Nilitamani sana kuwa sehemu ya tamasha la mbio za Jeshi la Kujenga Taifa (JKT Marathon), zilizofanyika wikiendi iliyopita.
Kama mhitimu na muumini mzuri wa jeshi hilo nilitamani mno kuwepo. Zaidi lilikuwa linafanyika Dodoma ambako mimi pia nilifanyia mafunzo yangu kwa mujibu wa sheria miaka 30 iliyopita.
Pamoja na kutoshiriki moja kwa moja, bado nilifuatilia kwa karibu sana kilichokuwa kinaendelea Dodoma.
Nilijikuta navutiwa sana na hotuba ya mgeni rasmi, Rais Mstaafu, Jakaya Mrisho Kikwete.
Katika hotuba yake, JK alielezea kilio chake kitabaki kuwa uendelezaji wa vipaji. Alitoa masikitiko yake anapoona wachezaji wa kigeni wakifanya vizuri na kutawala ligi yetu, huku wazawa na timu ya taifa letu ikiwa na mgao au sehemu ndogo ya mafanikio hayo.
Mheshimiwa Kikwete alielezea kusikitishwa na kiu ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) na baadhi ya klabu za Ligi Kuu katika kutaka kusajili wachezaji wa kigeni kiasi cha kufikia ruksa ya wachezaji 12 kwa msimu mmoja.
Nilihisi JK anajisikia vibaya sawa na mzazi aliyeitwa kwenye mkutano shuleni kwa mtoto wake, halafu anashuhudia zawadi za wanafunzi bora zinatolewa, huku mtoto wake anakosa kutajwa si tu kwenye mafanikio ya kitaaluma bali hata mafanikio binafsi kama usafi, nidhamu, michezo n.k.
Katika mazingira haya, mzazi anaweza kufikiria mengi ikiwemo kutamani ukubwa au wingi wa wanafunzi katika darasa ungepunguzwa ili mtoto wake aweze kufanya vizuri.
Mzazi anaweza hata kutamani kijana wake ahame shule au wanafunzi wanaochukua zawadi nyingi wahame shule ili angalau naye ajisikie fahari ya mwanaye kutajwa katika wanaofanya vizuri. Sio JK peke yake, Watanzania wengi wanajisikia vibaya.
Wanajisikia vibaya pale wanapogundua kwamba furaha za kufanya vizuri kwa Yanga na Simba hazitafsiriki katika viwango vya soka letu, hasa timu za taifa.
Wanasikitika sana wanapogundua kwamba hata TFF inajivunia mafanikio ya klabu kupitia wachezaji wa kigeni kiasi cha kufungulia milango wachezaji 12 kwa kila klabu.
Watanzania wanajisikia vibaya zaidi wanapoona juhudi ndogo za uendelezaji wa vipaji kuanzia mchangani, shuleni, klabu na TFF.
Ligi Kuu Bara inasemekana kuwa katika nafasi tano hadi 10 za juu katika ubora barani Afrika. Hii imetokana na kazi nzuri ya Bodi ya Ligi (TPLB) na klabu za Ligi Kuu.
Ndiyo klabu zilichangia pa kubwa katika uanzishwaji wa Bodi ya Ligi na vinatumika sana kuikuza na kuitangaza Ligi ya Bara. Wakati kwenye klabu kunanoga, lakini timu ya taifa iko hoi bin taabani; nafasi ya 130 duniani kwa viwango vya Fifa. Angalia Timu ya Taifa ya DR Congo tunakochukua wachezaji wa bei mbaya kwa viwango vya hapa kwetu, lakini wa bei rahisi kulinganisha na Wakongoman wanaocheza Ulaya, Afrika ya Kaskazini na Afrika Kusini. DR Congo iko nafasi ya 70 duniani katika viwango vya Fifa kwa timu za wanaume.
Huko nyuma, TFF ilikuja na mpango wa miaka 10 ya maendeleo ya soka la vijana kwa kuanza kutafuta vijana kutoka Umitashumita (Mashindano ya Shule za Msingi), kisha kuwatafutia vituo na Shule za Sekondari kwa ajili ya kuwakuza na kutengeneza timu za vijana za taifa na timu za Olimpiki.
