Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kopunovic yupo kwenye kipimo cha Pamba

 Kocha Goran Kopunovic .png Kocha Kopunovic

Fri, 21 Jun 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Dirisha la usajili linazidi kuchangamka na jamaa zetu wa Pamba FC wao wameanza kwa utambulisho wa kocha mkuu Goran Kopunovic kutoka Serbia.

Kocha huyo anachukua nafasi ya Mbwana Makata ambaye pamoja na kuipandisha daraja timu hiyo, imeamua kutoendelea naye na kuamua kumchukua kocha huyo wa zamani wa Simba.

Kabla ya kujiunga na Pamba FC, timu ya mwisho kwa Kopunovic kufundisha ilikuwa ni Tabora United ambayo nayo alijiunga nayo ikiwa ndiyo imetoka kupanda ligi kuu kama ilivyo kwa timu hiyo kutoka jijini Mwanza.

Kitendo cha Pamba kumchukua Kopunovic ni mtihani na mtego mkubwa kwa kocha huyo kutokana na historia ya kile alichokifanya hapo nyuma pindi alipokuja nchini kufundisha soka katika klabu tofauti.

Alipoifundisha Simba, alifanya vizuri japo hakuiwezesha kutwaa ubingwa kwa vile aliikuta ipo katika hali mbaya na kuiwezesha kumaliza nafasi tatu za juu kwenye msimamo wa ligi na wengi walitamani kuona akiendelea kuinoa timu hiyo enzi hizo.

Tabora United ilipomchukua mambo yakawa tofauti kwani haikufanya vizuri na kusababisha iwe katika nafasi mbaya kwenye msimamo wa ligi jambo ambalo lilifanya uongozi wa timu hiyo kuamua kumtimua.

Ndani ya Tabora United, Kopunovic alipata utetezi mkubwa kwa vile ilionekana kutofanya vizuri kumechangiwa na changamoto za kiutawala zilizosababisha timu isiwe na mwenendo mzuri kwenye ligi.

Hivyo kwa sasa watu tunatamani kuona nini Kopunovic atakifanya Pamba kama ni kuiwezesha kufanya vizuri kama ilivyokuwa kwa Simba au kuchemsha kama ilivyotokea kwa Tabora United.

Pamba ni timu inayoweza kutegua kitendawili cha ubora wa Kopunovic kama ni kocha wa daraja la juu au naye ni muomba Mungu tu.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live