Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kuku aliuzwa akanunuliwa kiatu beki Mashujaa

Beki Mashujaa Kuku aliuzwa akanunuliwa kiatu beki Mashujaa

Thu, 21 Sep 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Soka ni ajira kama zilivyo ajira nyingine na wazazi wengi wameanza kuamini katika mchezo huo kwa kutoa nafasi kwa watoto wao kuucheza.

Miaka ya nyuma ni wazazi wachache walikuwa wakiupa kipaumbele mchezo huo kwa kutoa nafasi kwa watoto zao kuamua kuingia kuucheza.

Mwanaspoti limepata nafasi ya kuzungumza na beki wa Mashujaa, Baraka Mtuwi ambaye amefunguka mambo mbalimbali na namna familia yake ilivyompa uhuru wa kuchagua nini anataka kufanya na baada ya hapo kumuongezea nguvu kwa kumsaidia baadhi ya mahitaji.

Beki huyo amekiri tangu anakua lengo lake lilikuwa ni kuwa mchezaji bila kuvutiwa na mchezaji yeyote mapenzi yake yalikuwa ni kucheza soka na kuamini katika mchezo huo kuwa anaweza kufikia malengo.

KUKU WALIVYONUNUA NJUMU

Mchezaji aliyekamilika ni yule ambaye anakuwa na viatu vizuri kwa ajili ya kuchezea mpira ukiachana na mpira wa mtaani ambao unaweza kucheza hata bila viatu.

“Tangu naanza mpira nikiwa mdogo wazazi wangu walitokea kuniamini kwa kila ninachokifanya na kunipa sapoti hawajawahi hata siku moja kuwa kikwazo kwangu walikuwa wakiniambia natakiwa kuchagua kilichokuwa bora katika maisha yangu ambacho naamini kitanitoa.”

Anasema chaguo lake liliangukia kwenye soka anamshukuru Mungu anaendelea kupambana kuhakikisha anafikia malengo huku akikiri soka bado halijamlipa,” anasema.

Akizungumzia sapoti aliyowahi kuipata kutoka kwa familia yake anasema anakumbuka kiatu chake cha kwanza kuchezea soka alinunuliwa na kaka yake baada ya kuuza kuku.

“Kiatu changu cha kwanza nilinunuliwa na kaka yangu tena alidiriki kuuza kuku wake akaninunulia kiatu cha mpira sina kumbukumbu vizuri alinunua bei gani ila kwa sasa navaa kiatu cha kuanzia laki kwenda juu,” anasema Mtuwi ambaye amekipiga Namungo, Ruvu Shooting timu ya vijana hadi kupandishwa Gwambina sasa yuko Mashujaa ya Kigoma.

HUMWAMBII KITU KWA NYONI

Erasto Nyoni ni mchezaji kiraka ambaye anacheza nafasi nyingi uwanjani amekuwa kivutio kwa wachezaji wengi wa miaka ya hivi karibuni ambao wanafunguka kuvutiwa na uchezaji wake beki wa Mashujaa amekuwa miongoni mwa wachezaji hao.

“Mbali na kucheza nafasi ya beki sasa, nilianza na kiungo wa chini na juu ni mchezaji ambaye nimekuwa nikimtazama zaidi ni Nyoni kwaajili ya kujifunza vitu kutoka kwake.

“Erasto ni kioo changu ni mchezaji ambaye ananifanya niuone mpira ni kitu rahisi sana anaujua anacheza kwa kuamini katika kujituma zaidi uwanjani amekuwa bora kwenye kila nafasi anayocheza najifunza mengi kutoka kwake ndiye mwalimu wangu nje ya makocha ninaopita chini yao,” anasema beki huyo ambaye amekiri kuwa sasa anafurahia kucheza nafasi hiyo.

KIUNGO HADI BEKI

Sio kila mchezaji anayefanya vizuri kwenye nafasi anayocheza alianzia hapo japo wapo walianza na nafasi hizo kwa upande wa beki wa Mashujaa anafunguka kutoka kucheza kiungo hadi beki.

“Sijaanza kucheza beki moja kwa moja nilikuwa nacheza eneo la kiungo wa chini au wa juu nilichezeza pia kwa muda mrefu na ni nafasi ambazo nilikuwa naifurahia kucheza;

“Sababu ya kubadili nafasi hadi beki nakumbuka kuna siku tulikuwa na mchezo dhidi ya Kagera Sugar tukiwa chini ya Kocha Salum Mayanga ambaye sasa yupo Mbeya City mabeki wa Ruvu Shooting wote walikuwa wanaumwa basi kocha alikuja akaniambia leo nitakutumia kama beki;

“Kwasababu ni mchezaji sikusita kulipokea hilo niliitumikia hiyo nafasi kwenye mchezo huo ambao nakumbuka ulimalizika kwa sisi kushinda mabao 2-1 tangu siku hiyo mechi ilivyoisha kila mmoja akaniambia unatakiwa kucheza hapo kwasababu nilifanya kazi nzuri safari yangu ya kuwa beki ndio ikaanzia hapo,” anasema.

