Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kufungiwa kocha Morocco, CAF inajiosha?

Regragui.jpeg Kufungiwa kocha Morocco, CAF inajiosha?

Sat, 27 Jan 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Hamu kubwa ya CAF kumuadhibu kocha Walid Regragui imechangiwa na nia ya shirikisho hilo la soka Afrika kujaribu kuonyesha kwamba linajitegemea kufuatia tuhuma, ambazo hazina ushahidi, kwamba “linaburuzwa kindezi” na Morocco.

Hivi karibuni, kocha wa timu ya taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’, Adel Amrouche alidai kwamba Morocco ina nguvu kubwa Caf kiasi kwamba inajipangia waamuzi wa kuchezesha mechi zao ili wawapendelee.

Kufutia kauli hiyo, Shirikisho la Soka la Tanzania (TFF) lilijiweka kando ya kauli hizo likisema hayo ni maoni binafsi ya kocha huyo mwenye uraia pacha wa Algeria na Ubelgiji.

Wengine wanaona kwamba Amrouche alichokiongea kinachangiwa na mvutano wa kisiasa uliopo kati ya nchi yake ya asili ya Algeria na Morocco.

Kwa mujibu wa mchambuzi wa Morocco Media News, Safaa Kasraoui, ugomvi wa uwanjani baina ya kocha wa timu ya taifa ya Morocco, Walid Regragui na beki wa DR Congo, Chancel Mbemba, umehukumiwa kisiasa na CAF.

Regragui alifungiwa mechi nne na kutozwa faini dola 5,000 (sawa na Sh12.5 milioni).

Mashabiki wa Morocco wamehoji kuhusu haki na ‘taimingi’ ya adhabu hiyo ya Caf.

Saa chache kabla ya mechi ya makundi Afcon katia ya Morocco na Zambia, mashabiki wa Morocco walishtushwa na uamuzi wa Caf wa kumfungia kocha wao mkuu Walid Regragui mechi nne.

Kwa uamuzi huu, Regragui anayesifika kwa uungwana, akaadhibiwa kwa uhusika wake katika ugomvi na Mbemba.

Kiujumla, wanaonekana kuhoji kwanini kocha wa Morocco amepewa adhabu kubwa wakati Mbemba ameachwa huru na atacheza mechi ijayo ya DR Congo dhidi ya Misri Jumapili hii.

Mashabiki wengine wameichukulia uzito zaidi adhabu hiyo ya Caf kwa kufanya mambo tofauti kwenye mitandao ya kijamii, ikiwamo kuweka hashtag mfululizo za kuelezea kumsapoti kocha wa Morocco.

Moja ya hashtags hizo ni ile ya “Tunasimama na Regragui.”

Mashabiki wengi pia wamedai kwamba adhabu hiyo ya Caf imetolewa ili kujaribu kuonyesha kwamba shirikisho hilo la soka “halijashikwa masikio” na Morocco.

“Katika kutaka kuwathibitishia wakosoaji kwamba Morocco haijaishika masikio Caf, imeamua kumpa adhabu kali ya kumfungia Regragui. Tangu lini kocha anafungiwa mechi 4 katika michuano kwa kwenda tu kumsalimia mchezaji uso kwa uso?” shabiki aliandika.

Chaneli rasmi ya TV ya Algeria ya Al Ikhbariya 3, ilidai kuwa Mbemba alibadili jina la utani la timu ya taifa ya Morocco la ‘Simba wa Atlas’ kwa kuwaita “Mafisi” wanaojificha nyuma ya kivuli cha simba.

Wengine wakadai kwamba kitendo kilichofanywa na Caf kimelenga kuipa presha ya kisaikolojia Morocco, ambayo itakabiliana na nchi ya Rais wa Caf, Patrice Motsepe ya Afrika Kusini katika hatua ya 16 bora ya Afcon Januari 30.

Chanzo: Mwanaspoti