Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kule Qatar ni maajabu tu, hapa Bongo kuna mengi ya kujifunza

VAR Mbelee Kule Qatar ni maajabu tu, hapa Bongo kuna mengi ya kujifunza

Wed, 30 Nov 2022 Chanzo: Mwanaspoti

Michuano ya Kombe la Dunia inazidi kupamba moto Qatar ambapo baadhi ya timu zimeanza kujua mwelekeo.

Wakati Kylian Mbappe wa Ufaransa,Rashford wa England, Gakpo wa Uholanzi na Enner Valencia wa Ecuador wakiwa wanaongoza katika safu ya ufungaji kwa kufunga mabao matatu kila mmoja, baadhi ya timu zipo njia panda kujua kama zitafuzu hatua ya 16 bora au hapana.

Kwa upande mwingine, ratiba za mechi za jana ilihitimisha safari ya kufungasha virago kwa baadhi ya timu katika mashindano hayo ambapo Ecuador na Qatar ziliaga mashindano katika kundi A baada ya Uholanzi na Senegal kufuzu.

Kwa upande wa kundi B, England na Marekani zimefanikiwa kufuzu kwa hatua inayofuata baada ya England kuichapa Wales Mabao 3-0 huku Marekani wakishinda bao 1-0 dhidi ya Iran.

Baada ya muhtasari huo, sasa turejee katika maudhui ya kolamu hii ambayo inazungumzia zaidi masuala mbalimbali ya sheria za soka na hasa matukio tata katika mechi mbalimbali za soka.

Nikianzia Qatar, juzi usiku kulikuwa na mechi ngumu kati ya Hispania na Ujerumani ambayo matokeo yake yalikuwa ya bao 1-1. Mechi hiyo ilikuwa na msisimko wa hali ya juu na kuwavutua mashabiki wengi wa soka hapa nchini.

Ni mechi iliyojaa ufundi mwingi na mashabiki wa soka walishindwa kutabiri kutokana na umuhimu wa mechi hiyo na hasa upande wa matokeo.

Mwamuzi kutoka Uholanzi, Danny Makkelie alikataa bao lililofungwa na beki wa Ujerumani, Antonio Rudiger baada ya kunaswa katika mtego wa kuotea.

Mabeki wa Hispania walishindwa kumzuia Rudiger ambaye aliruka na kuupiga kichwa mpira huo kufuata mpira uliopigwa na Joshua Kimmich na Rudiger kupiga kichwa kilichomshinda kipa wa Hispania, Unai Simon.

Tofauti na michezo mingine, wachezaji wa Hispania hawakuonyesha kupinga bao hilo kama mchezaji huyo wa Ujerumani alikuwa amezidi, lakini VAR ilifanya kazi yake na kufuta bao hilo.

Ilikuwa vigumu kugundua iwapo Rudiger alikuwa amezidi, lakini alimzidi kiungo mkabaji wa Hispania, Sergio Busquets ambaye pamoja na kuonekana kumzuia Rudiger, bado hakuweza kusababisha kumwezesha kuupata mpira huo na kufunga.

Kwa mujibu wa sheria namba 11 ya soka, Rudiger alizidi ndiyo maana bao hilo lilikataliwa na mwamuzi na hata wachezaji wa Ujerumani hawakuonyesha kupinga baada ya uamuzi huo.

Hata hivyo, bila ya kuwa na msaada wa VAR, mwamuzi angekubali bao hilo kwani hata mwamuzi msaidizi hakupinga bao zaidi ya taarifa ya haraka ya VAR ambayo mwamuzi alitaarifiwa.

SOKA LA BONGO

Yanga iliendeleza wimbi lake la ushindi katika mashindano ya Ligi Kuu Bara baada ya kuifunga Mbeya City kwa mabao 2-0.

Katika mchezo huo uliofanyika kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, mwamuzi Ramadhan Kayoko alikataa bao la Tuisila Kisinda alilofunga katika dakika ya 38 ya mchezo kwa kupiga shuti nje ya eneo la hatari, ikidaiwa kwamba kulikuwa na mazingira ya kuotea.

Katika tukio hilo, mwamuzi msaidizi wa pili hakukataa bao na kuanzisha mwendo kurejea katikati kwa lengo la kuanza mpira kwa mujibu wa taratibu. Hata hivyo, zoezi hilo halikufanyika kutokana na uamuzi wa mwamuzi wa kati ya kukataa bao.

Kwa mujibu wa sheria 11 ya soka kuhusiana na kuzidi au kuotea, ni wazi kuwa mwamuzi aliinyima Yanga bao kwani tafsiri ya kuzidi kwa kumzuia kipa kuona shuti la Kisinda ilitumika isivyo kwani wakati huo Mayele alikuwa sambamba na beki wa Mbeya City.

AZAM V COASTAL

Bao la tatu la Azam FC lilikuwa halali. Kama malalamiko ni muda, basi mashabiki wa soka lazima wajue kuwa mtunza muda mkuu katika soka ni mwamuzi na wala sio ofisa mwingine yeyote.

Hivyo mwamuzi anajua amefidia dakika ngapi katika mchezo huo pamoja na kumaliza mechi baada ya Azam kufunga bao la tatu.

Chanzo: Mwanaspoti