Nahodha Msaidizi wa Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Simba SC Mohamed Hussein ‘Tshabalala’ amesema wameshasahau kilichotokea Afrika Kusini, na sasa wamejikita kwenye maandalizi ya mchezo wa Ligi Kuu dhidi ya Young Africans, Jumamosi (April 30).
Tshabalala ambaye amekiongoza kikosi cha Simba SC katika michezo kadhaa msimu huu, kufuatia Nahodha na Mshambuliaji John Raphael Bocco kuwa majeruhi mara kwa mara, amesema hakuna kingine kwa sasa zaidi ya kuhakikisha wanapambana dhidi ya Young Africans na kupata alama tatu.
“Hakuna cha ziada kwa sasa zaidi ya kujiandaa na mchezo wetu dhidi ya Young Africans Jumamosi, yaliyopta yameshapita, ukiwa kama mchezaji unatakia kusahau ya nyuma na kufikiria yaliyo mbele yako.”
“Simba SC kuna watu makini sana, tunajua nini maana ya kushindwa na kushinda, kilichotokea Afrika Kusini Jumapili, ni sehemu ya matokeo ya mchezo wa soka, kwa sasa tunaamini lililo mbele yatu ndio halali yetu kulikabili.” amesema Tshabalala
Simba SC inakwenda kupambana na Young Africans Jumamosi (April 30), huku ikiwa na matarajio hafifu ya kutetea taji lake la Ligi Kuu msimu huu 2021/22, kufuatia tofauti ya alama ilopo kati ya klabu hizo za Kariakoo.
Young Africans iliyocheza michezo 20 hadi sasa inaongoza msimamo wa Ligi Kuu kwa kuwa na alama 54, huku Simba SC iliyocheza michezo 19 ikiwa nafasi ya pili kwa kumiliki alama 41.