Kocha wa Portsmouth, John Mousinho ameripotiwa kutaka beki wa kimataifa wa Tanzania, Haji Mnoga kuwa sehemu ya kikosi chake kwa ajili ya maandalizi ya msimu ujao wa Ligi Daraja la Pili England 'EFL League One'.
Mnoga alifanya vizuri msimu uliopita katika klabu ya Aldershot ambayo alikuwa akiichezea kwa mkopo kwenye Ligi ya Taifa tangu Januari, akicheza mara 17 huku akiteuliwa mara mbili kama mchezaji bora wa mwezi.
Kufanya vizuri kwa nyota huyo, kumeripotiwa kumechochea maamuzi ambayo ameyafanya Mousinho kutaka kumtazama kwenye maandalizi hayo ya msimu ujao ili kuona kama anaweza kuwa sehemu ya mipango yake.
Kocha huyo mkuu aliteuliwa siku chache baada ya Mnoga kuhusishwa na Aldershot kwa muda uliosalia wa msimu na hivyo hajawahi kumuona mazoezini.