Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kukaba kwa macho kosa la Singida Big Stars

Singida FG Viingilio.jpeg Kukaba kwa macho kosa la Singida Big Stars

Tue, 3 Oct 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Klabu ya Singida Big Stars jana ilitolewa katika michuano kombe la Shirikisho Afrika baada ya kufungwa 4-1 dhidi ya Future katika mchezo uliochezwa kwenye uwanja wa Al Salaam, Misri.

Singida imetolewa kwa jumla ya mabao 4-2 dhidi ya Future baada ya mchezo wa kwanza uliochezwa hapa nchini kushinda kwa bao 1-0 na ugenini wakalala 4-1.

Timu hiyo katika mechi ya kwanza ilikuwa na kila sababu ya kumaliza mchezo hapa nchini lakini umakini kwenye nafasi ya umaliziaji ulikuwa mdogo.

Katika mchezo wa juzi uliochezwa nchini Misri, Singida ni wazi kabisa eneo lake la ulinzi lilikuwa na shida kutokana na aina ya mabao matatu iliyofungwa kati ya mabao manne ambayo iliruhusu.

Katika eneo hilo hasa beki wa kati ambapo alikuwa anacheza Hamad Waziri 'Kukuu' na Biemes Carno walikuwa wanakaba kwa macho zaidi kuliko kufika kwa mpinzani.

Bao la kwanza lililofungwa na Ahmed Atef dakika ya nne kwa kichwa baada ya kupigwa krosi, beki wa Singida, Biemes Carno aliuangalia mpira bila kuruka wakati huohuo Kuku yeye alimuangalia Atef akifunga mbele yake.

Achana na bao la pili ambalo lilifungwa kwa mkwaju wa penalti.

Bao la tatu ambalo lilifungwa ni beki wake wa kati Biemes Carno kumuacha huru Ahmed Atef ambaye walikuwa sambamba ndani ya boksi lakini alimkaba kwa macho.

Uzembe mwingine ambao mabeki wa Singida walifanya ni kukaba kwa macho katika bao la nne baada ya kupigwa krosi ndefu kwenda kwa Nasser huku wakitega mtego wa kuotea.

Wakati mpira unapigwa, beki wa Singida, Biemes Carno alikuwa anaona mpira unaenda langoni kwao lakini alitoka na kwenda mbele wakati huo, Nasser Maher aliutuliza mpira na kumtoka kipa Beno Kakolanya (Singida BS) na kupiga shuti lililokwenda wavuni.

Kama Biemes angeweza kwenda hadi pale mpira ulipokuwa akiwa sambamba na mchezaji mwenzake, Gadiel Michael ni wazi wangempa wakati mgumu Nasser katika kufunga.

Atef alipigiwa pasi akiwa ndani ya boksi na yeye alipopokea mpira alipiga pasi kwa Ahmed Reffat ambaye alipiga mpira uliokwenda moja kwa moja wavuni.

Wakati huohuo timu hii imefundishwa na makocha watatu tofauti hali ambayo nayo imechangia kuwa na mvurugano wa kimbinu kwa wachezaji kuweza kuzoea kwa nyakati tofauti.

Singida katika mechi za kombe la Shirikisho Afrika imefundishwa na Hans Pluijm, Ernst Middendorp na Ramadhan Nswazurimo.

Akizungumzia mchezo huo, kocha wa sasa Singida BS, Ramadhan Nswazurimo alisema makosa ya walinzi wake kukaba kwa macho ndio yamechangia kufanya vibaya.

"Makosa ya mchezaji mmoja mmoja ndio yamefanya tutolewe, wachezaji walikuwa wanacheza kwa kukaba kwa kutumia macho;

"Ukifika katika hatua hii ukifanya kosa unaadhibiwa, kipindi cha kwanza tulicheza vizuri zaidi."

Nswazurimo alisema walipoteza umakini ndani ya uwanja na kujikuta makosa yakitokea mara kwa mara lakini wanaomba samahani kwa watanzania.

Chanzo: Mwanaspoti