Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kumbe Mourinho, Wenger hawajamalizana

Jose Mourinho X Wenger Utataaaa Kumbe Mourinho, Wenger hawajamalizana

Mon, 3 Jun 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Jose Mourinho haungi mkono kabisa pendekezo la Arsene Wenger kuhusu sheria mpya inayopendezwa kuhusu kuotea.

Mourinho aliyekuwa mchambuzi kwenye televisheni ya TNT Sports wakati wa mchezo wa fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya usiku wa juzi Jumamosi, ambapo Real Madrid iliichapa Borussia Dortmund mabao 2-0 na kubeba taji lake la 15, alifichua wazi haungi mkono sheria hiyo mpya, huku akigoma kabisa kukutana ana kwa ana na Wenger kwenye studio hizo.

Kocha huyo wa zamani wa Chelsea na Manchester United alikuwa sambamba na Rio Ferdinand kujadili ubingwa wa Real Madrid, ambayo pia ni timu yake aliyowahi kuinoa.

Mourinho, 61, ambaye atakwenda kuwa kocha wa Fenerbahce, alimtaka Toni Kroos kubadili mawazo yake ya kuhusu kustaafu. Lakini, katika usiku huo, jina la Wenger lilitajwa na Mourinho kutoa maoni.

“Arsene Wenger alikuwapo maeneo haya kabla na baada ya mechi. Ningependa kumnasa kwa ajili ya mahojiano ya haraka,” alisema mtangazaji Laura Woods.

Kisha Ferdinand aliongeza: “Ningependa pia kuona wakiwa pamoja na Jose!”

Baada ya hapo, Mourinho aliingilia kati na kusema: “Muulizeni anataka kufanya nini kwenye sheria ya kuotea. Mungu wangu, acheni mimi niondoke kabla hajaja.”

Baada ya kucheka, Woods alisema: “Tulifanya hivyo ili msikutane -- ila ningependa mkutane.”

Akikunja ndita, Mourinho alisema: “Hapana, huu ni muda wangu wa kuondoka!”

Wenger alipambana na Mourinho kwa miaka mingi sana walipokuwa makocha, lakini bosi huyo wa zamani wa Arsenal kwa sasa ni ofisa wa Fifa, anayeshughulikia maendeleo ya soka. Na moja ya shughuli zake, Wenger amekuja na pendekezo la kufanya mabadiliko kwenye sheria ya kuotea.

Sheria hiyo mpya, mchezaji atahesabika kuwa ameotea kama tu mwili mzima utakuwa umezidi mchezaji wa mwisho, lakini endapo kama mwili wote umezidi, isipokuwa kiungo kimoja au viwili ambavyo vinaruhusiwa kufunga bao vikiwa bado kwenye mstari sawa na mchezaji wa mwisho, hapo mchezaji huyo atakuwa hajaotea. Jambo hilo ndilo ambalo Mourinho haliungi mkono.

Chanzo: Mwanaspoti