Lengo na matamanio ilikuwa kuiona Tanzania ikicheza Kombe la Dunia 2026. Mavuno ya kwanza yalikuwa 2017 ambako timu ya vijana chini ya miaka 17 ilikuwa miongoni mwa timu nane zilizocheza Afcon U17, Gabon.
Baada ya timu hiyo kushindwa kutinga fainali za dunia za vijana matumaini yalibaki kwenye Afcon U 17 ya Mwaka 2019 iliyofanyika hapa nchini.
Bahati mbaya timu yetu (Serengeti Boys) ilifanya vibaya na kushindwa kutumia fursa ya uenyeji. Hakuna ajuaye tungekuwa wapi kama tungefuata mkondo wa 2017. Angalia vijana kama Ramadhan Kabwili, Kibwana Shomary, Dickosn Job, Israel Mwenda, Yohana Mkomola, Kelvin Nashoni na wengine wanatoka Serengeti Boys na kuingia kwenye vikosi vya kwanza vya timu za Ligi Kuu na sasa wanaunda sehemu kubwa ya timu ya taifa ya wakubwa, Taifa Stars.
Timu hiyo ilikuwa ni mfano na ilijengwa kwa juhudi zote na shirikisho bila kusahau mchango wa klabu kama Mtibwa Sugar, Azam FC na Alliance.
Hiyo imebaki ni historia. Shirikisho lina nafasi kupitia leseni za klabu kuhakikisha juhudi za kuboresha mpira wa vijana zinakuwa kubwa sambamba na uboreshaji wa ligi.
Nafasi ya Tanzania katika mpira wa dunia ni ya chini pamoja na ukweli kwamba tuko miongoni mwa nafasi za juu duniani katika mapenzi ya soka.
Hali halisi inaonyesha kuwa hatujawekeza vya kutosha au kujipanga vizuri katika kuzalisha kile tunachokipenda. Tunakula tusichokizalisha.
Tumekuwa kama jamii ambayo maisha yake yote inategemea chakula cha kuemea ili iweze kujitosheleza. Jamii ya namna hii ina machaguo mawili;chaguo la kwanza ni kuamua kupunguza au kuacha kula chakula cha kuemea huku ikitegemea siku moja itazalisha cha kwake na chaguo la pili ni kuamua kuemea chakula huku ikiweka juhudi kuzalisha kwa kujitosheleza na hata kuuzia wengine.
Kwa bahati mbaya Tanzania inaonekana kutokuwa na uamuzi mmojawapo katika machaguo yaliyotajwa hapo juu.Zimekosekana sera zenye nguvu ya kuendeleza michezo kutoka ngazi za chini na hili haliko kwenye mpira wa miguu peke yake.
Kama kuna wakati TFF limewekewa mazingira ya kufanya kazi kwa uhuru na ushirikiano mkubwa na serikali wakati huo ni sasa. Hata hivyo, juhudi kwenye kukuza vipaji hazionekani kutumia fursa hii ambayo si vyama vingi duniani vinaipata.
Kwenye klabu za soka, akademia, mtaani na mashuleni kuna fursa kubwa ya kufanikisha uibuaji na ukuzaji wa vipaji. TFF na wizara wakiweka sera za vijana na kusimamia utekelezaji wake, maumivu ya JK na watanzania wote yataondoka. Inawezekana.
Nionavyo mimi kuzuia au kupunguza wachezaji wa kigeni sio dawa mwafaka ya kukuza soka letu. Uwepo wa wachezaji wazuri wa kigeni waliopata leseni za kufanya kazi hapa kutokana na ubora wao kunaweza kuchochea mapenzi na vipaji vya vijana wetu. Kuacha kuemea nje hakuwezi kuondoa njaa kama hakuna juhudi za kuzalisha chakula nyumbani.
NB: Mwandishi wa makala hii ni Katibu Mkuu Mstaafu wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF). Unaweza kumtumia maoni yako kupitia simu yake hapo juu.