Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kumbe Taifa Stars bado ni mkuki moyoni

Stars 70Tc.jpeg Kumbe Taifa Stars bado ni mkuki moyoni

Tue, 23 Jan 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Wakati mwingine mwanadamu anayeishi maisha marefu ni yule anayekitazama kila kitu katika mtazamo chanya. Mimi nafuata falsafa hii. Najaribu kuchukulia kila kitu kwa urahisi. Hata hivyo, juzi nilishindwa kufanya hivyo katika dimba la Laurent Pokou mjini San Pedro hapa Ivory Coast.

Dakika ziliyoyoma huku Taifa Stars ikikaribia kupata ushindi wake wa kwanza wa kihistoria katika michuano ya Afcon. Haijawahi kutokea. Ningekuwa miongoni mwa Watanzania wachache kushuhudia jambo hilo lilitokea mbele ya mboni za macho yangu. Haikutokea.

Niliumia. Saimon Msuva alikuwa ameitanguliza Stars kwa bao la kipindi cha kwanza. Wakati ule wakitegea Zambia kufanya makosa halafu wao wafanye mashambulizi ya kushtukiza. Ilifanya kazi. Himid Mao alipora mpira, akampitishia Mbwana Samatta ambaye aliukimbiza mpaka katika boksi akampasia Msuva akafunga.

Huyu huyu Msuva alichezewa rafu katika kipindi cha kwanza na nahodha wa Zambia, Rodrick Kabwe. Halafu baadaye staa mwenzake, Samatta akachezewa rafu na Kabwe. Akapewa umeme. Ilikuwa faida ya ajabu kwa Stars. Haijawahi kutokea wapinzani wa Tanzania kupungua katika pambano la Mataifa ya Afrika.

Na sasa ilibaki kazi nyepesi tu ya kulinda ushindi. Kulikuwa na namna mbili. Kwanza kabisa ni kuwa ni nidhamu ya ulinzi ambayo inawezekana kama ukijihami kwa chini au kukaa na mpira kwa nidhamu kwa muda mrefu. Lakini hapo hapo tungeweza kumaliza mechi kwa kujipatia bao la pili.

Hakuna jambo tulilofanya vizuri katika yote haya. Tulipiga pasi nyingi za nyuma na hivyo kuuweka mchezo rehani. Wapinzani wetu siku zote wanajiona bora kuliko sisi. Waliendelea kujaribu kupishana na sisi hata baada ya wao kupungua. Hii ilikuwa nafasi nzuri kwetu kumalizia mechi yetu vema. Hatukufanya vema.

Tulichokosa ni ukomavu wa wachezaji wetu katika hatua hizi. Ni ukosefu wa ukomavu katika hatua hizi. Bado nasisitiza kwamba tunahitaji wachezaji wetu wakacheze nje wapate uzoefu wa kucheza katika hatua hizi. Lakini pia tunahitaji makocha wetu wawe na uzoefu zaidi.

Kwa mfano, baada ya Kabwe kupewa kadi nyekundu ilikuwa kipimo tosha kwa Hemed Morocco na Juma Mgunda kujua nini kifanyike katika kipindi cha pili kwa ajili ya kuihakikishia Tanzania ushindi wake wa kwanza katika michuano hii. Ukweli ni kwamba hatukujua hasa ambacho walitaka kifanyike.

Awali tulikuwa tunapiga pasi nyingi kuelekea kwetu. Mashambulizi yetu kwao yalikuwa machache ambapo mara mbili Mohammed Hussein ‘Tshabalala’ alishindwa kuchukua maamuzi sahihi wakati akikaribia katika boksi la adui. Walau yeye alishindwa, wengine hawakuwa na jitihada.

Kilichoshangaza ni kwamba baada ya kufunga bao, na hata kabla Kabwe hajatolewa, mechi ilikuwa salama kwa Stars. Walionekana kuwa katika uzito sawa. Baada ya Zambia kupungua Stars ikazima moto. Ni kosa la wachezaji au makocha waliokuwa wamekaa katika benchi la ufundi?

Lakini bado tunapaswa kutafakari. Stars ilikuwa inafanya mazoezi ya namna gani kuelekea michuano hii. Kadri dakika zilivyosonga mbele ndivyo ambavyo Stars walionekana kuchoka. Na kuchoka ndiko kulikopelekea kukosekana kwa umakini.

Hapa nchini Ivory Coast timu nyingi zinalalamika kuchoka kwa wachezaji wake kutokana na joto kali lililopo nchini hapa. Hata hivyo, hilo lilipaswa kuwa faida kwa wachezaji wa Taifa Stars ambao wengi wanacheza nchini. Tanzania ina joto hata kama inazidiwa kidogo na Ivory Coast. Ilipaswa kuwa faida kwetu lakini haikuwa hivyo.

Kadri dakika zilivyoyoyoma ndivyo tulivyochoka zaidi kuliko Zambia. Hapa ndipo Patson Daka aliporukia mpira wa kichwa akiwa peke yake angani kufuatia kona ya Clatous Chotta Chama. Na kama zingeongezwa dakika nyingine basi Zambia wangefunga tena.

Baada ya bao hili ndipo Stars walipoleta ule unafiki maarufu uliopo katika mpira. Stars wakafanya kile ambacho walitakiwa kufanya wakati wanaongoza bao moja. Walijaribu kwa haraka kusaka bao. Sasa hivi ndio Samatta akaanza kukimbiza mpira kwa kasi zaidi kuelekea katika lango la adui. Sasa hivi ndio Stars walipiga pasi za haraka haraka kuelekea kwa Zambia. Haikusaidia.

Mwamuzi alipomaliza pambano tuliishia kubakia na hesabu ngumu za vidole. Kama tungewafunga Zambia tulikuwa na hesabu nzuri ya kutoa sare katika pambano la mwisho dhidi ya DRC Congo huku tukisusbiri Morocco amfunge Zambia au watoke sare. Ni jambo ambalo lingewezekana kwa kiasi kikubwa.

Lakini sasa tunakabiliwa na kazi kubwa ya kumfunga Mcongo halafu Zambia na Morocco watoke sare au Zambia wafungwe. Ni kazi ngumu. Ulazima wa kumfunga Congo ni moja kati ya kazi ngumu katika soka. Wanatuzidi mambo mengi kuanzia uwezo na hadhi ya mchezaji mmoja mmoja hadi kucheza kitimu. Wana timu haswa.

Walituonyesha tofauti yao na sisi kwa namna walivyokabiliana na Morocco. Wakati sisi tulikuwa wanyonge wao walionyesha ubora wao. Walichomoa bao na wakataka la ushindi. Na ni mechi ambayo inatia shaka kufikiria namna ambavyo pambano letu na Congo linavyoweza kwenda. Kama Fiston Mayele anaanzia benchi unaweza kufikiria ubora wa timu yao.

Vyovyote ilivyo tuanze kufikiria namna ya kushindana katika michuano ijayo. Hadi sasa inaonekana imeanza kuwa rahisi kuja katika michuano hii lakini bado tupo katika uwezo wa ushiriki tu na si ushindani. Tunahitaji kufanya uwekezaji wa kisasa katika soka.

Chanzo: Mwanaspoti