Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kumbe yale mateso ya Madrid uwanjani ni staili yao

Real Madrid Uefaaaaaaaaaa Kumbe yale mateso ya Madrid uwanjani ni staili yao

Mon, 3 Jun 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Wachezaji wa Borussia Dortmund bado hawajui waielezeeje. Hata wachezaji wa Manchester City na wa Bayern Munich pia. Real Madrid imeshinda taji lake la 15 la Ligi ya Mabingwa Ulaya katika mtindo ambao unaonekana ni kama bahati tu.

“Hatukutumia nafasi zetu na Madrid hawawezi kukusamehe,” alisema Edin Terzic Kocha wa Dortmund baada ya filimbi ya mwisho ya mchezo na vijana wake waliitesa kwelikweli Real Madrid ya kocha Carlo Ancelotti.

Lakini, unachoambiwa ni kwamba kumbe Real Madrid hiyo ilikuwa mbinu yao ya msimu huu. Wanapocheza uwanjani unaona wanateseka, mpinzani anaamini muda wowote anaweza kupata ushindi, kisha wao wakipata nafasi tu, wanamaliza mechi.

“Sisi ni timu ambayo utaona tunataabika sana uwanjani, lakini sisi wachezaji tunajua. Ni ngumu kwetu kucheza staili hiyo ya kutotengeneza nafasi nyingi, lakini tunajua kuna mahali tutapata kitu,” alisema Lucas Vazquez baada ya kipute hicho cha Wembley.

“Ancelotti alituambia kuhusu hii staili ya ‘dead man’s tactic’ kwamba bado inafanya kazi. Tunaonekana kama tupo kwenye hali mbaya sana, lakini mwisho wa mechi, tunashinda sisi.”

Borussia Dortmund ilikuwa kwenye kiwango bora sana kabla ya kuruhusu mabao mawili ya Dani Carvajal na Vinicius Junior kwenye dakika za mwisho. Lakini, Real Madrid ilionekana kucheza kwa staili hiyo ya kichovu tangu kwenye mchezo wa robo fainali mbele ya Man City na kwenye nusu fainali dhidi ya Bayern. Kwenye mechi zote hizo, Real Madrid ilionekana kama itachapwa hivi, lakini mwisho wa mchezo, yenyewe ndiyo iliyoibuka kidedea. Wachambuzi wa soka wanasema ni zali la mentali.

Chanzo: Mwanaspoti