Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kombe la Muungano sawa, ila twende mbali zaidi ya hapo

Simba, Yanga Warejea Ligi Kuu Wikiendi Hii Kombe la Muungano sawa, ila twende mbali zaidi ya hapo

Tue, 13 Feb 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Kwa mujibu wa ratiba ya ligi iliyotolewa na Bodi ya Ligi Kuu (TPLB), baada ya Kombe la Mapinduzi na mapumziko ya Afcon, itasimama kati ya Aprili 23 na 26 kwa ajili ya Kombe la Muungano.

Mashindano hayo maalumu ya kuenzi miaka 60 ya Muungano, yatafanyika visiwani Zanzibar kwenye Uwanja wa New Amaan Sports Complex.

Timu nne za Bara na nne za Zanzibar zitashiriki katika mtoano kama ilivyochezwa African Football League, hadi kufikia fainali.

Mashindano haya ni muhimu sana kwa kujenga umoja wetu wa kitaifa sisi kama Watanzania ingawa hata hivyo tunaweza kufanya zaidi ya hapo na kupata kitu kizuri endelevu.

Badala ya kuwa na mashindano ya bonanza kama hayo, tuwe na mfumo rasmi utakaofanya kuwe na mashindano yatakayoshirikisha timu kutoka Tanzania nzima kwa maana (bara na visiwani) ambayo yatatoa nafasi za ushiriki wa mashindano ya Afrika.

TUFUNGUE MIPAKA

Sisi kama taifa bado tunakumbatia mifumo ya kikoloni inayotutenganisha kwa sababu hakuna ligi moja inayoweza kutufanya Watazania tukacheza pamoja.

Mwaka 2000 kwenye kilele cha UMITASHUMTA iliyofanyika Morogoro, Rais wa Jamhuri ya Muungano (awamu ya tatu), Benjamin William Mkapa (marehemu) aliyekuwa mgeni rasmi, alitoa wito kwa waandaaji wa michezo ile kuhakikisha inakuwa na sura ya Muungano ili watoto wetu wacheze pamoja.

Bahati mbaya mwaka mmoja baadae, yaani 2001 UMITASHUMTA (pamoja na UMIISETA) ikasimama kabisa, hadi 2006 wakati Mkapa mwenyewe alipotoka madarakani na hata iliporudi wakati wa awamu ya nne chini ya Kikwete, haikuwa na sura ile aliyoitaka Mkapa na hiki ndicho ninachokijadili hapa.

Tuwe na ligi moja itakayoshirikisha timu za bara na visiwani kama ilivyokuwa ligi ya Muungano iliyoanza 1982 na kufa 2003.

Sio lazima kuunganisha ligi zilizopo, hapana. Hizi ligi zinaweza kuendelea kama zilivyo ila ziondoe ile kanuni ya ovyo inayokataza timu za upande mmoja kushiriki ligi ya upande mwingine.

Ligi iwe wazi kwa timu zinazotaka kutoka upande wowote kujisajili upande mwingine na kupata nafasi ya kushiriki bila ya kikwazo.

Hiki ndicho wanachofanya wenzetu kama England ambao timu zao kutoka Wales yaani Cardiff City na Swansea City zinashiriki EPL.

Walichofanya wenzetu ni kuweka milango wazi kwa timu kujisajili inakotaka na kufuata michakato yote inayotakiwa ikiwemo kuanzia madaraja ya chini.

Yaani Cardiff City na Swansea City, zilisajiliwa England na FA na zikaanzia ligi ya chini kabisa hadi zilipo sasa.

Hii ina maana Mlandege ya Zanzibar inaweza kujisajili bara na kuanzia ligi daraja la nne hadi ifike Ligi Kuu Bara na kushiriki.

Au Singida Fountain Gate ya bara inaweza kwenda kujisajili ZFF na kuanzia ligi daraja la nne hadi kufika Ligi Kuu ya Zanzibar.

Zanzibar na Bara ni Tanzania moja, kama Wales na England ambazo ni UK (United Kingdom) moja ila ukiacha nchi kama hizi zenye historia ya udugu, kuna nchi zingine ambazo hazina uhusiano kama huu ila zinafanya hivyo.

Kwa ndani Ujerumani inaruhusu timu kutoka kwa majirani zake Austria na Poland kushiriki ligi yao japo hazijapanda ligi kuu lakini zipo kadhaa kutoka nchi hizo mbili zinazoshiriki kwenye ligi za Ujerumani za madaraja tofauti tofauti.

Tanzania tumemuuza kijana wetu, Cyprian Kachwele kwenda Canada kwenye timu ya Vancouver White Caps ingawa ni timu inayoshiriki Ligi ya Marekani, MLS.

Sio kwamba Canada hakuna ligi, la hasha. Ni kwamba Marekani imefungua mipaka kwa majirani zake kushiriki ligi yao na kama majirani tu wanaweza, sisi ndugu tunashindwa nini?

Hivi Karibuni kulikuwa na mjadala mkubwa kufuatia taarifa za Simba kuomba kutumia Uwanja wa New Amaan Sports Complex kama uwanja wao wa nyumbani baada ya kufungwa kwa Uwanja wa Uhuru ambao ndio ulikuwa unatumika kwa michezo ya nyumbani.

Hapo hapo zikaanza kunukuliwa kanuni kadhaa zinazokataza timu za Bara kutumia viwanja visivyo vya Bara kwenye Ligi Kuu Bara.

Kama tunataka kuutumia mpira kutuunganisha kama taifa, tusiishie kwenye mabonanza kama Kombe la Mapinduzi na Kombe la Muungano, tuwe na mashindano rasmi yatakayoubeba Muungano wetu mgongoni na kutuunganisha sisi wenyewe Watanzania.

Chanzo: Mwanaspoti