Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

#KuelekeaDERBYDay: Subirini mtajua hamjui

Simba Yanga Pic Mashabiki watambiana kuelekea mchezo wa Jumamosi

Wed, 8 Dec 2021 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Kila muda unavyosogea kuifikia Disemba 11, Joto la Dabi ya Kariakoo linazidi kupanda kwa majigambo, tambo na kila aina ya majisifu baina ya mashabiki wapande hizo mbili.

Simba ndio wenyeji wa mchezo huo uliopangwa kuchezwa kwenye uwanja wa Benjamin Mkapa kuanzia saa 11:00 jioni na wataingia wakiwa na kumbukumbu ya kupoteza kwa kufungwa bao 1-0 walipokutana na Yanga kwenye mchezo wa mwisho wa Ngao ya Jamii.

Ofisa Habari wa Yanga, Hassan Bumbuli pamoja na Kaimu Ofisa Habari wa Simba Ally Shatry maarufu Chico ndio wameziwakilisha timu zao katika mkutano wa waandishi wa habari uliofanyika kwenye makao makuu ya Shirikisho la mpira wa miguu Tanzania ‘TFF’ leo asubuhi.

Kwa upande wa Yanga anmbao ni wageni, Bumbuli amesema kuwa timu yao msimu huu ipo kwenye kiwango bora zaidi na inatarajia kushinda mchezo huo na kuendelea kukaa kileleni mwa msimamo wa ligi.

“Tupo tayari kwa mchezo, mashabiki wamehamasika na tunatarajia ushindi Jumamosi.

Maandalizi yote yamekamilika na sasa tunasubiri muda ufike, hadi sasa majeruhi ni mmoja tu, Yacouba Songne lakini wengine wote wapo timamu tayari kupambania alama tatu muhimu,” amesema Bumbuli na kuongeza; Advertisement

“Mashabiki wa timu yetu wajitokeze uwanjani kifua mbele kwani tunaenda kushinda na kuendelea kuufukuzia ubingwa wa ligi msimu huu,” amesema.

Naye Chico kwa niaba ya Simba amefunguka kuwa wamejipanga kuichapa Yanga na kila kitu kinaendelea vizuri baada kutoka Zambia kucheza mchezo wa Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Red Arrows na kupoteza kwa bao 2-1 lakini wakatinga hatua ya makundi ya mashindano hayo kwa jumla ya mabao 4-2 wakiwa wameshinda bao 3-0 nyumbani kwenye mechi ya kwanza.

“Mchezo uliopita dhidi ya Yanga tulipoteza na hatupo tayari kupoteza mchezo wa Jumamosi hivyo mashabiki wetu wajitokeze kwa wingi uwanjani wakati tukienda kushinda na kuongoza ligi,” amesema Chico na kuongeza;

“Tumeanza mazoezi ya mechi hii tangu tupo Zambia na leo tutaendelea tulipoishia. Wachezaji wote wako fiti na morali yao ipo juu kuelekea mechi hiyo na watani,” amesema.

Mshindi katika mchezo huyo ndiye ataongoza ligi baada ya hapo kwani Yanga ipo kileleni na pointi 19 huku Simba wakiwa nafasi ya pili na pointi 17, timu zote mbili zikiwa zimecheza mechi saba hadi sasa.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live