Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kufungwa kwa Singida, Gadiel, Onyango watajwa

Beno Kakolanya Tanga Beno Kakolanya

Thu, 29 Feb 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Singida Fountain Gate imepasuka tena jioni ya Februari 28 mbele ya Azam FC, huku langoni akisimama kipa Beno Kakolanya, lakini mapema kipa huyo amefichua kinachoiangusha timu hiyo kwa sasa ni kuondoka kwa mabeki Joash Onyango na Gadiel Michael.

Singida iliyoweka maskani jijini hapa, imepoteza mechi hiyo ya Ligi Kuu kwa kuchapwa bao 1-0 na kuifanya iendelee na rekodi ya kushindwa kupata ushindi tangu ligi hiyo iliporejea mapema mwezi huu baada ya awali kusimama kupisha michuano ya Kombe la Mapinduzi 2024 na Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon) 2023.

Hiyo ilikuwa ni mechi ya saba kwa Singida kucheza kwenye ligi bila ushindi, lakini kabla ya mchezo huo wa leo kipa Kakolanya alisema kuondoka kwa Onyango na Gadiel aliyepo Afrika Kusini, kumevuruga eneo la beki hadi kuruhusu idadi kubwa ya mabao.

Onyango kwa sasa yupo Ihefu na baadhi ya mastaa wengine waliokuwa Singida na ilianza msimu wa Ligi Kuu ikiwa na kasi kabla ya mambo kubadilika tangu dirisha dogo lifungwe Januari 15 mwaka huu na na Kakolanya aliwataja wachezaji hao waliondoka kikosini wameidhoofisha timu.

Miongoni mwa walioondoka hasa eneo la beki ni Onyango (Ihefu) na Gadiel ambaye alitolewa kwa mkopo Cape Town Spurs ya Afrika Kusini, huku Yusuph Kagoma akiwa hajarejea vyema kutokana na majeraha, huku Elvis Rupia, Marouf Tchakei, Khomein Aboubakari, Morice Chukwu na Duke Abuya wakitimkia pia Ihefu.

Katika mechi tatu za mwisho ukuta wa timu hiyo umejengwa na Kelvin Kijili, Amos Kadikilo, Yahya Mbegu na Nicholas Wadada upande wa pembeni huku kati wakicheza Biemes Carno, Ahmad Waziri na Ibrahim Makame.

Hadi sasa katika mechi walizocheza Ligi Kuu, Singida wameruhusu mabao manne ikiwa ni kupoteza mchezo mmoja dhidi ya Prisons 3-1 na sare ya 1-1 dhidi ya Tabora United.

Kipa na Nahodha wa timu hiyo, Beno Kakolanya amesema kuondoka kwa mabeki hao kumeifanya eneo hilo kuyumba kidogo akieleza kuwa kwa sasa wanaanza kujipata taratibu.

“Ukiangalia hata nyuma (mabeki) kuna mtikisiko watu wa katikati pale nafikiri muda unavyokwenda tutakaa vizuri kwani kocha anaendelea kuwaandaa waingie kwenye mfumo,” amesema kipa huyo wa zamani wa Tanzania Prisons, Yanga na Simba.

Nyota huyo anayeichezea pia timu ya taifa, Taifa Stars ameongeza matarajio yao ni kurejesha kasi yao kwani wameanza kuona mabadiliko tangu mchezo wa Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC) waliposhinda 2-0 dhidi ya Mbeya City, japo jioni ya leo imekumbana na kipigo kingine.

Chanzo: Mwanaspoti