Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kumekucha ASFC, Simba, Yanga kizungumzkuti

Aziz Che Malone Nstagram Kumekucha ASFC, Simba, Yanga kizungumzkuti

Thu, 14 Dec 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Pazia la michuano ya Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC) hatua ya 64 Bora linafunguliwa leo kwa mechi tano tofauti, huku vigogo Simba na Yanga zikiwa kwenye utata wa kucheza mechi ndani ya mwaka huu kutokana na kubanwa na ratiba ya viporo vya mechi za Ligi Kuu na ile ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Ratiba inaonyesha Cosmopolitan itakuwa wenyeji wa Rhino Rangers kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam, huku Dodoma Jiji ikikwaruzana na Magereza Dar kwenye Uwanja wa Jamhuri, Dodoma na Ihefu itaialika Rospa FC ya Mtwara kwenye Uwanja wa Highland Estate mkoani Mbeya.

Mechi nyingine za leo JKT Tanzania itakuwa mwenyeji wa Kurugenzi ya Simiyu kwenye Uwanja wa Azam Complex, ilihali Wagosi wa Kaya, Coastal Union ya Tanga itavaana na Greenland FC ya Kagera kwenye Uwanja wa Mkwakwani, jijini Tanga.

Mechi hizo zitachezwa kwa dakika 90 na ikishindikana kupatikana kwa mshindi,zitapigiana penalti ya atakayeibuka kidedea atasonga mbele kutinga hatua ya 32 Bora, huku vigogo Simba, Yanga, Mtibwa Sugar na Kagera wenye mechi za viporo vya Ligi Kuu ratiba za michezo yao ya ASFC hazijapangiwa siku.

Yanga ndiyo watetezi wa michuano hiyo ikitwaa taji msimu uliopita kwa kuitungua Azam FC kwa bao 1-0 na kwenye hatua hiyo imepangwa kucheza na Hausung ya Njombe, huku watani wao, Simba wakipangwa na Tembo ya Tabora, lakini hadi sasa kuna utata wa mechi za timu hizo kuchezwa lini kutokana na ratiba ngumu.

Ugumu upo zaidi kwa Simba kulinganisha na Yanga, japo mabosi wa klabu hiyo wameweka wazi kuwa kwa sasa wanasubiri waendeshaji wa michuano hiyo TFF kupanga wacheze lini kutokana na muingiliano wa ratiba za timu hizo.

Simba ina mechi ya Ligi Kuu itakayopigwa kesho Ijumaa kabla ya Jumanne ijayo kuumana na Wydad Casablanca ya Morocco, halafu itamalizana na KMC Desemba 23 kabla ya kusafiri hadi Kigoma kucheza na Mashujaa Desemba 26 na siku tatu baadaye itakuwa Tabora kuumana na Tabora United.

Januari Mosi, Simba itarudi Dar es Salaam kucheza mechi nyingine ya Ligi dhidi ya Azam kabla ya kusafiri hadi Zanzibar kwa michezo ya michuano ya Kombe la Mapinduzi 2024.

Kwa upande wa Yanga itashuka uwanjani Jumamosi kuvaana na Mtibwa Sugar katika Ligi Kuu kabla ya Desemba 20 kucheza na Medeama katika mechi ya Ligi ya Mabingwa Afrika kabla ya Desemba 22 kuumana na Tabora United mjini Tabora na Desemba 29 itakwaruzana na Mashujaa.

Kagera yenyewe imepangwa kuumana na Dar City mjini Bukoba na Mtibwa Sugar kuialika Nyakangwe ya Geita, Uwanja wa Manungu, lakini ratiba kwa sasa bado hazijapangwa.

Ofisa Habari wa TFF, Cliford Ndimbo alipoulizwa jana juu ya ratiba ya mechi za Simba na Yanga, alisema watazipanga kulingana na nafasi zitakavyopata, huku akidai kwamba hana uhakika kama mechi za vigogo hao zinaweza kuvuka hadi mwakani kwa sababu nafasi bado ipo.

Kwa upande wa maofisa habari wa Simba na Yanga, Ally Kamwe (Yanga) na Ahmed Ally wa Wekundu wa Msimbazi walisema kwa nyakati tofauti walipozungumza na Mwanaspoti kuwa wanasubiri ratiba zitakazopangwa na TFF na timu zao zitakuwa tayari kucheza, ingawa ni kweli ratiba kwa sasa zinazibana timu hizo zinazowakilisha nchi kimataifa - zote zikishiriki Ligi ya Mabingwa Afrika zikiwa katika hatua ya makundi.

Msimu uliopita Yanga ilibeba ubingwa wa Kombe la Shirikisho la Azam kwa kuifunga Azam FC katika mchezo uliopigwa kwenye Uwnaja wa Mkwakwani mjini Tanga, Juni 12, mwaka huu.

Katika mchezo huo, Yanga ilibeba ndoo kwa bao lililofungwa na Kennedy Musonda katika dakika ya 16 aliyeunganisha kwa kichwa krosi iliyopigwa na winga Tuisila Kisinda.

Kisinda alikuwa akicheza Yanga kwa mkopo kutoka Berkane ya Morocco alikorejea baada ya msimu kumalizika.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live