Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kule Mbeya hesabu zimeanza upyaaa

Kuleeeeee Kule Mbeya hesabu zimeanza upyaaa

Tue, 9 Jan 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Licha ya kupunguzwa kasi kwenye mechi zilizopita, Mbeya Kwanza na Ken Gold zimesema bado hesabu ni kupanda Ligi Kuu Bara msimu ujao ziko palepale, huku zikichora ramani ya ushindi katika michezo inayofuata.

Timu hizo za mkoani Mbeya zimekuwa na matokeo mazuri hasa kwenye mzunguko wa kwanza zikimaliza katika nafasi mbili za juu kwenye Championship huku zikianza kwa maumivu raundi ya pili.

Ken Gold ambao inaongoza ligi hiyo kwa alama 36, ilipunguzwa kasi na Transit Camp zilipomaliza dakika 90 kwa sare ya kufungana bao 1-1, huku Mbeya Kwanza ikilala kwa mabao 2-1 dhidi ya Polisi Tanzania na kushuka hadi nafasi ya tano ikiwa na alama 32.

Timu hizo zinatarajia kurejea uwanjani wikiendi hii, ambapo Mbeya Kwanza itamenyana na FGA Talents, huku Ken Gold ikibaki ugenini dhidi ya Green Warriors. Kocha mkuu wa Ken Gold, Jumanne Challe amesema walipambana kutafuta ushindi lakini haikuwa bahati yao akieleza kuwa bado hawajatoka kwenye malengo.

“Tunakwenda kujipanga upya na mchezo ujao tunafahamu ugumu wake kwa muda huu wa lala salama. Tunahitaji pointi tatu ambazo zitatuweka nafasi nzuri kubaki kileleni,” amesema Challe.

Kocha msaidizi wa Mbeya Kwanza, Michael Mnyali amesema walihitaji ushindi, lakini matokeo ya mpira yaliwakatili na kusisitiza kuwa hawatakata tamaa badala yake watasahihisha makosa kwa ajili ya mechi ijayo.

“Hizi ni mbio za marathoni. Tunaamini tutarejea kwenye nafasi yetu kwa sababu nia na malengo ni kuhakikisha tunarejea Ligi Kuu. Hatujakata tamaa na vijana wana ari na morali,” amesema kocha huyo. Kwa sasa Pamba Jiji iko nafasi ya pili ikiwa na alama 34.

TAKWIMU NZITO Baada ya mwishoni mwa Pamba Jiji kukwea katika nafasi ya pili ilipoifumua Cosmopolitan kwa mabao 2-1 ugenini jijini Dar es Salaam, na kuchupa kutoka nafasi ya nne ikiishusha Mbeya Kwanza na TMA FC katika msimamo unaongozwa na KenGold yenye pointi 36 katika mechi 16 ilizocheza, takwimu za namba zimeanza kushtua.

Hata hivyo, ushindi wa Pamba kumbe unaibeba kutokana na namba tu za pointi, lakini timu hiyo iliyoshinda michezo 10 inalingana na Biashara United pamoja Mbeya Kwanza ambazo pia zimeshinda idadi hiyo ya michezo, zikiifuata KenGold iliyoshinda mechi 11.

Timu zingine zilizokamata nafasi za juu kwa mechi nyingi zilizoshinda ni TMA FC iliyoshinda tisa ikishoka namba nne katika msimamo ikiwa na alama 33, huku Mbuni FC ikishinda mechi nane ilhali katika msimamo ikishika nama sita na pointi 27.

Ukiachana na timu hizo, Mbeya City na Polisi Tanzania zimeshinda mara sabaa zikiwa nafasi ya saba na nane mtawalia, huku Stand United ikishika nafasi ya tisa kwa ushindi wa michezo sita, ikifuatiwa na Green Warriors, FGA Talents na Pan Africans zilizoshinda michezo minne zikifuatana kwa mtiririko huo katika msimamo.

Transit Camp na Cosmopolitan zimeshinda mechi tatu zikishika namba 13 na 14, huku Copco ikishinda mechi tatu ikiwa ya 15 katika msimamo unaofungwa na Ruvu Shooting ambayo haina ushindi wowote.

Hata hivyo, maajabu mengine katika msimamo huo yapo katika timu iliyo na sare nyingi ambayo ni TMA FC iliyosare mara sita sawa na Green Warriors, huku Cosmopolitan na Transit Camp zikiifuata kwa sare tano ilhali Pamba, Mbeya City na Stand United zina sare nne.

Timu zenye sare tatu ni Copco, Pan Africans, FGA Talents, Mbuni na Biashara United huku Mbeya City, Polisi Tanzania na Ruvu Shooting zikiwa zimetoka sare mara mbili katika michezo 16.

Kati ya timu 16 zinazowania kupanda Ligi Kuu msimu ujao zile mbili zilizo mkiani yaani Ruvu Shooting na Copco zimechapwa jumla ya mechi 24 zilizocheza ikiwa ni vipigo viwili zaidi ya vile ambavyo timu saba kwa ujumla wake zilizo juu mwa msimamo zimevipata. Timu hizo kuanzia namba moja hadi saba zimepoteza michezo 22 kwa ujumla wake.

Upande wa mabao ya kufunga, safu ya ushambuliaji ya KenGold imeendelea kuwa bora zaidi ikifunga mabao 29, ikifuatiwa na Biashara United iliyotupia 28, huku Pamba ikiwa ya tatu na mabao 24 inayofuatiwa na Mbeya Kwanza na Mbuni zilizofunga mabao 23 kila moja. Timu zingine 12 zimefunga chini ya mabao 20. Kwa ujumla timu zote zimefunga mabao 286 zikiwa na jumla ya pointi 355.

Chanzo: Mwanaspoti