Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kumbe Arsenal haijamaliza kwa Osimhen

Victor Osimhen Rekodi Victor Osimhen

Wed, 31 Jul 2024 Chanzo: Mwananchi

Arsenal imeendelea kuwa na matumaini ya kumsajili straika wa Napoli, Victor Osimhen dirisha hili licha ya kiasi kikubwa cha pesa kinachohitajika na timu yake ili kumuuza.

Osimhen ambaye pia anawindwa na PSG, mkataba wake na Napoli unatarajiwa kumalizika mwaka 2026 na ana kipengele kinachoitaka timu inayomhitaji kulipa zaidi ya Pauni 111 milioni ili kuuvunja.

Kipengele hicho kilichopo katika mkataba wake kinadaiwa kuzirudisha nyuma timu nyingi na sasa Napoli imeripotiwa kuwa tayari kujadiliana na timu inayomhitaji na ikiwezekana itamuuza kwa pesa pungufu.

Chelsea pia ni moja kati ya timu zinazohitaji saini yake na inataka kufanya mabadilishano ya wachezaji na itawapa Romelu Lukaku kisha wao kumchukua Osimhen.

Kocha mpya wa Napoli, Antonio Conte anahitaji saini ya Lukaku na amewaambia mabosi wa timu hiyo kuhakikisha wanamsajili lakini nao pia wanasubiria kwanza kuona kama watamuuza Osimhen ndio watoe pesa kwa ajili ya Lukaku.

Wakati huo huo kocha wa Arsenal, Mikel Arteta amewaambia mabosi wa timu hiyo anataka kuboresha eneo la kiungo kwa kusajili staa wa Real Sociedad na Hispania, Mikel Merino katika dirisha hili. Arsenal imekuwa ikihusishwa kutaka kumsajili staa huyu kwa muda mrefu lakini hivi karibuni Arteta ameripotiwa kutilia mkazo na kusisitiza anahitaji saini ya fundi huyo kwani anamwona kama sehemu ya mipango yake kwa msimu ujao.

MSHAMBULIAJI wa Crystal Palace na Ghana, Jordan Ayew, 32, ameingia katika rada za Leicester City inayohitaji kumsajili katika dirisha hili la majira ya kiangazi. Ayew ambaye amekuwa akitamba sana katika michuano ya mataifa ya Afrika (Afcon) mara kadhaa alizoshiriki akiiwakilisha Ghana, msimu uliopita alicheza mechi 37 za michuano yote na kufunga mabao manne.

WEST Ham huenda ikaangukia pua katika mchakato wao wa kumsajili kiungo wa AS Monaco, Youssouf Fofana, 25, katika dirisha hili kwa ajili baada ya kuibuka kwa ripoti kwamba AC Milan fundi huyo anapendelea zaidi kujiunga na AC Milan badala ya wao. Fofana mkataba wake unamalizika mwaka 2025. Msimu uliopita alicheza mechi 35 za michuano yote.

LICHA ya Arsenal kuonyesha nia ya kutaka kumsajili winga wa Bayern Munich na Ujerumani katika dirisha hili, Leroy Sane, ripoti zinaeleza kwamba staa huyo hana mpango wa kuondoka kwa sasa. Sane ambaye mkataba wake na Bayern unamalizika mwakani, ana umri wa miaka 28 na msimu uliopita alicheza mechi 42 za michuano yote na kufunga mabao 10.

DILI la straika wa Arsenal, Eddie Nkeitah kujiunga na Marseille dirisha hili huenda likafeli kwa kile kinachoelezwa timu hizo zinashindwa kufikia mwafaka katika masuala ya ada ya uhamisho. Ili kumuuza mshambuliaji huyu, Arsenal inaripotiwa kuhitaji kiasi kisichopungua Pauni 50 milioni wakati Marseille ikiwa tayari kutupa chini ya Pauni 30 milioni.

MANCHESTER United huenda ikafanya mabadilishano ya wachezaji na PSG ambapo inaweza kumchukua beki wa kulia, Nordi Mukiele, kiungo, Manuel Ugarte na beki wa kati raia wa Slovakia, Milan Skriniar ili kumruhusu Jadon Sancho aende kwenye timu hiyo. PSG imekuwa ikihusishwa kutaka kumsajili Sancho tangu wiki iliyopita. Mkataba wa Sancho na Man United unatarajiwa kumalizika mwaka 2026.

WEST Ham imeanza mazungumzo na Manchester United kwa ajili ya kuipata saini ya beki wa kulia wa timu hiyo, Aaron Wan-Bissaka, 26, na inataka kutoa Pauni 15 milioni ili kufanikisha mchakato wa kumsajili. Bissaka msimu uliopita alicheza mechi 30 za michuano yote na amekuwa akihusishwa na timu mbalimbali za nje ya England ni pamoja na Galatasaray.

Chanzo: Mwananchi