Uongozi wa Klabu ya Simba imesema kuwa unatambua mchezo wao wa nusu fainali ya African Football League dhidi ya Al Ahly ni mgumu ndani na nje ya uwanja hivyo wamejidhatititi kuhakikisha wanapata matokeo chanya na kusonga mbele.
Hayo yamesemwa na Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally wakati akizungumza na wanahabari nchini humo kuelekea mchezo huo utakaopigwa leo Oktoba 24, 2023 nchini Misri baada ya ule wa kwanza kumalizika kwa sare ya bao 2-2 katika Dimba la Mkapa.
“Mchezo wa dar wa bao 2-2 umetupa morali kwamba tunaweza kupata matokeo katika mchezo ujao. Ni timu tano pekee duniani ambazo zimewahi kuifunga Al Ahly zaidi ya bao 2 kwenye miaka mitano iliyopita, Real Madrid, Flamingo ya Brazil, Mamelodi Sundowns, Pyramids na Simba Sc hata Waarabu wenyewe wameshamshindwa ndugu yao Ahly, kwa hiyo Simba msituchukulie poa.
“Tukichanga karata zetu vizuri hasa mwalimu Robertinho akaweka mpango mzuri wa kuzuia tusiruhusu kufungwa mabao ndani ya dakika 90, maana yake wale wa mbele wanaweza kupambana na kupata mabao. Hatima ya Mnyama kwenda nusu fainali ipo kwa Mnyama mwenyewe,” amesema Ahmed.