tangu Saido amerejea katika kikosi cha kwanza cha Yanga hakuna mchezaji aliyefanya vizuri Zaidi yake. Labda Fiston Mayele tu.

Saido amekuwa na wastani mzuri wa magoli ya kufunga. Ndio mchezaji anayeamua Yanga ishambulie vipi. Ule ushawishi aliokuwa nao Feisal Salum mwanzoni mwa msimu sasa umehamia kwa Saido.

Anaisukuma timu mbele kwa kasi ya ajabu. Anatengeneza nafasi kwa wachezaji wenzake. Anakaa kwenye nafasi na kuifanya Yanga kuwa na utulivu wa kutosha katika eneo la kushambulia. Halafu ana utulivu mkubwa ndani ya eneo la hatari.

Kuanzia mwishoni mwa Novemba Saido amefunga magoli matano na kutoa pasi moja ya goli kwenye Ligi Kuu. Katika kipindi hicho Feisal amefunga goli moja tu na pasi moja ya goli.

Hii ndiyo sababu nasema kuna namna tunamkosea heshima Saido. Kwa sasa pale Yanga amekuwa na mchango mkubwa sana. Ni tofauti na anavyozungumzwa.

Chanzo: Mwanaspoti