Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kumbe si Kagere tu, wengine hawa hapa

Kagere X Baleke Kumbe si Kagere tu, wengine hawa hapa

Fri, 12 Jan 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Straika Meddie Kagere juzi usiku alipiga penalti dhaifu iliyoibua mjadala kwa wadau wa soka wakati Singida FG ikiaga michuano ya Kombe la Mapinduzi, huku mastaa wengine wakifunguka stresi walizowahi kukutana nazo kwa kukosa penalti kama nyota huyo wa zamani wa Simba.

Kagere alikosa penalti iliyokuwa ya mwisho kwa Singida ambayo ingeweza kuirejesha timu mchezoni, lakini aliipiga kwa mbwembwe na kuzuiwa na miguu ya kipa Ally Salim na kuivusha Simba kwenda nusu fainali.

Wengine waliokosa penalti za juzi kwa Singida alikuwa ni mabeki, Hamad Waziri na Gadiel Michael, huku kwa upande wa Simba walikuwa ni Shomari Kapombe na Saido Ntibanzokiza.

Hiyo sio mara ya kwanza kwa Kagere kukosa penalti, kwani alishakosa dhidi Yanga, Januari 13, 2021 katika michuano kama hiyo ya Mapinduzi na Wanajangwani kubeba ubingwa kwa penalti 4-3, pia alikosa katika mechi ya Ligi Kuu akiwa na Simba dhidi ya KMC, Aprili 25, 2020 na akawafunga hao hao KMC bao la penalti Desemba 16, 2020.

Ingawa huko nyuma aliwahi kuzungumzia kukosa penalti ni jambo la kawaida, ila alivyotafutwa awamu hii, ilikuwa ngumu kupata ushirikiano kwake, kwani alipopigiwa simu iliita bila kupokelewa, hata hivyo, mastaa wengine waliowahi kupata kasheshe kama hiyo ya kukosa akiwamo straika wa zamani wa Yanga, Said Bahanuzi, aliyekiona cha moto 2014 baada ya kukosa dhidi ya Al Ahly ya Misri ilikuwa mechi ya Ligi ya Mabingwa Afrika alisema; “Penalti ilizuia nongwa, wakati bado nipo Misri nilipigiwa simu kwamba mashabiki wamekwenda kufanya fujo nyumbani kwangu, huku wakitukana matusi ya kila aina, mke na watoto walikuwa ndani na kama haitoshi wakati tunarudi hakuna mchezaji aliyekuwa ananiongelesha.”

“Nilijihisi mkosaji nisiyestahili kusamehewa, roho ya kuacha soka ilinivaa, aliyenisaidia ni kiongozi Hussein Ndama, alinikalisha chini, akanijenga na kuniambia haikuwa ridhiki yako, himili mtikisiko unaokupata, nakumbuka siku hiyo alinipa dola 500, kwani aliona jinsi wenzangu walivyokuwa wanapewa pesa na mashabiki halafu mimi nilinyimwa,” alisema Bahamuzi aliyewahi kuwika Mtibwa.

Nyota mwingine aliyewahi kukiona cha moto kwa mashabiki wake baada ya kukosa penalti ni straika wa zamani wa Simba, Adam Salamba dhidi ya Asante Kotoko, 2018, ambapo alikaririwa akisema; “Baadhi ya mashabiki walikuwa wananiona nanata sana hadi uwanjani, ila nashukuru sana kaka zangu Emmanuel Okwi, Clatous Chama, John Bocco walinijenga kuona ni mambo ya kawaida hata mastaa ulaya wanakosa.”

Kocha wa makipa wa Mtibwa Sugar, Patrick Mwangata alisema; “Alivyopiga Kagere kwa dharau, angefunga kipa angeonekana dhaifu, ila kwa sababu Ally Salim kadaka Kagere anaonekana dhaifu, ndio mambo ya mpira.”

Kocha mwingine aliyechangia hilo ni Meja Mstaafu wa Jeshi, Abdul Mingange alisema “Penalti zinahitaji utulivu wa hali ya juu, kwani hapo kunakuwa na ubora wa kipa na mpigaji, nilichokiona kwa Kagere alitaka kupiga kwa kutokutumia nguvu, ingemshinda Salim kusemwa kungekuwa upande wake.”

Chanzo: Mwanaspoti