Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kufuzu AFCON 2023: Taifa Stars inapenya hapa

TAIFA STARS SHANGWE 1140x640 Taifa Stars

Mon, 27 Mar 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Timu ya Taifa ya Tanzania, Taifa Stars, imebakiwa na mechi tatu za kusaka nafasi ya kufuzu michuano ya Kombe la Mataifa Afrika (AFCON) inayotarajiwa kufanyika mwakani nchini Ivory Coast.

Ikiwa imepangwa Kundi F, Taifa Stars tayari imecheza mechi tatu dhidi ya Niger, Algeria na Uganda, imejikusanyia pointi nne kutokana na kupata sare dhidi ya Niger, kufungwa na Algeria, kisha kushinda mbele ya Uganda.

Ushindi wa juzi ugenini dhidi ya Uganda kwa bao 0-1, umeifanya Taifa Stars kuhitaji pointi sita ili kushiriki AFCON kwa mara ya tatu katika historia yake.

Nikukumbushe tu kwamba, mchezo wa kwanza ugenini dhidi ya Niger uliochezwa Juni 4, 2022, ulimalizika kwa sare ya bao 1-1, mfungaji wa Taifa Stars akiwa George Mpole ambaye safari hii hayupo kwenye kikosi.

Baada ya hapo, Taifa Stars ikacheza nyumbani dhidi ya Algeria, ilikuwa Juni 8, 2022, ikapoteza kwa mabao 0-2 pale Uwanja wa Mkapa, Dar.

Juzi ugenini dhidi ya Uganda mechi ikichezwa Misri, bao la Simon Msuva dakika ya 68 liliipa ushindi Taifa Stars.

Katika mchezo huo, kiungo wa Taifa Stars, Himid Mao aliumia na kuwa kwenye hatihati ya kuukosa mchezo wa ujao dhidi ya Uganda.

Ukiangalia Kundi F lilivyo, Algeria inaongoza ikiwa na pointi 9 baada ya kushinda mechi zote tatu za kwanza dhidi ya Uganda, Tanzania na Niger.

Mechi mbili zijazo dhidi ya Uganda na Niger ambazo zote zitachezwa Dar, Taifa Stars ikizitumia vema ndiyo itakuwa tiketi ya kushiriki AFCON.

Ushindi katika mechi hizo mbili za nyum¬bani, zitaifanya Taifa Stars kufikisha pointi kumi ambazo zitakuwa salama zaidi kwao kwani Niger na Uganda hazitaweza kuzifikia.

Hiyo inatokana na namna Algeria ilivy¬oonekana kuwa mfupa mgumu zaidi kwa wapinzani wote wa kundi hilo. Kumbuka Algeria imeshinda mechi zote tatu. Mbili nyumbani na moja ugenini.

Wakati Taifa Stars ikiwa nafasi ya pili, Niger inashika nafasi ya tatu ikikusanya pointi mbili, na Uganda inaburuza mkia, haina pointi.

Jumanne ijayo, itakuwa nyumbani kucheza dhidi ya Algeria, hapo wageni Algeria wakipata sare tu, watakuwa wapo kwenye mwendo mzuri zaidi wa kuzidi kuongoza kundi na kufuzu.

Kikosi cha Taifa Stars chini ya Kocha Adel Amrouche raia wa Ubelgiji aliyeteuliwa hivi karibuni, kinapambana kumaliza nafasi mbili za juu kwenye msimamo ili ifuzu.

MSIMAMO KUNDI F P W D L GF GA GD Pts 1. Algeria 3 3 0 0 6 1 +5 9 2. Tanzania 3 1 1 1 2 3 −1 4 3. Niger 3 0 2 1 3 4 −1 2 4. Uganda 3 0 1 2 1 4 −3 1

RATIBA NA MATOKEO JUNI 4, 2022 Niger 1–1 Tanzania Algeria 2–0 Uganda JUNI 8, 2022 Uganda 1–1 Niger Tanzania 0–2 Algeria MACHI 23, 2023 Algeria 2–1 Niger Uganda 0–1 Tanzania MACHI 27, 2023 Niger v Algeria MACHI 28, 2023 Tanzania v Uganda JUNI 2023 Tanzania v Niger Uganda v Algeria SEPTEMBA 2023 Algeria v Tanzania Niger v Uganda.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live