Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kufunga hat-trick Ujerumani kazi sana

Harry Kane Perfect Kufunga hat-trick Ujerumani kazi sana

Tue, 12 Mar 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Straika Harry Kane yupo kwenye makali kama ya kiwembe huko Bayern Munich msimu huu.

Staa huyo wa England alifunga mara tatu wakati Bayern iliposhusha kipigo cha mabao 8-1 dhidi ya Mainz katika mikikimikiki ya Bundesliga wikiendi iliyopita.

Katika mchezo huo, Kane aliasisti pia mara moja, bao lililofungwa na Jamal Musiala na kuzidi kudhihirisha kwamba Bayern haikufanya makosa ilipolipa pesa nyingi kunasa saini yake mwaka jana.

Mabao hayo matatu yamemfanya Kane sasa amwe amefunga mara 30 kwenye Bundesliga na hivyo kuwa na mwanzo matata kabisa kwenye soka la Ujerumani.

Kane alifungua ukurasa wa mabao wa Bayern kwa kufunga dakika 13, kabla ya staa anayewindwa na Manchester United, Leon Goretzka kufunga la pili sekunde sita baadaye.

Nadiem Amiri aliifungia mara moja Mainz, kabla ya Kane kufunga la pili kwake na tatu kwa Bayern sekunde chache kabla ya filimbi ya mapumziko. Kipindi cha pili, baada ya dakika mbili tu, Thomas Muller alifunga mabo la nne, kabla ya Musiala kufunga la tano na Serge Gnabry la sita.

Kane alikamilisha bao lake la tatu dakika 70 alipofunga kwa kichwa, kabla ya Goretzka kufunga tena na kukamilisha idadi hiyo ya mabao manane katika dakika ya 93.

Kane amekuwa kiboko ya nyavu huko Ujerumani, ambapo hadi sasa ameshafunga mabao 36 katika mechi 34 alizocheza katika michuano yote. Hii ilikuwa mara ya nne tofauti kufunga mara tatu kwenye mechi moja.

Hata hivyo, licha ya kufunga mabao yanayofahamika kama hat-trick, huko Ujerumani mambo ni tofauti.

Huko Ujerumani, hat-trick ni ile kwamba mfungaji anapofunga bao la kwanza, basi afunge kwenye kipindi kimoja na afunge kwa kufuata, asitokee mchezaji mwingine wa timu yake akafunga bao katikati yake.

Hivyo, kwa kesi ya wikiendi, ambapo Kane alifunga bao la kwanza, la tatu na saba, hivyo haiwezi kuhesabika kama hat-trick.

Chanzo: Mwanaspoti