Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kuna namna Yanga inaendeshwa kisela

Yanga Haire N Kuna namna Yanga inaendeshwa kisela

Mon, 6 Feb 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Hii nchi huwa haiishi vituko. Kila siku tunaamka na vituko vipya na kulala na vingine. Inachekesha sana.

Ndio kama kilichotokea wiki hii pale Yanga. Ni mambo ya ajabu sana. Ni kituko kutokea katika nyakati hizi.

Yanga ikiwa katika udhamini na Sportpesa imetangaza udhamini mpya. Madai yao ni kwamba ni udhamini kwa ajili ya mashindano ya CAF. Inashangaza sana.

Ni wazi kuwa Sportpesa haiwezi kukaa kifuani kwenye jezi za Yanga katika mechi za kuanzia hatua ya makundi CAF.

Hii ni kutokana na pia CAF kuwa na udhamini wa kampuni ya kubeti. Lakini hii haiondoi ukweli kuwa bado Sportpesa ni mdhamini wao mkuu. Ndio waliopaswa kuwapa ruhusa Yanga kufanya jambo lolote.

Hata hivyo, kwa mujibu wa SportPesa ni kwamba hawakushirikishwa. Inashangaza sana.

Yanga ikafanya sherehe ya kutangaza mdhamini mpya. Inazindua jezi mpya na kuweka chapa ya mdhamini mpya.

Hizi ndizo jezi zinazotembea zaidi huko mtaani. Tayari Yanga imeuza maelfu ya jezi hizo ambazo mdhamini wao mkuu Sportpesa hajawekwa popote. Inaelezwa siku ya kwanza tu jezi zote zilizokuwa sokoni ziliisha licha ya bei yake kuwa Sh50,000. Zile zenye nembo ya SportPesa zinapigwa kwa Sh35,000. Kuna tofauti ya Sh15,000 baina ya jezi hizo mbili za Yanga.

Ndizo jezi zinazovaliwa zaidi hivi sasa lakini zinatangaza mdhamini mwingine wakati mdhamini wao mkuu yupo.

Ingewezekana Yanga kuweka mdhamini mpya kifuani katika jezi zao za mechi za CAF, lakini vipi kuhusu zile zinazouzwa kwa mashabiki?

Je, CAF inakataza jezi hizi za mashabiki kuwa na nembo ya Sportpesa? Hapana. Hapa Yanga imepeleka mambo yao kisela sana.

Inamuumiza mdhamini yeyote kuona jezi za timu aliyodhamini zinauzwa mtaani bila nembo yake. Katika jezi hizi za mashabiki Yanga ingeweza kuwaweka Sportpesa popote pale. Ingekuwa ni jambo la busara na kutia tija.

Lakini kwa kuwa pale Yanga mambo yanakwenda kisela hawakuweza kufanya hivyo. Wamefanya jambo kwa mhemko na kukurupuka.

Waliwezaje kutengeneza jezi mpya za CAF, wakazisafirisha hadi nchini bila kukubaliana na Sportpesa? Ni wazi kuwa Yanga na huyu mdhamini mpya walikubaliana naye siku nyingi zilizopita. Wakawa wanazuga tu na Sportpesa lakini tayari walikuwa na uamuzi wao.

Mchakato wa kuagiza jezi, kuzichapa na kuzileta nchini unachukua si chini ya wiki nne hadi sita. Ni wazi kuwa hadi Yanga wanaagiza jezi hawakuwa na muafaka wowote na Sportpesa.

Ndio matokeo tuliyoshuhudia ya mikwaruzano ya wadhamini wao wakuu. Ni kama vile Yanga imechukulia mikataba yao kiwepesi sana. Haijajali na wala kuheshimu.

Sijui tatizo lipo wapi, kwani hata kwenye sakata la Bernard Morrison, Wanayanga waliaminishwa kila kitu kitakuwa poa, lakini mwishowe waliangushwa na Mghana huyo mjanja. Hata ukifuatilia sakata la Feisal Salum ‘Fei Toto’ utabaini kitu. Lakini kwa hili la SportPesa linavunja nguvu na moyo kama kweli kuna vitu vimekiukwa.

Hili sio jambo zuri kwa wadhamini tunaowahitaji katika soka letu.

Huwezi kumpa nafasi mdhamini mpya kwa kugombana na aliyepo. Hii inawavunja moyo wale wanaopenda kuwekeza katika soka.

Pengine huu ni ugeni katika mashindano, lakini tulifikiri kwa uwepo wa mtendaji mkuu wa kimataifa mambo yangekuwa tofauti, lakini ukweli ni kwamba Yanga bado ni ileile.

Yawezekana idara ya sheria pale Yanga ina shida, lakini tusiwalaumu moja kwa moja kwani wanaweza kuwa wanafanya kazi kwa maelekezo zaidi.

Kwa maana ya kwamba mfumo wa utendaji upo lakini watendaji wenyewe hawana uhuru na kazi zao kwani wanapaswa zaidi kufanya kwa kumfurahisha mtu fulani.

Wakati fulani mwaka juzi Simba ilipata udhamini kwa ajili ya mashindano ya CAF. Wakazungumza na Sporpesa juu ya hilo, lakini wakawagomea. Simba wakaamua kuweka ‘Visit Tanzania’ ili wasigombane na mdhamini wao. Ndio busara ya kuishi na wadhamini.

Simba inafahamu nguvu ya mikataba. Inaheshimu mikataba ya wadhamini. Haishangazi kuona kila siku inapata wadhamini wapya.

Lakini kwa kuwa pale Yanga mambo yanakwenda watakavyo hawawezi kuona hilo. Hebu fikiria Januari Yanga ilitangaza kuanzishwa kwa chaneli ya Yanga TV ndani ya kisimbuzi cha Azam. Ikatangaza jambo hilo usiku mkali. Watu wakatoka na kuwapongeza kwa hatua hiyo kubwa.

Lakini wengine wakahoji kama ni kweli Yanga inaanzisha chaneli yake kwanini hili jambo litangazwe usiku? Kwanini Yanga itangaze yenyewe? Ni maswali magumu.

Nini kimetokea baada ya hapo? Hakuna chaneli imeanzishwa hadi leo. Hakuna neno lolote kutoka Azam TV. Hakuna chochote. Ni mambo ya kisela tu.

Ndio kama hili la kuachana na Gael Bigirimana. Yanga imemtoa kwenye usajili kinyemela na kumuingiza mchezaji mwingine wa kigeni.

Nimeona barua kutoka Shirikisho la Soka Burundi likitaka TFF iwape uhakika kama Bigirimana ameondolewa katika usajili.

Wanataka kwenda kushtaki Fifa ili mchezaji alipwe fidia. Hii ndio hasara ya kuendesha mambo katika timu kisela.

Chanzo: Mwanaspoti