NIDHAMU INAMBEBA

Kwa asilimia kubwa wachezaji wanaocheza nafasi ya beki ndio wanaongoza kwa kulimwa kadi nyekundu kutokana na kukabiliana zaidi ya washambuliaji lakini kwa beki wa Mashujaa kwake imekuwa tofauti.

“Nimecheza nafasi ya beki kwa miaka mingi sasa lakini suala la kadi nyekundu kwangu limenipita kushoto kwasababu tangu nimeanza soka sijaoneshwa.

“Hii inatokana na nidhamu ya uchezaji naamini katika kukaa kwenye nafasi na kucheza kwa kumheshimu mpinzani wangu mpira ni akili sio nguvu nafikiri hiki ndiko kinanifanya nikwepe kadi,” anasema beki huyo.

FEI TOTO, JOB BALAA

Tanzania imebarikiwa kuwa na viungo wengi tofauti na wachezaji wa nafasi nyingine zote uwanjani wingi wao unasadifu na ubora sio kujazana tu kwenye nafasi kama walivyo wachezaji wa maeneo mengine hilo limethibitishwa na Mtuwi.

“Kuna wachezaji wengi kwenye nafasi ya kiungo lakini kwangu bora ni Feisal Salum ‘Fei Toto’ ni kiungo ambaye anatumia akili na sio nguvu mpira wake ni wa kujiamini na kutekeleza;

“Mbali na nafasi ya kiungo navutiwa pia na uchezaji wa Dickson Job ambaye anacheza beki ya kati kama nimekuwa nikivutiwa na aina ya uchezaji wake, anajiamini na mpambanaji kwaajili ya timu yake anajitoa katika hali zote,” anasema.

USAJILI UTABAMBA

“Ni mapema sana kuzungumzia matukio mazuri na mabaya msimu huu kwasababu ligi bado haijachangamka lakini kitu pekee nilichokiona ni ushindani utakavyokuwa;

“Timu nyingi zimejiandaa vizuri kwa kufanya usajili mzuri, hivyo ligi imekuwa nzuri pia ninavyoona ligi imekuwa bora zaidi timu inapata matokeo uwanja wowote sio kama misimu iliyopita mwenyeji lazima ashinde;

“Waamuzi wa ligi yetu wapo vizuri pongezi kwao ila haya yote yanasababishwa na Azam TV kwa kuonyesha kila mchezo wa ligi yetu pia pongezi wamesaidia kupunguza makosa yaliyokuwa yanajirudia,” anasema beki huyo.

MAYELE HAIJAWAHI KUTOKEA

Fiston Mayele ametimka Tanzania akiwa ameacha historia ya kuwa mshambuliaji mzuri baada ya kutwaa kiatu cha Ligi na Kombe la Shirikisho Afrika lakini hadi sasa anatajwa midomoni mwa mabeki.

“Sijawahi kupata machungu yake nikiwa na maana ya kutufunga lakini ni kati ya washambuliaji ambao wanakera kutokana na kasi yake na nguvu.

“Mabeki hatupendi washambuliaji wenye kasi na nguvu hii nikutokana na kuogopa kuchoshwa na kazi ngumu tunayoifanya kuhakikisha tunamkaba kila mchezaji anayejaribu kuvuka mstari wetu,” anasema.

Mtuwi anasema kabla ya kukutana na Mayele alikuwa anafanya mazoezi ya tofauti zaidi kwasababu anamfahamu ni mchezaji mwenye kasi uwanjani na anacheza soka kwa akili kubwa.

KILICHOISHUSHA RUVU SHOOTING

Ruvu Shooting imeshuka daraja msimu ulioisha.

“Shida nafikiri ilikuwa ni matokeo mabaya ya uwanjani lakini kwa upande wa majukumu ya viongozi walikuwa wanafanya kila kilichokuwa kinawezekana.

“Naumia kuwa mmoja kati ya wachezaji walioishusha timu nimejenga rekodi mbaya kumbukumbu ambayo haiwezi kufutika kwenye maisha yangu hata kwa wadau wa soka ambao wamekuwa wakiifuatilia timu hiyo,” anasema.

NI SITA AU 60

Namba za jezi za wachezaji kuna zenye maana na nyingine zinavaliwa na baadhi ya mastaa kulingana na namna wanavyovutiwa na waliowatangulia huku wengine zikiwa na maana kwenye kumbukizi za matukio ya furaha na huzuni.

“Napenda jezi namba sita na 60 na ndio namba ambazo nimezivaa sana tangu nimeanza kucheza ikiwa inavaliwa moja wapo basi nachukua nyingine.

“Kwangu hazina maana yoyote ni mapenzi tu mfano sita niliipenda sana kutokana na kuanza kucheza kiungo ya chini nilikuwa naipenda sana sasa ni beki nikajikuta naipendelea hivyo hivyo,” anasema Mtuwi.

Chanzo: Mwanaspoti